151 - 200
151. Kama tulivyo mtuma Mtume kwenu anaye tokana na nyinyi,
anakusomeeni Aya zetu na kukutakaseni na kukufundisheni Kitabu na hikima na
kukufundisheni mliyo kuwa hamyajui.
152. Basi nikumbukeni nitakukumbukeni, na nishukuruni wala
msinikufuru.
153. Enyi mlio amini! Takeni msaada kwa subira na Sala.
Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri.
154. Wala msiseme kuwa wale walio uwawa katika Njia ya
Mwenyezi Mungu ni maiti; bali hao ni wahai, lakini nyinyi hamtambui.
155. Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na
njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanao subiri,
156. Wale
ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye
hakika tutarejea.
157. Hao juu
yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao Mlezi na rehema. Nao ndio wenye
kuongoka.
158.
Hakika vilima vya Safaa na Marwa ni katika alama za Mwenyezi Mungu. Basi anaye
hiji kwenye Nyumba hiyo au akafanya Umra, si kosa kwake kuvizunguka. Na anaye
jitendea mwenyewe kheri basi bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye shukrani na
Mjuzi.
159.
Hakika wale wanao ficha tuliyo yateremsha -- nazo ni hoja zilizo wazi na
uwongofu baada ya Sisi kuzibainisha kwa watu Kitabuni -- hao anawalaani
Mwenyezi Mungu, na wanawalaani kila wenye kulaani.
160. Ila
wale walio tubu na wakatengeneza na wakabainisha, basi hao nitapokea toba yao,
na Mimi ni Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu.
161.
Hakika walio kufuru na wakafa hali ni makafiri, hao iko juu yao laana ya
Mwenyezi Mungu na ya Malaika na ya watu wote.
162.
Watadumu humo. Hawata-punguziwa adhabu wala hawatapewa muda wa kupumzika.
163. Na
Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, hapana mungu ila Yeye. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
164. Hakika
katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku na mchana, na
marikebu ambazo hupita baharini kwa viwafaavyo watu, na maji anayo yateremsha
Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwa hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa
kwake, na akaeneza humo kila aina ya wanyama; na katika mabadiliko ya pepo, na
mawingu yanayo amrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka zimo Ishara
kwa watu wanao zingatia.
165. Na katika
watu wapo wanao chukua waungu wasio kuwa Mwenyezi Mungu. Wanawapenda kama
kumpenda Mwenyezi Mungu. Lakini walio amini wanampenda Mwenyezi Mungu
zaidi sana. Na laiti walio dhulumu wakajua watakapo iona adhabu kuwa nguvu zote
ni za Mwenyezi Mungu na kuwa Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu!
166. Walio fuatwa watakapo wakataa wale walio wafuata, na
hali ya kuwa wamekwisha iona adhabu; na yatakatika mafungamano yao.
167. Na watasema wale walio fuata: Laiti tungeweza kurudi
tukawakataa wao kama wanavyo tukataa sisi! Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu atakavyo
waonyesha vitendo vyao kuwa majuto yao; wala hawatakuwa wenye kutoka Motoni.
168. Enyi
watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi, halali na vizuri, wala msifuate nyayo za
Shet'ani. Hakika yeye ni adui
yenu aliye dhaahiri.
169. Yeye
anakuamrisheni maovu na machafu, na mumsingizie Mwenyezi Mungu mambo msiyo
yajua.
170. Na wanapo
ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu; wao husema: Bali tutafuata
tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je, hata ikiwa baba zao walikuwa hawaelewi kitu,
wala hawakuongoka?
171. Na mfano wa
walio kufuru ni kama mfano wa anaye mpigia kelele asiye sikia ila wito na sauti
tu -- ni viziwi, mabubu, vipofu, kwa hivyo hawaelewi.
172. Enyi mlio amini! Kuleni vizuri tulivyo kuruzukuni, na
mumshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli mnamuabudu Yeye tu.
173.Yeye amekuharimishieni mzoga tu na damu na nyama ya
nguruwe na kilicho tajiwa, katika kuchinjwa kwake, jina la asiye kuwa Mwenyezi
Mungu. Lakini aliye fikiwa na dharura bila ya kutamani wala kupita kiasi, yeye
hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
174. Hakika wale wafichao aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu
katika Kitabu, wakanunua kwacho thamani ndogo, hao hawali matumboni mwao isipo
kuwa moto, wala Mwenyezi Mungu hatawasemeza Siku ya Kiyama, wala hatawatakasa.
Nao watapata adhabu chungu.
175. Hao ndio walio nunua upotofu badala ya uwongofu, na
adhabu badala ya maghfira. Ama
wavumilivu wa Moto watu hawa!
176. Hayo
ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameteremsha Kitabu kwa haki. Na wale walio khitilafiana
katika Kitabu wamo katika upinzani ulio mbali na haki.
177. Sio
wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni
wa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na
Manabii, na anawapa mali, kwa kupenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na
wasafiri, na waombao, na katika ugombozi, na akawa anashika Sala, na akatoa
Zaka, na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi, na wanao vumilia katika shida na
dhara na wakati wa vita; hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wajilindao.
178.Enyi mlio amini! Mmepewa ruhusa kulipa kisasi katika
walio uwawa - muungwana kwa muungwana, na mtumwa kwa mtumwa, na mwanamke kwa
mwanamke. Na anaye samehewa na ndugu yake chochote basi ashikwe kulipa kwa
wema, na yeye alipe kwa ihsani. Huko ni kupunguziwa kuliko tokana na Mola wenu Mlezi,
na ni rehema. Na atakaye vuka mipaka baada ya haya, basi yeye atapata adhabu
chungu.
