51 - 100
51. Na waonye kwayo wanao ogopa kuwa watakusanywa kwa Mola
wao Mlezi, hali kuwa hawana mlinzi wala mwombezi isipo kuwa Yeye, ili wapate
kuchamngu.
52. Wala usiwafukuze wanao mwomba Mola Mlezi wao asubuhi na
jioni kwa kutaka radhi yake. Si juu yako hisabu yao hata kidogo, wala hisabu
yako si juu yao hata kidogo, hata uwafukuze na uwe miongoni mwa wenye
kudhulumu.
53. Na hivi ndivyo tunavyo wajaribu wao kwa wao, ili
waseme: Ni hao ndio Mwenyezi Mungu amewafadhilisha miongoni mwetu? Kwani
Mwenyezi Mungu hawajui wanao shukuru?
54. Na wanapo kujia wanao ziamini Ishara zetu waambie:
Assalamu alaikum! Amani iwe juu yenu! Mola wenu Mlezi amejilazimisha rehema, ya
kwamba atakaye fanya uovu miongoni mwenu kwa ujinga, kisha akatubu baada yake
na akatengenea, basi hakika Yeye ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.
55. Na ndio hivi tunavyo zieleza Ishara ili ibainike njia
ya wakosefu.
56. Sema: Mimi nimekatazwa kuwaabudu hao mnao waomba badala
ya Mwenyezi Mungu. Sema: mimi sifuati matamanio yenu. Hivyo nitakuwa nimepotea,
na sitakuwa miongoni mwa walio ongoka.
57. Sema: Mimi nipo kwenye sharia iliyo wazi itokayo kwa
Mola wangu Mlezi, nanyi mnaikanusha. Mimi sinacho hicho mnacho kihimiza. Hapana
hukumu ila ya Mwenyezi Mungu. Yeye anasimulia yaliyo kweli; naye ni Mbora wa
kuhukumu kuliko wote.
58. Sema: Lau kuwa ninacho hicho mnacho kihimiza, ingeli
kwisha katwa shauri baina yangu na nyinyi. Na Mwenyezi Mungu anawashinda wote
kuwajua madhaalimu.
59. Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila
Yeye tu. Na Yeye anajua kilioko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila
analijua. Wala punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika
Kitabu kinacho bainisha.
60. Naye ndiye anaye kufisheni usiku, na anakijua mlicho
fanya mchana. Kisha Yeye hukufufueni humo mchana ili muda ulio wekwa utimizwe.
Kisha kwake Yeye ndiyo marejeo yenu, na tena akwambieni mliyo kuwa mkiyafanya.
61. Naye ndiye Mwenye nguvu za kushinda, aliye juu ya waja
wake. Na hukupelekeeni waangalizi, mpaka mmoja wenu yakimjia mauti wajumbe wetu
humfisha, nao hawafanyi taksiri.
62. Kisha watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa Haki.
Hakika, hukumu ni yake. Naye ni Mwepesi kuliko wote wanao hisabu.
63. Sema: Ni nani anaye kuokoeni katika giza la nchi kavu
na baharini? Mnamwomba kwa unyenyekevu na kwa siri, mkisema: Kama akituokoa na
haya bila ya shaka tutakuwa miongoni mwa wanao shukuru.
64. Sema: Mwenyezi Mungu hukuokoeni kutoka hayo, na kutoka
kila mashaka, na kisha nyinyi mnamshirikisha!
65. Sema: Yeye ndiye Muweza wa kukuleteeni adhabu kutoka
juu yenu au kutoka chini ya miguu yenu, au kukuleteeni fujo la mfarakano, na
kuwaonjesha baadhi yenu jeuri ya wenzao. Tazama vipi tunavyo zieleza Aya ili
wapate kufahamu.
66. Na watu wako wameikanusha, nayo ni Haki. Sema: Mimi
sikuwakilishwa juu yenu.
67. Kila khabari ina kipindi chake. Nanyi mtakuja jua.
68. Na unapo waona wanao ziingilia Aya zetu, basi jitenge
nao mpaka waingilie mazungumzo mengine. Na kama Shet'ani akikusahaulisha, basi
baada ya kutanabahi usikae pamoja na watu madhaalimu.
69. Wala wamchao Mungu hawana jukumu lolote kwao, lakini ni
kukumbusha, asaa wapate kujiepusha.
