1 - 50
1. Alif
Laam Miim.
2.
Mwenyezi Mungu, hakuna mungu ila Yeye Aliye Hai, Msimamizi wa yote milele.
3. Amekuteremshia
Kitabu kwa haki, kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake. Na
aliteremsha Taurati na Injili
4. Kabla yake, ziwe uwongofu kwa watu. Na akateremsha
Furqani (Upambanuo). Hakika walio zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu watakuwa
na adhabu kali. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye kulipa.
5. Hakika Mwenyezi Mungu hakifichiki chochote kwake,
duniani wala mbinguni.
6. Yeye ndiye anaye kuundeni ndani ya matumbo ya wazazi kwa
namna apendayo. Hapana mungu ila Yeye, Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
7.Yeye ndiye aliye kuteremshia Kitabu hichi. Ndani yake
zimo Aya muhkam, zenye maana wazi. Hizo ndizo msingi wa Kitabu hichi. Na ziko
nyengine za mifano. Ama wale ambao nyoyoni mwao umo upotovu wanafuata zile za
mifano kwa kutafuta fitna, na kutafuta maana yake; na wala hapana ajuaye maana
yake ila Mwenyezi Mungu. Na wale wenye msingi madhubuti katika ilimu husema:
Sisi tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki hayo
isipo kuwa wenye akili.
8. (Na hao husema): Mola wetu Mlezi! Usizipotoe nyoyo zetu
baada ya kwisha tuongoa, na utupe rehema itokayo kwako. Hakika Wewe ndiye Mpaji.
9. Mola wetu Mlezi! Wewe ndiye Mkusanyaji wa watu kwa Siku
isiyo na shaka ndani yake. Hakika Mwenyezi Mungu havunji miadi yake.
10. Kwa hakika wale walio kufuru hazitowafaa kitu kwa
Mwenyezi Mungu mali zao, wala watoto wao; nao hao ndio kuni za Motoni-
11. - Kama yaliyo wapata watu wa Firauni na wale walio kuwa
kabla yao. Walikanusha Ishara zetu, basi Mwenyezi Mungu aliwashika kwa madhambi
yao; na Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
12. Waambie walio kufuru: Karibuni mtashindwa na
mtakusanywa, mtiwe kwenye Jahannam; nako huko ni makao mabaya kabisa.
13. Hakika ilikuwa ni Ishara kwenu katika yale majeshi
mawili yalipo pambana. Jeshi moja likipigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na
jingine kafiri likiwaona zaidi kuliko wao mara mbili, kwa kuona kwa macho. Na
Mwenyezi Mungu humuunga mkono amtakaye kwa nusura yake. Hakika katika hayo yapo
mazingatio kwa wenye macho.
14. Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na
wana, na mirundi ya dhahabu na fedha, na farasi asili, na mifugo, na mashamba.
Hayo ni starehe ya maisha ya duniani; na kwa Mwenyezi Mungu ndio kwenye marejeo
mema.
15. Sema: Nikwambieni yaliyo bora kuliko hayo? Kwa
wachamngu ziko Bustani kwa Mola wao zipitazo mito kati yake. Watadumu humo, na
wake walio takaswa, na wanazo radhi za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kuwaona waja wake,
16. Ambao husema: Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tumeamini,
basi tufutie madhambi yetu, na tuepushe na adhabu ya Moto,
17. Wanao subiri, wanao sema kweli, na wat'iifu, na wanao
toa sadaka, na wanao omba maghafira kabla ya alfajiri.
18. Mwenyezi Mungu, na Malaika, na wenye ilimu,
wameshuhudia kuwa hakika hapana mungu ila Yeye, ndiye Mwenye kusimamisha
uadilifu; hapana mungu ila Yeye Mwenye nguvu na Mwenye hikima.17
19. Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu.
Na walio pewa Kitabu hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa sababu
ya uhasidi ulio kuwa baina yao. Na anaye zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu basi
hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
20. Na pindi wakikuhoji, basi sema: Mimi nimeusalimisha uso
wangu kumwelekea Mwenyezi Mungu, na kadhaalika walio nifuata. Na waambie walio
pewa Kitabu na wasio na kisomo: Je! Mmesilimu? Wakisilimu basi wameongoka. Na
wakikengeuka basi juu yako ni kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kuwaona waja wake.
21. Hakika wanao zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, na
wakawauwa Manabii pasipo haki, na wakawauwa watu waamrishao Haki wabashirie
adhabu kali.
22. Hao ndio ambao vitendo vyao vimeharibika duniani na
Akhera. Nao hawatapata wa kuwanusuru.
23. Huwaoni wale walio pewa sehemu ya Kitabu? Wanaitwa
kukiendea Kitabu cha Mwenyezi Mungu ili kiwahukumu baina yao; kisha baadhi yao
wanageuka wanakikataa.
24. Hayo ni kwa sababu walisema: Hautatugusa Moto isipo
kuwa kwa siku chache tu. Na yakawadanganya katika dini yao yale ambayo wenyewe
waliyo kuwa wakiyazua.
25. Basi itakuwaje tutakapo wakusanya Siku ambayo haina
shaka kuja kwake? Na kila nafsi italipwa kama ilivyo chuma, bila ya
kudhulumiwa.
26. Sema: Ewe Mwenyezi Mungu uliye miliki ufalme wote! Wewe
humpa ufalme umtakaye, na humwondolea ufalme umtakaye, na humtukuza umtakaye,
na humuangusha umtakaye. Kheri yote iko mikononi mwako. Hakika Wewe ni Muweza
wa kila kitu.
