94. SURAT ASH-SHARH'
(Imeteremka
Makka)
Inathibitisha Sura hii
kwamba Mwenyezi Mungu ameukunjua moyo wa Nabii wake, na akaufanya ndipo pahala
pa kuteremkia siri na ilimu, na akaondoa matatizo yaliyo kuwa yakimthakilisha
mgongo wake, nayo ni katika mizigo ya kazi ya Da'wa, yaani Wito. Na
akalikutanisha jina lake Mwenyezi Mungu na jina lake Mtume katika asli ya Imani
na alama za Dini. Kisha Aya hizi zikataja sunna ya Mwenyezi Mungu ya
kuambatisha mepesi na mazito, dhiki na faraji, na zikamtaka Mtume kila anapo
pata nafasi kutokana na kutenda kheri, atende kheri nyengine, na afanye lengo
lake ni Mola wake Mlezi, kwani Yeye ni Muweza wa kumsaidia.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Hatukukunjulia kifua chako?
2. Na tukakuondolea mzigo wako,
3. Ulio vunja mgongo wako?
4. Na tukakunyanyulia utajo wako?
5. Basi kwa hakika pamoja na uzito upo wepesi,
6. Hakika pamoja na uzito upo wepesi.
7. Na ukipata faragha, fanya juhudi.
8. Na Mola wako Mlezi ndio mshughulikie.
|