51 - 100
51. Enyi mlio amini! Msiwafanye Mayahudi na Wakristo kuwa
ni marafiki. Wao ni marafiki wao kwa
wao. Na miongoni mwenu mwenye kufanya urafiki nao, basi huyo ni katika wao.
Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wenye kudhulumu.
52. Utawaona
wale wenye maradhi nyoyoni mwao wanakimbilia kwao wakisema: Tunakhofu
yasitusibu mabadiliko. Huenda Mwenyezi Mungu akaleta ushindi au jambo jingine
litokalo kwake wakawa wenye kujuta kwa waliyo yaficha katika nafsi zao.
53. Na walio
amini watasema: Hivyo hawa ndio wale walio apa ukomo wa viapo vyao kuwa wao wa
pamoja nanyi? Vitendo vyao vitapotea bure, na wataamkia kuwa wenye kukhasirika.
54. Enyi mlio amini! Atakaye iacha miongoni mwenu Dini
yake, basi Mwenyezi Mungu atakuja leta watu anao wapenda nao wanampenda,
wanyenyekevu kwa Waumini na wenye nguvu juu ya makafiri, wanapigania Jihadi
katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawaogopi lawama ya anaye laumu. Hiyo ndiyo
fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu na
Mwenye kujua.
55. Hakika rafiki yenu mlinzi ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake
na walio amini, ambao hushika Sala na hutoa Zaka nao wananyenyekea.
56. Na atakaye fanya urafiki na Mwenyezi Mungu na Mtume
wake na walio amini, basi hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kushinda.
57. Enyi mlio amini! Msiwafanye marafiki wale walio ifanyia
kejeli na mchezo Dini yenu miongoni mwa walio pewa Kitabu kabla yenu, na
makafiri wengine. Na mcheni Mwenyezi Mungu kama nyinyi ni wenye kuamini.
58. Na mnapo adhinia Sala wao wanaichukulia maskhara na
mchezo. Hayo ni kwa sababu wao ni watu wasio na akili.
59. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Hivyo mnatuchukia kwa kuwa
tumemuamini Mwenyezi Mungu na tuliyo teremshiwa na yaliyo teremshwa kabla, na
kwa kuwa wengi katika nyinyi ni wapotofu?
60. Sema: Je! Nikwambieni yule ambaye ni mwenye malipo
mabaya zaidi kuliko hayo mbele ya Mwenyezi Mungu? Ni yule ambaye Mwenyezi Mungu
amemlaani na amemkasirikia, na amewafanya miongoni mwao manyani na nguruwe, na
wakamuabudu Shet'ani. Hao ndio wenye mahali pabaya na wamepotea zaidi njia
iliyo sawa.
61. Na wanapo kujieni husema: Tumeamini. Lakini hakika wao
wameingia na ukafiri wao, na wametoka nao pia. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi
kabisa wa yote wanayo yaficha.
62. Na utawaona wengi katika wao wanakimbilia kwenye
dhambi, na uadui, na ulaji wao vya haramu. Ni maovu mno hayo wayatendayo!
63. Mbona hao wanazuoni na makohani wao hawawakatazi maneno
yao ya dhambi, na ulaji wao vya haramu? Ni maovu mno hayo wayafanyayo!
64. Na Mayahudi walisema: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba.
Mikono yao ndiyo iliyo fumba, na wamelaaniwa kwa sababu ya waliyo yasema. Bali
mikono yake iwazi. Hutoa apendavyo. Kwa yakini yaliyo teremshwa kwako kutoka
kwa Mola wako Mlezi yatawazidisha wengi katika wao uasi na kufuru. Na Sisi
tumewatilia uadui na chuki baina yao mpaka Siku ya Kiyama. Kila mara wanapo
washa moto wa vita, Mwenyezi Mungu anauzima. Na wanajitahidi kuleta uharibifu
katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi waharibifu.
65. Na lau kuwa Watu wa Kitabu wangeli amini na wakachamngu
hapana shaka tungeli wafutia makosa yao, na tungeli waingiza katika Bustani
zenye neema.
66. Na lau kuwa wangeli ishika Taurati na Injili na yote
waliyo teremshiwa kutokana na Mola wao Mlezi, basi hapana shaka wangeli kula
vya juu yao na vya chini ya miguu yao. Wapo watu miongoni mwao walio sawa,
lakini wengi wao wanayo yafanya ni mabaya mno.
