95. SURAT AT-TIN
(Imeteremka
Makka)
Mwenyezi Mungu anaapa
katika Sura hii kwa matunda mawili yenye baraka, na pahala pawili pazuri, ya
kwamba Yeye hakika amemuumba mtu kwa njia kunjufu kabisa, kwa kumkamilishia
akili, na uwezo wa kutaka na kutotaka, na mengineyo katika sifa za ukamilifu.
Kisha Aya zikataja kuwa mtu hakusimama kwa mujibu wa alivyo umbiwa, bali
akateremka kwa daraja mpaka akawa wa chini kabisa, isipo kuwa walio amini na
wakatenda mema kati yao. Hao Mwenyezi Mungu amewakunjulia vipawa. Kisha Sura
imewageukia kuwakemea wanao kadhibisha kufufuliwa baada ya kudhihiri dalili
zote za uweza wa Mwenyezi Mungu na khabari za hikima yake.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Naapa kwa tini na zaituni!
2. Na kwa Mlima wa Sinai!
3. Na kwa mji huu wenye amani!
4. Bila ya shaka tumemuumba mtu kwa umbo lilio bora kabisa.
5. Kisha tukamrudisha kuwa chini kuliko walio chini!
6. Lakini wale walio amini na wakatenda mema, hao watapata
ujira usio kwisha.
7. Basi ni kipi baadaye kitacho kukukadhibishia malipo?
8. Kwani Mwenyezi Mungu si muadilifu kuliko mahakimu wote?
|