51 - 100
51. Ambao waliifanya dini yao kuwa ni pumbao na mchezo, na
maisha ya dunia yakawadanganya. Basi leo Sisi tunawasahau kama walivyo usahau
mkutano wa Siku yao hii, na kwa sababu ya kule kuzikataa Ishara zetu.
52. Na hakika tumewaletea Kitabu tulicho kipambanua kwa
ilimu, uwongofu na rehema kwa watu wenye kuamini.
53. Je,
lipo wanalo lingojea isipo kuwa matokeo yake? Siku yatapo fika matokeo yake
watasema wale walio kisahau: Kweli Mitume wa Mola Mlezi wetu walileta Haki! Je,
tunao waombezi ili watuombee? Au turudishwe ili tufanye yasiyo kuwa yale tuliyo
kuwa tukiyafanya? Bila ya shaka wamejikhasiri nafsi zao, na yamewapotea waliyo
kuwa wakiyazua.
54. Hakika
Mola Mlezi wenu ni Mwenyezi Mungu aliye ziumba mbingu na ardhi katika siku
sita. Kisha akatawala juu ya Kiti cha Enzi. Huufunika usiku kwa mchana, ufuatao
upesi upesi. Na jua, na mwezi, na nyota zinazo tumika kwa amri yake. Fahamuni!
Kuumba na amri ni zake. Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe
vyote.
55.
Muombeni Mola wenu Mlezi kwa unyenyekevu na kwa siri. Hakika Yeye hawapendi
warukao mipaka.
56. Wala msifanye
uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwisha tengenezwa. Na muombeni kwa
kuogopa na kwa kutumai. Hakika rehema ya Mwenyzi Mungu iko karibu na wanao
fanya mema.
57. Na
Yeye ndiye anaye peleka pepo (za kuvuma) kuwa ni bishara kabla ya kufika rehema
yake. Hata hizo pepo zinapo beba mawingu mazito tunayachunga mpaka kwenye nchi
iliyo kufa. Kisha tunateremsha kwayo maji, ndio kama hivyo tukatolesha kila aina
ya matunda. Basi hali kadhaalika tunavyo wafufua wafu, ili mpate kukumbuka.
58. Na
ardhi njema, yenye udongo wa rutba, hutoa mimea yenye kukua vizuri yenye uhai,
kwa idhini ya Mola Mlezi wake. Na ardhi mbaya haitoi ila mimea michache,
isiyo na faida, tena kwa shida. Na hivyo ndivyo tunavyo zipambanua Ishara (Aya)
kwa watu wanao shukuru.
59. Tulimpeleka Nuhu kwa kaumu yake, naye akasema: Enyi
kaumu yangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku
iliyo kuu.
60. Wale
watukufu katika kaumu yake wakasema: Hakika sisi tunakuona wewe umo katika
upotofu ulio dhaahiri.
61. Akasema:
Enyi watu wangu! Mimi simo katika upotofu, lakini mimi ni Mtume nitokaye kwa
Mola Mlezi wa viumbe vyote.
62.
Nakufikishieni Ujumbe wa Mola Mlezi wangu, na ninakunasihini; na ninayajua kwa
Mwenyezi Mungu msiyo yajua nyinyi.
63. Je,
mnastaajabu kukujieni mawaidha yanayotoka kwa Mola Mlezi wenu kwa njia ya mtu aliye
ni mmoja katika nyinyi, ili akuonyeni na ili mumchemngu, na ili mpate
kurehemewa?
64. Basi
walimkanusha. Nasi tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye katika jahazi. Na
tukawazamisha wale walio kanusha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu vipofu.
65. Na kwa
A'adi tulimpeleka ndugu yao, Hud. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna mungu ila Yeye. Basi je, hamumchi?
66. Wakasema
watukufu wa wale walio kufuru katika kaumu yake: Sisi tunakuona umo katika
upumbavu, na hakika sisi tunakufikiria kuwa wewe ni katika waongo.