67. Ewe
Mtume! Fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hukufanya
hayo basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika
Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
68. Sema:
Enyi Watu wa Kitabu! Hamna lenu jambo mpaka muishike Taurati na Injili na yote
mlio teremshiwa kutokana na Mola wenu Mlezi. Na hakika ulio teremshiwa wewe
kutokana na Mola wako Mlezi yatawazidishia wengi katika wao uasi na ukafiri.
Basi usiwasikitikie watu makafiri.
69. Hakika
walio amini, na Mayahudi na Masabii na Wakristo, walio muamini Mwenyezi Mungu,
na Siku ya mwisho, na wakatenda mema, basi hawatakuwa na khofu wala
hawatahuzunika.
70. Tulifanya agano na Wana wa Israili, na tukawatumia
Mitume. Kila alipo wajia Mtume kwa wasio yapenda nafsi zao wengine waliwakanusha
na wengine wakawauwa.
71. Na wakadhani kuwa hapatakuwa majaribio; basi wakawa
vipofu na viziwi. Kisha Mwenyezi Mungu akawapokelea toba zao. Kisha tena wengi
katika wao wakawa vipofu na viziwi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona hayo
wayatendayo.
72. Hakika wamekufuru walio sema: Mwenyezi Mungu ni Masihi
mwana wa Maryamu! Na hali Masihi mwenyewe alisema: Enyi Wana wa Israili!
Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Kwani anaye
mshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu atamharimishia Pepo, na
mahala pake ni Motoni. Na walio dhulumu hawatakuwa na wa kuwanusuru.
73. Kwa hakika wamekufuru walio sema: Mwenyezi Mungu ni wa
tatu wa Utatu. Hali hakuna mungu ila Mungu Mmoja. Na ikiwa hawaachi hayo wanayo
yasema, kwa yakini itawakamata adhabu chungu wale wanao kufuru.
74. Je! Hawatubu kwa Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha?
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.
75. Masihi mwana wa Maryam si chochote ila ni Mtume.
Wamekwisha pita Mitume kabla yake. Na mama yake ni mwanamke mkweli. Wote wawili
walikuwa wakila chakula. Angalia jinsi tunavyo wabainishia Aya, kisha angalia
vipi wanavyo geuzwa.
76. Sema: Je! Mnawaabudu, badala ya Mwenyezi Mungu, wale
ambao hawawezi kukudhuruni wala kukufaeni? Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye
kusikia, Mwenye kujua.
77. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini
yenu bila ya haki. Wala msifuate matamanio ya watu walio kwisha potea tangu
zamani, na wakawapoteza wengi, na wenyewe wakapotea njia iliyo sawa.
78. Walilaaniwa walio kufuru miongoni mwa Wana wa Israili
kwa ulimi wa Daud na wa Isa mwana wa Maryamu. Hayo ni kwa sababu waliasi na
wakawa wanapindukia mipaka.
79. Walikuwa hawakatazani maovu waliyo kuwa wakiyafanya.
Hakika ni maovu yalioje mambo waliyo kuwa wakiyafanya!
80. Utawaona wengi wao wanafanya urafiki na walio kufuru.
Hakika ni maovu yaliyo tangulizwa na nafsi zao hata Mwenyezi Mungu
amewakasirikia, nao watadumu katika adhabu.
81. Na lau wangeli kuwa wanamuamini Mwenyezi Mungu, na huyu
Nabii, na yaliyo teremshwa kwake, wasingeli wafanya hao marafiki. Lakini wengi
katika wao ni wapotofu.
82. Hakika utawakuta walio shadidi kuliko watu wote katika
uadui kwa walio amini ni Mayahudi na washirikina. Na utawakuta walio karibu mno
kwa mapenzi ni wale wanao sema: Sisi ni Manasara. Hayo ni kwa sababu wapo
miongoni mwao makasisi na wamonaki, na kwa sababu wao hawafanyi kiburi.
83. NA WANAPO SIKIA yaliyo teremshwa kwa Mtume utaona macho
yao yanachururika machozi kwa sababu ya Haki waliyo itambua. Wanasema: Mola
wetu Mlezi! Tumeamini. Basi tuandike pamoja na wanao shuhudia.
