98. SURAT AL-BAYYINAH
(Imeteremka
Madina)
Watu wa Kitabu, yaaani
Mayahudi na Wakristo, wamejua kutokana na Vitabu vyao, na washirikina wa Makka
wakajua kutokana nao sifa za Nabii wa zama za mwisho. Na yalikuwa yanatakikana
kutokana na hayo ni kuwa wamuamini huyo Nabii pindi akiteuliwa. Lakini alipo
teuliwa miongoni mwao Mtume wa Mwenyezi Mungu mwenye kuungwa mkono na Qur'ani,
walikhitalifiana na wakaacha ahadi yao. Na vitendo vya Watu wa Kitabu katika
hayo vilikuwa viovu zaidi kuliko vya washirikina. Na hukumu ya watu hawa wote
Akhera ni kukaa milele katika Moto. Na Waumini, watu wa vyeo vya juu kwa
fadhila, ndio bora wa viumbe. Malipo yao ni kukaa milele Peponi, na kuridhika
kwa kuyapata wayatakayo na kupewa wanayo yapenda. Hii ndiyo neema ya mwenye
kumkhofu Mola wake Mlezi.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Hawakuwa walio kufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu na
washirikina waache walio nayo mpaka iwajie bayana,
2. Yaani Mtume aliye toka kwa Mwenyezi Mungu anaye wasomea
kurasa zilizo takasika,
3. Ndani yake mna maandiko yaliyo nyooka.
4. Wala hawakufarikiana walio pewa Kitabu ila baada ya
kuwajia hiyo bayana.
5. Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa
kumtakasia Dini, wawe waongofu, na washike Sala, na watoe Zaka. Na hiyo ndiyo
Dini madhubuti.
6. Hakika walio kufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu na
washirikina wataingia katika Moto wa Jahannamu wadumu milele humo. Hao ndio
viumbe waovu kabisa.
7. Hakika walio amini na wakatenda mema, hao ndio bora wa
viumbe.
8. Malipo yao kwa Mola wao Mlezi ni Bustani za daima,
zipitazo mito kati yake. Wakae humo milele. Mwenyezi Mungu yu radhi nao, na wao
waradhi naye. Hayo ni kwa anaye mwogopa Mola wake Mlezi.
|