27. Wewe huingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana
katika usiku. Na humtoa hai kutokana na maiti, na humtoa maiti kutokana na
aliye hai. Na unamruzuku umtakaye bila ya hisabu.
28. Waumini wasiwafanye makafiri kuwa wapenzi wao badala ya
Waumini. Na anaye fanya hivyo, basi hatakuwa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu.
Ila ikiwa kwa ajili ya kujilinda na shari zao. Na Mwenyezi Mungu
anakuhadharisheni naye. Na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu.
29. Sema: Mkificha yaliyomo vifuani mwenu au mkiyafichua
Mwenyezi Mungu anayajua; na anayajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo duniani. Na
Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
30. Siku ambayo kila nafsi itakuta mema iliyo yafanya
yamehudhurishwa, na pia ubaya ilio ufanya. Itapenda nafsi lau kungekuwako
masafa marefu baina ya ubaya huo na yeye. Na Mwenyezi Mungu anakuhadharisheni
naye. Na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.
31. Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi
nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu.
32. Sema: Mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume. Na wakigeuka
basi Mwenyezi Mungu hawapendi makafiri.
33. Hakika Mwenyezi Mungu alimteuwa Adam na Nuhu na ukoo wa
Ibrahim na ukoo wa Imran juu ya walimwengu wote.
34. Ni wazao wao kwa wao; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusikia na Mwenye kujua.
35. Alipo sema mke wa Imran: Mola wangu Mlezi! Nimekuwekea
nadhiri kilichomo tumboni mwangu kuwa wakfu; basi nikubalie. Hakika Wewe ndiye
Mwenye kusikia na Mwenye kujua.
36. Basi alipo mzaa alisema: Mola wangu Mlezi! Nimemzaa
mwanamke - na Mwenyezi Mungu anajua sana aliye mzaa - Na mwanamume si sawa na
mwanamke. Na mimi nimemwita Maryamu. Nami namkinga kwako, yeye na uzao wake,
uwalinde na Shet'ani aliye laaniwa.
37. Tena Mola wake Mlezi akampokea kwa mapokeo mema na
akamkuza makuzo mema, na akamfanya Zakariya awe mlezi wake. Kila mara Zakariya
alipo ingia chumbani kwake alimkuta na vyakula. Basi alimwambia: Ewe Maryamu!
Unavipata wapi hivi? Naye akasema: Hivi vinatoka kwa Mwenyezi Mungu; na
Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.
38. Pale pale Zakariya akamwomba Mola wake Mlezi, akasema:
Mola wangu Mlezi! Nipe kutoka kwako uzao mwema. Wewe ndiye unaye sikia maombi.
39. Alipo kuwa kasimama chumbani akisali, Malaika kamnadia:
Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria Yahya, ataye kuwa mwenye kusadikisha neno
litokalo kwa Mwenyezi Mungu, na ni bwana na mt'awa na Nabii kwa watu wema.
40. Akasema Zakariya: Mola wangu Mlezi! Vipi nitapata mwana
na hali ukongwe umenifikia, na mke wangu ni tasa? Akasema: Ndivyo vivyo hivyo,
Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo.
41. Akasema: Mola wangu Mlezi! Niwekee alama. Akasema:
Alama yako ni kuwa hutasema na watu kwa siku tatu, isipo kuwa kwa kuashiria tu.
Na mdhukuru Mola Mlezi wako kwa wingi na mtakase jioni na asubuhi.
42. Na angalia pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Kwa
hakika Mwenyezi Mungu amekuteuwa, na akakutakasa, na akakutukuza kuliko
wanawake wote.
43. Ewe
Maryamu! Mnyenyekee Mola Mlezi wako na usujudu na uiname pamoja na wainamao.
44. Hizi
ni khabari za ghaibu tunazo kufunulia; nawe hukuwa nao walipo kuwa wakitupa
kalamu zao nani wao atamlea Maryamu, na hukuwa nao walipo kuwa wakishindana.
45. Na pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Hakika
Mwenyezi Mungu anakubashiria (mwana) kwa neno litokalo kwake. Jina lake ni
Masihi Isa mwana wa Maryamu, mwenye hishima katika dunia na Akhera, na miongoni
mwa walio karibishwa (kwa Mwenyezi Mungu).
46. Naye atazungumza na watu katika utoto wake na katika
utuuzima wake, na atakuwa katika watu wema.
47. Maryamu akasema: Mola wangu Mlezi! Vipi nitampata mwana
na hali hajanigusa mwanaadamu? Mwenyezi Mungu akasema: Ndivyo vivyo hivyo,
Mwenyezi Mungu huumba apendacho. Anapo hukumu jambo, huliambia: Kuwa! Likawa.
48. Na
atamfunza kuandika na Hikima na Taurati na Injili.
49. Na ni Mtume kwa Wana wa Israili kuwaambia: Mimi
nimekujieni na Ishara kutoka kwa Mola Mlezi wenu, ya kwamba nakuundieni kwa
udongo kama sura ya ndege. Kisha nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi
Mungu. Na ninawaponesha vipofu wa tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua
maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ninakwambieni mnacho kila na mnacho weka
akiba katika nyumba zenu. Hakika katika haya ipo Ishara kwenu ikiwi nyinyi ni
wenye kuamini.
50. Na ninasadikisha yaliyo kuwa kabla yangu katika
Taurati, na ili nikuhalalishieni baadhi ya yale mlio harimishiwa, na
nimekujieni na Ishara kutokana na Mola Mlezi wenu. Kwa hivyo mcheni Mwenyezi
Mungu na nit'iini mimi.
|