151 - 200
151. Tutazitia khofu nyoyo za walio kufuru kwa vile walivyo
mshirikisha Mwenyezi Mungu na washirika ambao hakuwateremshia hoja yoyote. Na
makaazi yao ni Motoni; na maovu yaliyoje maskani ya wenye kudhulumu!
152. Na Mwenyezi Mungu alikutimilizieni miadi yake, vile
mlivyo kuwa mnawauwa kwa idhini yake, mpaka mlipo legea na mkazozana juu ya
amri, na mkaasi baada ya Yeye kukuonyesheni mliyo yapenda. Wapo miongoni mwenu wanao
taka dunia, na wapo miongoni mwenu wanao taka Akhera. Kisha akakutengeni nao
(maadui) ili akujaribuni. Naye sasa amekwisha kusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye fadhila juu ya Waumini.
153. Pale mlipo kuwa mkikimbia mbio wala hamumsikilizi
yeyote, na Mtume anakuiteni, yuko nyuma yenu. Mwenyezi Mungu akakupeni dhiki
juu ya dhiki, ili msisikitike kwa yaliyo kukoseeni wala kwa yaliyo kusibuni. Na
Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda.
154. Kisha baada ya dhiki alikuteremshieni utulivu -
usingizi ambao ulifunika kundi moja kati yenu. Na kundi jengine nafsi zao
ziliwashughulisha hata wakamdhania Mwenyezi Mungu dhana isiyo kuwa ya haki,
dhana ya kijinga. Wakisema: Hivyo tuna lolote sisi katika jambo hili? Sema:
Mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Wanaficha katika nafsi zao wasiyo kubainishia.
Wanasema: Lau ingelikuwa tuna lolote katika jambo hili tusinge uliwa hapa.
Sema: Hata mngeli kuwa majumbani mwenu, basi wangeli toka walio andikiwa kufa,
wakenda mahali pao pa kuangukia wafe.(Haya ni hivyo) ili Mwenyezi Mungu
ayajaribu yaliyomo vifuani mwenu, na asafishe yaliyomo nyoyoni mwenu. Na
Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo vifuani.
155. Hakika wale walio rudi nyuma miongoni mwenu siku
yalipo pambana majeshi mawili, Shet'ani ndiye aliye watelezesha kwa sababu ya
baadhi ya makosa waliyo yafanya; na Mwenyezi Mungu amekwisha wasamehe. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mpole.
156. Enyi mlio amini! Msiwe kama wale walio kufuru na
wakawasema ndugu zao walipo safiri katika nchi au walipo kuwa vitani: Wangeli
kuwa kwetu wasingeli kufa na wasingeli uwawa. Ili Mwenyezi Mungu afanye hayo
kuwa ni majuto katika nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu huhuisha na hufisha. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona myatendayo.
157. Na pindi mkiuliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu, au
mkifa, hakika maghfira na rehema zitokazo kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko
yote wanayo yakusanya.
158. Na mkifa au mkiuliwa ni kwa Mwenyezi Mungu ndio
mtakusanywa.
159. Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi
Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu,
bila ya shaka wangeli kukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na
shauriana nao katika mambo. Na ukisha kata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu.
Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao mtegemea.
160. Akikunusuruni Mwenyezi Mungu hapana wa kukushindeni,
na akikutupeni ni nani, basi, baada yake Yeye ataye kunusuruni? Na Waumini
wamtegemee Mwenyezi Mungu tu.
161. Na haiwezekani kwa Nabii yeyote kufanya khiyana. Na
atakaye fanya khiyana, atayaleta Siku ya Kiyama aliyo yafanyia khiyana, kisha
kila mtu atalipwa kwa aliyo yachuma, kwa ukamilifu; wala hawatadhulumiwa.
162. Je! Aliye yafuata ya kumridhisha Mwenyezi Mungi ni
kama yule aliye stahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na makaazi yake yakawa
Jahannamu? Napo ni mahala pabaya pa kurejea.
163. Hao wana vyeo mbali mbali kwa Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona yote wayatendayo.
164. Hakika Mwenyezi Mungu amewafanyia wema mkubwa Waumini
vile alivyo waletea Mtume aliye miongoni mwao wenyewe, anaye wasomea Aya zake,
na anawatakasa, na anawafunza Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya hapo
walikuwa katika upotovu ulio wazi.
