84. SURAT AL-INSHIQAAQ
(Imeteremka
Makka)
Sura hii imetaja baadhi ya
ishara za Saa ya Kiyama, na kunyenyekea ardhi na mbingu kufuata atakavyo
Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na imefahamisha kwamba mtu anachungwa ende akakutane na
Mola wake Mlezi, na kwamba vitendo vyake vimeandikwa katika daftari atakalo
kuja likuta. Basi mwenye kulipokea kwa mkono wake wa kulia, hisabu yake itakuwa
nyepesi. Na mwenye kulipokea kwa mkono wa kushoto atayayatika kuipata adhabu na
kuingia Motoni. Tena Mwenyezi Mungu Subhanahu ameapa kwa Ishara ambazo
zinashuhudia uweza wake, na ambazo zinaitia imani ya kufufuliwa. Lakini juu ya
hayo walio kufuru hawaamini, wala hawaizingatii Qur'ani, wala hawazifuati
hukumu zake. Kisha Sura inakhitimisha kwa kuonya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua
wanayo dhamiria, na kwamba Yeye amekwisha waandalia adhabu iliyo chungu, kama
alivyo waandalia Waumini ujira wa daima usio katika.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1.Itapo chanika mbingu,
2. Na ikamsikiliza Mola wake Mlezi, na ikapasiwa
kumsikiliza,
3. Na ardhi itakapo tanuliwa,
4. Na kuvitoa vilivyo kuwa ndani yake, ikawa tupu,
5. Na ikamsikiliza Mola wake Mlezi, na ikapasiwa
kumsikiliza,
6. Ewe mtu!
Hakika wewe unajikusuru kwa juhudi kumwendea Mola wako Mlezi, basi utamkuta.
7. Ama
atakaye pewa daftari lake kwa mkono wa kulia,
8. Basi
huyo atahisabiwa hisabu nyepesi,
9. Na arudi kwa ahali zake na furaha.
10. Na ama atakaye pewa daftari lake kwa nyuma ya mgongo
wake,
11. Basi huyo ataomba kuteketea.
12. Na ataingia Motoni.
13. Hakika alikuwa furahani kati ya jamaa zake.
14. Huyo hakika alidhani kuwa hatarejea tena.
15. Kwani?
Hakika Mola wake Mlezi alikuwa akimwona!
16. Basi
ninaapa kwa wekundu wa jua linapo kuchwa,
17. Na kwa
usiku na unavyo vikusanya,
18. Na kwa mwezi unapo pevuka,
19. Lazima mtapanda t'abaka kwa t'abaka!
20. Basi wana nini hawaamini?
21. Na wanapo somewa Qur'ani hawasujudu?
22. Bali walio kufuru wanakanusha tu.
23. Na Mwenyezi Mungu anajua wanayo yadhamiria.
24. Basi wabashirie adhabu chungu!
25. Isipo kuwa wale walio amini na wakatenda mema; hao
watakuwa na ujira usio malizika.
|