84. Na kwa nini tusimuamini Mwenyezi Mungu na Haki iliyo
tujia, na hali tunatumai Mola wetu Mlezi atuingize pamoja na watu wema?
85. Basi Mwenyezi Mungu atawalipa, kwa yale waliyo yasema,
Bustani zipitazo mito katika yake; humo watadumu. Na haya ndiyo malipo ya wafanyao
wema.
86. Na wale walio kufuru na wakazikanusha Ishara zetu, hao
ndio watu wa Motoni.
87. Enyi mlio amini! Msiharimishe vizuri alivyo
kuhalalishieni Mwenyezi Mungu, wala msikiuke mipaka. Hakika Mwenyezi Mungu
hawapendi wakiukao mipaka.
88. Na kuleni katika alivyo kuruzukuni Mwenyezi Mungu,
halali na vizuri. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mnamuamini.
89. Mwenyezi Mungu hatakushikeni kwa viapo vyenu vya
upuuzi, lakini atakushikeni kwa mnavyo apa kweli kweli kwa makusudio. Basi
kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnacho walisha
ahali zenu, au kuwavisha, au kumkomboa mtumwa. Asiye pata hayo, basi afunge
siku tatu. Hii ndiyo kafara ya viapo vyenu mnapo apa. Na hifadhini yamini zenu.
Namna hivyo Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake ili mpate kushukuru.
90. Enyi mlio amini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na
kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shet'ani. Basi
jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa.
91. Hakika Shet'ani anataka kutia kati yenu uadui na chuki
kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Basi je, mmeacha?
92. Na mt'iini
Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume, na tahadharini. Na ikiwa mtageuka basi jueni
ya kuwa juu ya Mtume wetu ni kufikisha ujumbe tu ulio wazi.
93. Si dhambi
juu ya walio amini na wakatenda mema kwa walivyo vila (zamani) maadamu
wakichamngu na wakiamini na wakitenda mema, kisha wakachamngu, na wakaamini,
kisha wakachamngu na wakafanya mazuri. Na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao mazuri.
94. Enyi mlio amini! Mwenyezi Mungu atakujaribuni kidogo
kwa wanyama wa kuwinda inayo wafikia mikono yenu na mikuki yenu, ili Mwenyezi
Mungu amjue nani anaye mkhofu kwa ghaibu. Basi atakaye ruka mipaka baada ya
hayo atapata adhabu kali.
95. Enyi mlio amini! Msiue wanyama wa kuwinda nanyi
mmeharimia katika Hija. Na miongoni mwenu atakaye muuwa makusudi, basi malipo
yake yatakuwa kwa kuchinja kilicho sawa na alicho kiuwa, katika mifugo, kama
wanavyo hukumu waadilifu wawili miongoni mwenu. Mnyama huyo apelekwe kwenye Al
Kaaba, au kutoa kafara kwa kuwalisha masikini; au badala ya hayo ni kufunga,
ili aonje ubaya wa jambo lake hili. Mwenyezi Mungu amekwisha yafuta yaliyo
pita; lakini atakaye fanya tena Mwenyezi Mungu atampa adhabu. Na Mwenyezi Mungu
ndiye Mwenye nguvu na Mwenye kuadhibu.
96. Nyinyi mmehalalishiwa kuvua vinyama vya baharini na
kuvila, kwa faida yenu na kwa wasafiri. Na mmeharimishiwa mawindo ya wanyama wa
bara maadamu mmeharimia Hija. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mtakusanywa
kwake.
97. Mwenyezi Mungu ameifanya Al Kaaba, hii Nyumba Tukufu,
ni simamio la watu, na kadhaalika Miezi Mitukufu, na wanyama wa dhabihu, na vigwe.
Hayo ili mjue ya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo
katika ardhi, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
98. Jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu, na ya
kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira, na Mwenye kurehemu.
99. Haimlazimu Mtume ila kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi
Mungu anajua mnacho kidhihirisha na mnacho kificha.
100. Sema: Haviwi sawa viovu na vyema ujapo kupendeza wingi
wa viovu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, enyi wenye akili, ili mpate kufanikiwa.
|