70. Waachilie mbali walio ifanya dini yao ni mchezo na
pumbao, na uhai wa dunia ukawaghuri. Nawe kumbusha kwayo, isije nafsi
ikaangamizwa kwa sababu ya iliyo yachuma, nayo haina mlinzi wala mwombezi ila
Mwenyezi Mungu. Na ingatoa kila fidia haitokubaliwa. Hao ndio walio angamizwa
kwa sababu ya yale waliyo yachuma. Wao watapata kinywaji cha maji ya moto
kabisa, na adhabu chungu.
71. Sema: Je, tumuombe asiye kuwa Mwenyezi Mungu ambae
hatufai wala hatudhuru, na turejee nyuma baada ya Mwenyezi Mungu kwisha tuhidi?
Tuwe kama ambao mashet'ani wamempumbaza katika ardhi, amebabaika? Anao marafiki
wanao mwita ende kwenye uwongofu, wakimwambia: Njoo kwetu! Sema: Hakika
uwongofu wa Mwenyezi Mungu ndio Uwongofu. Nasi tumeamrishwa tusilimu kwa Mola
Mlezi wa viumbe vyote,
72. Na mshike Sala, na mcheni Yeye, na kwake Yeye ndiko
mtako kusanywa.
73. Naye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi kwa Haki. Na
anaposema: Kuwa! Basi huwa. Kauli yake ni Haki. Na ufalme wote ni wake Siku
litapo pulizwa barugumu, Mjuzi wa yaliyo fichikana na yanayo onekana. Naye
ndiye Mwenye hikima na Mwenye khabari.
74. Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake, Azar:
Unayafanya masanamu kuwa ni miungu? Hakika mimi nakuona wewe na watu wako mmo
katika opotofu ulio wazi.
75. Na kadhaalika tulimwonyesha Ibrahim ufalme wa mbingu na
ardhi, na ili awe miongoni mwa wenye yakini.
76. Na ulipo muingilia usiku akiona nyota, akasema: Huyu ni
Mola Mlezi wangu. Ilipo tua akasema: Siwapendi wanao tua.
77. Alipo uona mwezi unachomoza alisema: Huyu ndiye Mola
Mlezi wangu. Ulipotua akasema: Kama Mola Mlezi wangu hakuniongoa, nitakuwa
katika kaumu walio potea.
78. Na alipo liona jua linachomoza akasema: Huyu ndiye Mola
Mlezi wangu. Huyu mkubwa kuliko wote. Lilipo tua, alisema: Enyi watu wangu!
Mimi simo katika hayo mnayo fanyia ushirikina.
79. Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu sawa sawa kwa aliye
ziumba mbingu na ardhi, wala mimi si miongoni mwa washirikina.
80. Na
watu wake wakamhoji. Akasema: Je, mnanihoji juu ya Mwenyezi Mungu, na hali Yeye
ameniongoa? Wala siogopi hao mnao washirikisha naye, ila Mola wangu Mlezi
akipenda kitu. Mola wangu Mlezi amekusanya ilimu ya kila kitu. Basi je,
hamkumbuki?
81. Na
vipi nivikhofu hivyo mnavyo vishirikisha, hali nyinyi hamkhofu kuwa nyinyi
mmemshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu ambacho hakukiteremshia uthibitisho. Basi
kundi gani katika mawili haya lina haki zaidi kupata amani, kama nyinyi mnajua?
82. Wale
ambao wameamini, na hawakuchanganya imani yao na dhulma - hao ndio watakao pata
amani na wao ndio walio ongoka.
83. Na
hizo ndizo hoja zetu tulizo mpa Ibrahim kuhojiana na watu wake. Tunamnyanyua
kwa vyeo tumtakaye. Hakika Mola Mlezi wako ni Mwenye hikima na Mwenye ujuzi.
84. Na
tukamtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaakub. Kila mmoja wao tulimwongoa. Na Nuhu
tulimwongoa kabla. Na katika kizazi chake tulimwongoa Daud na Suleiman na Ayyub
na Yusuf na Musa na Harun. Na hivi ndivyo tunavyo walipa wafanyao wema.
85. Na Zakaria na Yahya na Isa na Ilyas. Wote walikuwa
miongoni mwa watu wema.
86.Na Ismail, na Al Yasaa, na Yunus, na Lut'. Na wote
tuliwafadhilisha juu ya walimwengu wote.
87. Na kutokana na baba zao, na vizazi vyao na ndugu zao.
Na tukawateuwa na tukawaongoa kwenye Njia iliyo nyooka.
