107. SURAT AL-MAAU'N
(Imeteremka
Makka)
Sura hii inahadithia
khabari za mwenye kukadhibisha malipo ya Akhera. Ikataja katika sifa zake kuwa
yeye anamdhalilisha yatima, na anamkemea kwa ukali, si kwa kumtengeza. Na
kwamba yeye hamhimizi mtu yeyote, la kwa kauli wala kwa kitendo, kuwalisha
masikini; kwa sababu huyo ni mchoyo kwa mali yake, bakhili kwa alicho nacho
mkononi. Kisha Sura imewataja watu wa kikundi kingine wanao shabihiana na hawa
wanao kadhibisha malipo. Hawa ni wale wanao ghafilika na Sala zao, ambao
hawasali kama itakikanavyo, na ambao husimama kwa hayo kwa dhaahiri tu si kwa
hakika. Ni wenye kuonyesha tu a'mali zao, wenye kuzuia msaada wao wasiwape
wanao hitajia. Na Sura inawaahidi hao kuwa watapata misiba na maangamio,
ili waache uasi wao.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Je! Umemwona
anaye kadhibisha Malipo?
2. Huyo ndiye
anaye msukuma yatima,
3. Wala hahimizi
kumlisha masikini.
4. Basi, ole wao wanao sali,
5. Ambao wanapuuza Sala zao;
6. Ambao
wanajionyesha,
7. Nao
huku wanazuia msaada.
|