165. Nyinyi - ulipo kusibuni msiba ambao nyinyi mmekwisha
watia mara mbili mfano wa huo - mnasema: Umetoka wapi huu? Sema: Huo umetoka
kwenu wenyewe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
166. Na yaliyo kusibuni siku yalipo pambana majeshi mawili
yalikuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ili awajue Waumini.
167. Na ili awapambanue walio kuwa wanaafiki, wakaambiwa:
Njooni mpigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu au lindeni. Wakasema: Tungeli jua
kuna kupigana bila ya shaka tungeli kufuateni. Wao siku ile walikuwa karibu na
ukafiri kuliko Imani. Wanasema kwa midomo yao yasiyo kuwamo nyoyoni mwao. Na
Mwenyezi Mungu anajua kabisa wanayo yaficha.
168. Hao ndio walio waambia ndugu zao na wao wenyewe
wakakaa kitako: Lau wengeli tut'ii wasingeli uliwa. Sema: Ziondoleeni nafsi
zenu mauti kama mnasema kweli.
169. Wala kabisa usiwadhanie walio uliwa katika Njia ya
Mwenyezi Mungu kuwa ni maiti. Bali hao ni wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao
Mlezi.
170. Wanafurahia aliyo wapa Mwenyezi Mungu kwa fadhila
yake, na wanawashangilia wale ambao bado hawajajiunga nao, walio nyuma yao, ya
kwamba haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.
171. Wanashangilia neema na fadhila za Mwenyezi Mungu, na
ya kwamba Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa Waumini,
172. Walio mwitikia Mwenyezi Mungu na Mtume baada ya kwisha
patwa na majaraha - kwa walio fanya wema miongoni mwao na wakamchamngu utakuwa
ujira mkubwa -
173. Walio ambiwa na watu: Kuna watu wamekukusanyikieni,
waogopeni! Hayo yakawazidishia Imani, wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosha, naye
ni mbora wa kutegemewa.
174. Basi wakarudi na neema na fadhila za Mwenyezi Mungu.
Hapana baya lilio wagusa, na wakafuata yanayo mridhi Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu.
175. Hakika huyo ni Shet'ani anawatia khofu marafiki zake,
basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi mkiwa nyinyi ni Waumini.
176. Wala wasikuhuzunishe
wale wanao kimbilia ukafirini. Hakika hao hawamdhuru kitu Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu anataka asiwawekee sehemu yoyote katika Akhera, na yao wao
adhabu kubwa.
177.
Hakika wale walio nunua ukafiri kwa Imani hawatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu, na
yao wao ni adhabu chungu.
178. Wala
wasidhani wale wanao kufuru kwamba huu muhula tunao wapa ni kheri yao. Hakika
tunawapa muhula wazidi madhambi. Na yao wao ni adhabu ya kuwadhalilisha.
179. Haiwi
kwa Mwenyezi Mungu kuwaacha Waumini katika hali mliyo nayo mpaka apambanue
wabaya na wema. Wala haiwi kwa Mwenyezi Mungu kukujuulisheni mambo ya ghaibu.
Lakini Mwenyezi Mungu humteua katika Mitume wake amtakaye. Basi
muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume yake. Na mkiamini na mkamchamngu mtakuwa na
ujira mkubwa.
180. Wala wasidhani wale ambao wanafanya ubakhili katika
aliyo wapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake kuwa ni kheri yao. Bali hiyo ni
shari kwao. Watafungwa kongwa za yale waliyo yafanyia ubakhili Siku ya Kiyama.
Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anazo
khabari za yote myatendayo.
181. Mwenyezi Mungu amekwisha sikia kauli ya walio sema:
Mwenyezi Mungu ni masikini, na sisi ni matajiri. Tumeyaandika waliyo yasema, na
pia kuwauwa kwao Manabii bila ya haki, na tutawaambia Siku ya Kiyama: Onjeni adhabu
ya kuungua.