67. Akasema:
Enyi watu wangu! Mimi sina upumbavu. Lakini mimi ni Mtume niliye toka
kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote.
68. Nakufikishieni ujumbe wa Mola wangu Mlezi. Na mimi
kwenu ni mwenye kukunasihini, muaminifu.
69. Mnaona ajabu kukufikieni mawaidha yanayo toka kwa Mola
wenu Mlezi kwa mtu aliye mmoja wenu nyinyi ili akuonyeni? Na kumbukeni alivyo
kufanyeni mshike pahala pa kaumu ya Nuhu, na akakuzidisheni katika umbo. Basi
zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa.
70. Wakasema: Je! Umetujia ili tumuabudu Mwenyezi Mungu
peke yake, na tuyaache waliyo kuwa wakiyaabudu baba zetu? Basi tuletee hayo
unayo tuahidi, ukiwa miongoni mwa wasemao kweli.
71. Akasema: Bila ya shaka adhabu na ghadhabu zimekwisha
kukuangukieni kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Mnabishana nami kwa ajili ya majina
tu mliyo yaita nyinyi na baba zenu ambayo kwayo Mwenyezi Mungu hakuteremsha
uthibitisho? Basi ngojeni, mimi pia ni pamoja nanyi katika wanao ngoja.
72. Basi tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye kwa
rehema zetu, na tukakata mizizi ya wale walio zikanusha Ishara zetu, na
hawakuwa wenye kuamini.
73. Na kwa Thamud tulimpeleka ndugu yao, Saleh. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni
Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna
Mungu ila Yeye. Hakika imekwisha kukufikieni Ishara iliyo wazi kutoka kwa Mola
wenu Mlezi. Huyu ni ngamia jike wa Mwenyezi Mungu aliye ni Ishara kwenu. Basi
mwachieni ale kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimdhuru, isije
kukushukieni adhabu chungu.
74. Na
kumbukeni alivyo kufanyeni wa kushika pahala pa A'adi na akakuwekeni vizuri
katika nchi, mnajenga majumba ya fakhari katika nyanda zake, na mnachonga
majumba katika milima. Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu wala msitende
uovu katika nchi kwa ufisadi.
75.
Waheshimiwa wa kaumu yake wanao jivuna waliwaambia wanao onewa wenye kuamini
miongoni mwao: Je, mnaitakidi ya kwamba Saleh ametumwa na Mola Mlezi wake?
Wakasema: Hakika sisi tunayaamini yale aliyo tumwa.
76.
Wakasema wale wanao jivuna: Sisi tunayakataa hayo mnayo yaamini.
77. Na
wakamuuwa yule ngamia, na wakaasi amri ya Mola Mlezi wao, na wakasema: Ewe
Saleh! Tuletee unayo tuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume.
78. Basi
tetemeko la ardhi likawanyakua, na kulipo kucha wakawa majumbani mwao
kifudifudi wamekwisha kufa.
79. Basi
Saleh akwaacha na akasema: Enyi watu wangu! Nilikufikishieni Ujumbe wa Mola
wangu Mlezi, na nikakunasihini, lakini nyinyi hamwapendi wenye nasaha.
80. Na
tulimtuma Lut', alipo waambia watu wake: Je, mnafanya uchafu ambao
hajakutangulieni yeyote kwa uchafu huo katika viumbe vyote!
81. Hivyo
nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio mkwawacha wanawake? Kumbe nyinyi ni
watu wafujaji!
82. Na
haikuwa jawabu ya kaumu yake isipo kuwa kuambizana: Wafukuzeni katika mji wenu,
maana hao ni watu wanao jitakasa.
83. Basi
tukamwokoa yeye na watu wake, isipo kuwa mkewe, alikuwa miongoni mwa walio
bakia nyuma.
84. Na tukawamiminia mvua. Basi tazama jinsi ulivyo kuwa
mwisho wa wakosefu.