179. Mtakuwa nao uhai mzuri katika kulipiza kisasi enyi
wenye akili, ili msalimike.
180. Mmeandikiwa -- mmoja wenu anapo fikwa na mauti, kama
akiacha mali -- afanye wasia kwa wazazi wake na jamaa zake kwa namna nzuri
inayo pendeza. Ni waajibu haya kwa wachamngu.
181. Na atakaye ubadilisha wasia baada ya kuusikia, basi
dhambi yake ni juu ya wale watakao ubadilisha; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusikia Mwenye kujua.
182. Na mwenye kumkhofia muusiaji kwenda kombo au kupata
dhambi akasuluhisha baina yao, basi hatakuwa na dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu
ni Msamehevu na Mwenye kurehemu.
183, Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo
andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu.
184. (Mfunge) siku maalumu za kuhisabika. Na atakaye kuwa
miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine.
Na wale wasio weza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini. Na atakaye fanya wema
kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na mkifunga ni bora kwenu, kama mnajua.
185. Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani
kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi
ataye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini,
basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo
mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze
Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.
186. Na waja wangu watakapo kuuliza khabari zangu, waambie
kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anapo niomba. Basi na
waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka.
187. Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana na wake
zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu anajua kwamba
mlikuwa mkizikhini nafsi zenu. Kwa hivyo amekukubalieni toba yenu na amekusameheni.
Basi sasa changanyikeni nao na takeni aliyo kuandikieni Mwenyezi Mungu. Na
kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa
usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku. Wala msichanganyike nao, na hali
mnakaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi msiikaribie.
Namna hivi Mwenyezi Mungu anabainisha Ishara zake kwa watu ili wapate kumcha.
188. Wala msiliane mali zenu kwa baat'ili na kuzipeleka kwa
mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi, na hali mnajua.
189. Wanakuuliza khabarai ya miezi. Sema: Hiyo ni vipimo
vya nyakati kwa ajili ya watu na Hija. Wala sio wema kuziingia nyumba kwa
nyuma. Bali mwema ni mwenye kuchamngu. Na ingieni majumbani kupitia milangoni.
Na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa.
190. Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu na wale
wanao kupigeni, wala msianze uadui. Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi waanzao
uadui.
191. Na wauweni popote mwakutapo, na muwatoe popote walipo
kutoeni; kwani fitina ni mbaya zaidi kuliko kuuwa. Wala msipigane nao kwenye
Msikiti Mtakatifu mpaka wakupigeni huko. Wakikupigeni huko basi nanyi pia
wapigeni. Na hivi ndivyo yalivyo malipo ya makafiri.
192. Lakini wakiacha basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe
Mwenye kurehemu.
193. Na piganeni nao mpaka pasiwepo fitina, na Dini iwe ya
Mwenyezi Mungu tu. Na kama wakiacha basi usiweko uadui ila kwa wenye kudhulumu.
194. Mwezi mtakatifu kwa mwezi mtakatifu. Na vitu
vitakatifu vimeekewa kisasi. Anaye kushambulieni nanyi mshambulieni, kwa kadiri
alivyo kushambulieni. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu
yu pamoja na wachamngu.
195. Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala msijitie
kwa mikono yenu katika maangamizo. Na fanyeni wema. Hakika Mwenyezi Mungu
huwapenda wafanyao wema.
196. Na timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Na ikiwa mkizuiwa,basi (chinjeni) wanyama walio wepesi kupatikana. Wala msinyoe
vichwa vyenu mpaka wanyama hao wafike machinjoni mwao. Na atakaye kuwa mgonjwa
au ana vya kumuudhi kichwani mwake basi atoe fidiya kwa kufunga au kwa kutoa
sadaka au kuchinja wanyama. Na mtakapo kuwa salama, basi mwenye kujistarehesha
kwa kufanya Umra kisha ndio akahiji, basi achinje mnyama aliye mwepesi kumpata.
Na asiye pata, afunge siku tatu katika Hija na siku saba mtakapo rudi; hizi ni
kumi kaamili. Hayo ni kwa ajili ya yule ambaye watu wake hawako karibu na
Msikiti Mtakatifu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni Mwenyezi Mungu ni Mkali
wa kuadhibu.
197. Hija ni miezi maalumu. Na anaye kusudia kufanya Hija
katika miezi hiyo, basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu
wala asibishane katika Hija. Na kheri yoyote mnayo ifanya Mwenyezi Mungu
anaijua. Na jitengezeeni zawadi. Na hakika bora ya zawadi ni uchamngu. Na
nicheni Mimi, enyi wenye akili!
198. Si vibaya kwenu kuitafuta fadhila ya Mola wenu Mlezi.
Na mtakapo miminika kutoka A'rafat mtajeni Mwenyezi Mungu penye Masha'ril
Haram. Na mkumbukeni kama alivyo kuongoeni, ijapo kuwa zamani mlikuwa miongoni
mwa walio potea.
199. Kisha miminikeni kutoka pale wanapo miminika watu, na
muombeni Mwenyezi Mungu msamaha: hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe
Mwenye kurehemu.
200. Na mkisha timiza ibada zenu basi mtajeni Mwenyezi
Mungu kama mlivyo kuwa mkiwataja baba zenu au mtajeni zaidi. Na wapo baadhi ya
watu wanao sema: Mola wetu Mlezi, tupe duniani! Naye katika Akhera hana sehemu yoyote.
|