182. Haya ni kwa sababu ya iliyo tanguliza mikono yenu, na
kwamba Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja,
183. Walio sema: Mwenyezi Mungu ametuahidi tusimuamini
Mtume yeyote mpaka atuletee kafara inayo teketezwa na moto. Waambie:
Walikujieni Mitume kabla yangu kwa hoja zilizo wazi na kwa hayo mnayo sema,
basi kwa nini mkawauwa ikiwa mlikuwa wakweli?
184. Na wakikukanusha basi walikanushwa Mitume wengine
kabla yako walio kuja na hoja waziwazi na Vitabu vyenye hikima, na Kitabu
chenye nuru.
185. Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa
ujira wenu kaamili Siku ya Kiyama. Na atakaye epushwa na Moto na akatiwa Peponi
basi huyo amefuzu. Na maisha ya dunia si kitu ila ni starehe ya udanganyifu.
186. Hapana shaka yoyote mtapata misukosuko katika mali
zenu na nafsi zenu, na bila ya shaka yoyote mtasikia udhia mwingi kutokana na
walio pewa Kitabu kabla yenu na wale walio shiriki. Na ikiwa mtasubiri na
mkamchamngu basi hakika hayo ni katika mambo ya kuazimia.
187. Na pale Mwenyezi Mungu alipo fungamana na walio pewa
Kitabu kuwa: Lazima mtawabainishia watu, wala hamtokificha, walikitupa nyuma ya
migongo yao, na wakanunua kwacho thamani duni. Basi ni kiovu hicho walicho
nunua.
188. Usiwadhanie kabisa wale wanao furahia waliyo yafanya,
na wakapenda kusifiwa kwa wasiyo yatenda, usiwadhanie kuwa watasalimika na
adhabu. Yao wao ni adhabu chungu.
189. Na Ufalme
wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu
ya kila kitu.
190. Hakika
katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara
kwa wenye akili,
191. Ambao
humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala, na
hufikiri kuumbwa mbingu na ardhi, wakisema: Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi
bure. Subhanaka, Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto.
192. Mola wetu Mlezi! Hakika unaye mtia Motoni umemhizi; na
walio dhulumu hawana wasaidizi.
193. Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tumemsikia mwenye kuita
akiitia Imani kwamba: Muaminini Mola wenu Mlezi; nasi tukaamini. Basi tusamehe
madhambi yetu, na utufutie makosa yetu, na utufishe pamoja na watu wema.
194. Mola wetu Mlezi! Na utupe uliyo tuahidi kwa Mitume
wako, wala usituhizi Siku ya Kiyama. Hakika Wewe huvunji miadi.
195. Mola Mlezi wao, akayakubali maombi yao akajibu: Hakika
sipotezi kazi ya mfanya kazi miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, kwani
ni nyinyi kwa nyinyi. Basi walio hama, na walio tolewa makwao, na wakateswa
katika Njia yangu, na wakapigana, na wakauliwa, kwa yakini Mimi nitawafutia
makosa yao, na kwa yakini nitawaingiza katika Mabustani yanayo pita mito kati
yake. Hayo ndiyo malipo yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu kwake
yapo malipo mema kabisa.
196. Kabisa kusikudanganye kubakia kutangatanga kwa walio
kufuru katika nchi.
197. Hiyo ni starehe ndogo. Kisha makaazi yao yatakuwa
Jahannamu. Na ni mahali pabaya mno pa kupumzikia.
198. Lakini walio mcha Mola wao Mlezi watapata Mabustani
yanayo pita mito kati yake. Watadumu humo. Hayo ni makaribisho yao yatokayo kwa
Mwenyezi Mungu. Na vilioko kwa Mwenyezi Mungu ni bora kwa watu wema.
199. Hakika miongoni mwa Watu wa Kitabu wapo wanao muamini
Mwenyezi Mungu na yaliyo teremshwa kwenu na yaliyo teremshwa kwao,
wakimnyenyekea Mwenyezi Mungu. Hawabadili Aya za Mwenyezi Mungu kwa thamani
duni. Hao wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi
wa kuhisabu.
200. Enyi mlio amini! Subirini, na shindaneni kusubiri, na kuweni
macho, na mcheni Mwenyezi Mungu, ili mpate kufanikiwa.
|