85. Na kwa watu wa Madyana tulimtuma ndugu yao Shua'ib. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni
Mwenyezi Mungu. Hamna mungu mwengine isipo kuwa Yeye. Imekwisha kufikieni hoja
wazi kutoka kwa Mola Mlezi wenu. Basi timizeni sawasawa vipimo na mizani, wala
msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye uharibifu katika nchi, baada ya kuwa
imekwisha tengenea. Hivi ndivyo bora kwenu ikiwa nyinyi ni Waumini.
86. Wala msikae katika kila njia mkitisha watu, na
kuwazuilia na Njia ya Mwenyezi Mungu wale wenye kumuamini, na mkataka njia
ipotoke. Na kumbukeni mlipo kuwa wachache, naye akakufanyeni kuwa wengi. Na
tazameni jinsi ulivyo kuwa mwisho wa mafisadi.
87. Na kama liko kundi miongoni mwenu lililo amini haya
niliyo tumwa, na kundi jengine halikuamini, basi subirini mpaka Mwenyezi Mungu
ahukumu baina yetu. Naye ndiye Mbora wa wenye kuhukumu.
88. WAHESHIMIWA WALIO TAKABARI katika kaumu yake wakasema:
Ewe Shua'ib! Tutakutoa wewe pamoja na wale walio kuamini katika mji wetu, au
mrejee katika mila yetu. Akasema: Je, ingawa tunaichukia?
89. Bila ya shaka itakuwa tumemzulia uwongo Mwenyezi Mungu tukirudi
katika mila yenu baada ya kwisha tuokoa nayo Mwenyezi Mungu. Wala haiwi kwetu
sisi kuirejea mila hiyo, ila akitaka Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wetu. Ujuzi wa
Mola Mlezi wetu umeenea katika kila kitu. Kwa Mwenyezi Mungu tunategemea. Ewe Mola Mlezi wetu! Tuhukumie baina
yetu na kaumu yetu kwa haki, nawe ndiye mbora wa wanao hukumu.
90. Na waheshimiwa walio kufuru katika kaumu yake wakasema:
Mkimfuata Shua'ib, basi hakika hapo nyinyi mtakuwa mlio khasiri.
91. Basi tetemeko la ardhi likawanyakua, na wakaamkia
majumbani mwao wamejifudikiza, wamekwisha kufa.
92. Wale walio mkanusha Shua'ib wakawa kama kwamba
hawakuwako. Walio mkanusha Shua'ib ndio walio kuwa wenye kukhasiri.
93. Basi akawaachilia mbali na akasema: Enyi kaumu yangu!
Nimekufikishieni Ujumbe wa Mola Mlezi wangu, na nimekunasihini; basi vipi
niwahuzunikie watu makafiri?
94. Na hatukumtuma Nabii yeyote katika mji ila
tuliwapatiliza wakaazi wake kwa taabu na mashaka ili wapate kunyenyekea.
95. Kisha Sisi hubadilisha mahala pa ubaya kwa wema, hata
wakazidi, na wakasema: Taabu na raha ziliwafikia baba zetu. Basi kwa ghafla
tukawashika, hali ya kuwa hawajatambua.
96. Na lau kuwa watu wa miji wangeli amini na wakamchamngu,
kwa yakini tungeli wafungulia baraka kutoka mbinguni na katika ardhi. Lakini
walikanusha basi tukawapatiliza kwa sababu ya yale waliyo kuwa wakiyachuma.
97. Je, watu wa mijini wameaminisha ya kuwa adhabu yetu
haitawafika usiku, nao wamelala?
98. Au watu wa mijini wameaminisha ya kuwa adhabu yetu
haitawafika mchana, nao wanacheza?
99. Je, wamejiaminisha na mipango ya Mwenyezi Mungu? Kwani
hawajiaminishi na mipango ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye kukhasiri.
100. Je, hawahidiki hawa wanao rithi ardhi baada ya wale
wenyewe kwamba tukitaka tutawapatiliza kwa madhambi yao, na tutapiga muhuri juu
ya nyoyo zao, na kwa hivyo hawatasikia?
|