96. SURAT AL-A'LAQ
(Imeteremka
Makka)
Katika Sura hii upo wito wa
kusoma na kujifunza, na kwamba aliye weza kumuumba mtu kutokana na asli nyonge
ni Mweza wa kumfunza kuandika kwa kudhibitia ilimu na kutimizia kufahamu, na
amfunze aliyo kuwa hayajui. Kwani Yeye Subhanahu ndiye Mwenye kummiminia ilimu
mwanaadamu. Na Sura inanabihisha kwamba utajiri na nguvu huenda zikampelekea
mtu kupindukia mipaka ya Mwenyezi Mungu, lakini marejeo ya wote ni kwa Mwenyezi
Mungu mwishoni. Na mazungumzo yanamwelekea kila mwenye kusilihi kusemezwa
kuwaonya hao majeuri wanao pinga kheri, kuwaonya kuwa watakuja kushikwa kwa
nywele zao za utosi wakibururwa Motoni; na hawatofaliwa na wasaidizi wowote. Na
Sura inakhitimisha kwa kuwataka wasikivu wende kinyume na hao wenye inda wanao
kadhibisha, na wajijongeze kwa ut'iifu kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba,
2. Amemuumba binaadamu kwa tone la damu,
3. Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote!
4. Ambaye
amefundisha kwa kalamu.
5. Kamfundisha
mtu aliyo kuwa hayajui.
6. Kwani!
Hakika mtu bila ya shaka huwa jeuri
7. Akijiona
katajirika.
8. Hakika kwa
Mola wako Mlezi ndio marejeo.
9. Umemwona yule
anaye mkataza
10. Mja
anapo sali?
11. Umeona kama yeye yuko juu ya uwongofu?
12. Au anaamrisha uchamngu?
13. Umeona kama yeye akikanusha na anarudi nyuma?
14. Hajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anaona?
15. Kwani!
Kama haachi, tutamkokota kwa shungi la nywele!
16. Shungi la uwongo, lenye makosa!
17. Basi na awaite wenzake!
18. Nasi tutawaita Mazabania!
19. Hasha!
Usimt'ii! Nawe sujudu na ujongee!
|