90. SURAT AL-BALAD
(Imeteremka
Makka)
Mwenyezi Mungu anaapa kwa
mji mtakatifu wa Makka, mji wa kuzaliwa Muhammad s.a.w. na ndipo alipo kulia na
akapapenda, na pia anaapa kwa mzazi na anacho kizaa, kwani kwa hao ndio jinsi
inahifadhika na maamrisho yanabakia, na ya kwamba mtu ameumbwa kwa mashaka na
shida na taabu. Tena anabainisha kwamba mtu anadanganyika kwa kudhani kuwa
uweza wake haushindiki, na kwamba yeye ana mali mengi anayo yatumia kuridhisha
matamanio yake na pumbao lake. Kisha Subhanahu akazitaja neema alizo mneemesha
mwanaadamu na kumsahilishia njia za uwongofu na za kupitia milimani, ili awe
katika watu wa Peponi, watu wa mkono wa kulia, na aikimbie njia ya kumpelekea
kuwa katika watu wa kushoto ambako itawatumbukiza Motoni na kufungiwa milango.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Naapa kwa Mji huu!
2. Nawe unaukaa Mji huu.
3. Na naapa kwa mzazi na alicho kizaa.
4. Hakika tumemuumba mtu katika taabu.
5. Ati anadhani hapana yeyote ataye muweza?
6. Anasema: Nimeteketeza chungu ya mali.
7. Ati anadhani ya kuwa hapana yeyote anaye mwona?
8. Kwani hatukumpa macho mawili?
9. Na ulimi, na midomo miwili?
10. Na tukambainishia zote njia mbili?
11. Lakini hakujitoma kwenye njia ya vikwazo vya milimani.
12. Na nini kitakujuvya ni nini njia ya vikwazo vya
milimani?
13. Kumkomboa
mtumwa;
14. Au kumlisha
siku ya njaa
15. Yatima aliye
jamaa,
16. Au masikini
aliye vumbini.
17. Tena awe miongoni mwa walio amini na wakausiana
kusubiri na wakausiana kuhurumiana.
18. Hao ndio watu wa kheri wa kuliani.
19. Lakini walio zikataa Ishara zetu, hao ndio watu wa
shari wa kushotoni.
20. Juu yao utakuwa Moto ulio fungiwa kila upande.
|