88. Hiyo ni hidaya ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo humhidi
amtakaye katika waja wake. Na lau wangeli mshirikisha yangeli waharibikia
waliyo kuwa wakiyatenda.
89. Hao ndio tulio wapa Vitabu na hukumu na Unabii. Ikiwa
hawa watayakataa hayo, basi tumekwisha yawakilisha kwa watu wasio yakataa.
90. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewahidi. Basi fuata
hidaya yao. Sema: Mimi sikuombeni ujira. Haya hayakuwa ila ni mawaidha kwa
walimwengu wote.
91. Na hawakumkadiria Mwenyezi Mungu kwa haki ya kadri
yake, walipo sema: Mwenyezi Mungu hakumteremshia mwanaadamu chochote. Sema: Nani
aliyo teremsha Kitabu alicho kuja nacho Musa, chenye nuru na uwongofu kwa watu,
mlicho kifanya kurasa kurasa mkizionyesha, na mengi mkiyaficha. Na mkafunzwa
mlio kuwa hamyajui nyinyi wala baba zenu? Sema: Mwenyezi Mungu. Kisha waache wacheze katika porojo lao.
92. Na hiki ni
Kitabu tulicho kiteremsha, kilicho barikiwa, chenye kuhakikisha yaliyo
tangulia, na ili uuwonye Mama wa Miji na walio pembezoni mwake. Na wenye
kuamini Akhera wanakiamini hichi, nao wanazihifadhi Sala zao.
93. Nani
dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzuliya uwongo Mwenyezi Mungu, au anaye sema:
Mimi nimeletewa wahyi; na hali hakuletewa wahyi wowote. Na yule anaye sema:
Nitateremsha kama alivyo teremsha Mwenyezi Mungu. Na lau ungeli waona
madhaalimu wanavyo kuwa katika mahangaiko ya mauti, na Malaika wamewanyooshea
mikono wakiwambia: Zitoeni roho zenu! Leo mtalipwa adhabu ya fedheha kwa sababu
ya mliyo kuwa mkiyasema juu ya Mwenyezi Mungu yasiyo ya haki, na mlivyo kuwa
mkizifanyia kiburi Ishara zake.
94. Nanyi
mlitujia wapweke kama tulivyo kuumbeni mara ya kwanza. Na mkayaacha nyuma yenu
yote tuliyo kupeni, na wala hatuwaoni hao waombezi wenu, ambao mlidai kuwa ni
washirika wa Mwenyezi Mungu kwenu. Yamekatika makhusiano baina yenu, na
yamekupoteeni mliyo kuwa mkidai.
95. Hakika
Mwenyezi Mungu ndiye mpasuaji mbegu na kokwa, zikachipua. Humtoa aliye hai kutoka
maiti, naye ni mtoaji maiti kutokana na aliye hai. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu. Basi
vipi mnageuzwa?
96. Ndiye anaye pambazua mwangaza wa asubuhi; na ameufanya
usiku kwa mapumziko na utulivu, na jua na mwezi kwenda kwa hisabu. Hayo ndiyo
makadirio ya Aliye tukuka Mwenye nguvu, Mwenye ujuzi.
97. Na Yeye ndiye aliye kuwekeeni nyota ili mwongoke kwazo
katika kiza cha bara na bahari. Hakika tumezichambua Ishara hizi kwa watu wanao
jua.
98. Na Yeye ndiye aliye kuzalisheni kutokana na nafsi moja.
Pako pahali pa kutulia na pa kupita njia. Hakika tumezichambua Ishara hizi kwa
watu wanao fahamu.
99. Na Yeye ndiye anaye teremsha maji kutoka mbinguni; na
kwayo tunatoa mimea ya kila kitu. Kutokana na baadhi yao tukatoa mimea ya
majani, tukatoa ndani yake punje zilizo pandana; na kutokana na mitende
yakatoka kwenye makole yake mashada yaliyo inama; na bustani za mizabibu na
mizaituni, na makomamanga, yaliyo fanana na yasiyo fanana. Angalieni matunda
yake yanapo zaa na yakawiva. Hakika katika hayo pana Ishara kwa watu wanao
amini.
100. Bado wamemfanyia Mwenyezi Mungu majini kuwa washirika
wake, na hali Yeye ndiye aliye waumba. Na wakamzulia, bila ya ujuzi wowote,
kuwa ana wana wa kiume na wa kike. Subhanahu, Ametakasika na ametukuka juu ya
hayo wanayo mbandikiza nayo!
|