6. SURAT AL - AN-A'AM
(Imeteremka
Makka)
SURA hii ni ya Makka isipo
kuwa Aya hizi: 20, 23, 91, 93, 114, 141, 151, 152, na 153. Na Aya zake ni 165. Iliteremka
baada ya Sura Al-Hijr. Na Sura hii tukufu imekusanya maana zilizo wekwa mbali
mbali kama ifuatavyo:
Imewazindua watu wauzingatie ulimwengu na dalili ziliomo ndani yake zenye
kuonyesha Ubora wa aliye uumba, na Utukufu wake na Umoja wake wa pekee, na kuwa
Yeye hashirikiani na yeyote, la katika kuumba, wala katika kuabudiwa, wala
katika dhati yake.
Na imekusanya visa vya baadhi ya Manabii, na ikaanza kwa kisa cha Ibrahim
a.s. kwa kubainisha kuwa alichukua maana ya ibada na Tawhidi kwa kuuchungua
ulimwengu, na kufuata yaliyomo ndani yake. Naye alianza kwa kupeleleza nyota,
kisha mwezi, kisha jua, na akamalizia kwa kufuata ibada ya Mwenyezi Mungu peke
yake.
Na ikapelekea macho yaangalie ajabu za uumbaji na vipi mambo yanavyo kuwa.
Ikabainisha vipi kilicho hai kinyevu kinatokana na kisicho kuwa na uhai kikavu;
na vipi mbegu inavyo pasuka na ukachipua mmea.
Na Sura hii imezitaja sifa za wapinzani, na vipi wanavyo shikilia ndoto zao
zinazo watenga na Haki, na zinazo wapotosha.
Na ndani ya Sura hii umebainishwa uhalali wa vyakula alivyo halalisha
Mwenyezi Mungu Mtukufu, na upotovu wa Washirikina walivyo jiharimishia wenyewe
bila ya kutegemea dalili yoyote, na vipi wanavyo mnasibishia kuharimisha huko
Mwenyezi Mungu Aliye Takasika.
Na ndani yake yamebainishwa mambo haya, ambayo ndio mukhtasari wa Uislamu na
tabia njema za kusifika. Mambo yenyewe ni:- kuharimisha ushirikina, uzinzi,
kuuwa mtu, kula mali ya yatima, waajibu wa kutimiza vipimo na mizani, kutimiza
uadilifu, kutekeleza ahadi, kuwatendea wema wazazi, na kukataza kuwazika watoto
wa kike nao wahai.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
|