51 - 100
51. Sema: Halitusibu ila alilo tuandikia Mwenyezi Mungu.
Yeye ndiye Mola wetu Mlinzi. Na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu!
52. Sema: Hivyo mnatutazamia litupate lolote isipo kuwa
moja katika mema mawili? Na sisi tunakutazamieni kuwa Mwenyezi Mungu
akufikishieni adhabu itokayo kwake, au kutokana na mikono yetu. Basi ngojeni,
nasi tunangoja pamoja nanyi.
53. Sema: Toeni mkipenda msipende. Hakitopokelewa kitu
kwenu, kwani nyinyi ni watu wapotovu.
54. Na hawakuzuiliwa kukubaliwa michango yao ila kwa kuwa
walimkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawaji kwenye Sala ila kwa uvivu,
wala hawatoi michango ila nao wamechukia.
55.
Yasikufurahishe mali yao wala wana wao. Hakika Mwenyezi Mungu anataka
kuwaadhibu kwayo hapa duniani, na zitoke roho zao na hali wao ni makafiri.
56. Na
wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wao ni katika nyinyi, wala wao si katika
nyinyi. Lakini ni watu wanao ogopa.
57. Lau
kama wangeli pata pa kukimbilia au mapango au pahala pa kuingia basi wangeli
fyatuka mbio kuelekea huko.
58. Na
miongoni mwao wapo wanao kusengenya katika kugawa sadaka. Wanapo pewa wao
huridhika. Na wakito pewa hukasirika.
59. Na
laiti wao wangeli ridhia kile alicho wapa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na
wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosheleza, Mwenyezi Mungu atatupa katika fadhila
yake - na pia Mtume wake; hakika sisi ni wenye kumtaka Mwenyezi Mungu!
60. Wa
kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanao zitumikia, na wa kutiwa nguvu
nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya
Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni waajibu ulio faridhiwa na Mwenyezi Mungu.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
61. Na
miongoni mwao wapo wanao muudhi Nabii na kusema: Yeye huyu ni sikio tu. Sema:
Basi ni sikio la kheri kwenu. Anamuamini Mwenyezi Mungu, na ana imani na
Waumini, naye ni rehema kwa wanao amini miongoni mwenu. Na wanao muudhi Mtume
wa Mwenyezi Mungu watapata adhabu chungu.
62. Wanakuapieni Mwenyezi Mungu ili kukuridhisheni nyinyi,
hali ya kuwa wanao stahiki zaidi kuridhishwa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake,
lau kama wao ni Waumini.
63. Je, hawajui ya kwamba anaye shindana na Mwenyezi Mungu
na Mtume wake, basi huyo atapata Moto wa Jahannamu adumu humo? Hiyo ndiyo
hizaya kubwa.
64. Wanaafiki wanaogopa isije teremshwa Sura itakayo
watajia yaliyomo katika nyoyo zao. Sema: Fanyeni mzaha! Hakika Mwenyezi Mungu
atayatoa nje hayo mnayo yaogopa.
65. Na ukiwauliza, wanasema: Sisi tulikuwa tukipiga porojo
na kucheza tu. Sema: Mlikuwa mkimfanyia maskhara Mwenyezi Mungu na Ishara zake
na Mtume wake?
66. Msitoe udhuru; mmekwisha kufuru baada ya kuamini kwenu!
Tukilisamehe kundi moja kati yenu, tutaliadhibu kundi jingine kwa kuwa wao ni
wakosefu.
67. Wanaume wanaafiki na wanawake wanaafiki, wote ni hali
moja. Huamrisha maovu na huyakataza mema, na huifumba mikono yao. Wamemsahau
Mwenyezi Mungu, basi na Yeye pia amewasahau. Hakika wanaafiki ndio wapotofu.
68. Mwenyezi Mungu amewaahidi wanaafiki wanaume na
wanaafiki wanawake na makafiri Moto wa Jahannamu kudumu humo. Hayo yanawatosha,
na Mwenyezi Mungu amewalaani; nao wana adhabu milele.
69. Ni kama wale walio kuwa kabla yenu. Walikuwa wana nguvu
na mali na watoto zaidi kuliko nyinyi. Basi walistarehea fungu lao, na nyinyi
mnastarehea fungu lenu, kama walivyo starehe kwa fungu lao wale walio kuwa
kabla yenu. Na nyinyi mkazama katika maovu kama wao walivyo zama. Hao ndio
ambao vitendo vyao vimeharibika katika dunia na Akhera; na hao ndio walio
khasiri.
70. Je, hazikuwafikia khabari za walio kuwa kabla yao -
kaumu ya Nuhu, na A'ad, na Thamud, na kaumu ya Ibrahim, na watu wa Madyana, na
miji iliyo pinduliwa chini juu? Mitume wao waliwafikia kwa hoja zilizo wazi.
Basi Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, walakini wao walikuwa
wakijidhulumu wenyewe.
71. Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni
marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika Sala, na hutoa
Zaka, na humt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
72. Mwenyezi Mungu amewaahidi Waumini wanaume na Waumini
wanawake Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na makaazi mema katika
Bustani za kudumu, na Radhi za Mwenyezi Mungu ndio kubwa kuliko yote. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
73. Ewe
Nabii! Pambana na makafiri na wanaafiki, na wakazanie. Na makaazi yao ni
Jahannamu, na huo ndio mwisho mbaya.
74.
Wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hawakusema; nao wamekwisha sema neno la
ukafiri, na wakakufuru baada ya kusilimu kwao. Na wakajihimu kufanya ambayo
hawakuweza kuyafikia. Na hawakuchukia ila kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake
amewatajirisha kutokana na fadhila zake. Wakitubu itakuwa kheri kwao, na
wakigeuka Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu chungu duniani na Akhera. Na wala
hawana katika ardhi mlinzi wala wa kuwanusuru.
75. Na
miongoni mwao wapo walio muahidi Mwenyezi Mungu kwa kusema: Akitupa katika
fadhila yake hapana shaka tutatoa sadaka, na tutakuwa katika watendao mema.
76. Alipo
wapa katika fadhila yake wakaifanyia ubakhili na wakageuka, na huku wakipuuza.
77. Basi
akawalipa unaafiki kuutia nyoyoni mwao mpaka Siku watapo kutana naye, kwa
sababu ya kuwa walimkhalifu Mwenyezi Mungu katika yale waliyo muahidi, na kwa
sababu ya kusema kwao uwongo.
78. Je,
hawajui kwamba Mwenyezi Mungu anajua siri zao na minong'ono yao, na kwamba
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua sana ya ghaibu?
79. Wale
wanao wabeuwa Waumini wanao toa sadaka nyingi na wasio nacho cha kutoa ila
kadri ya juhudi yao, basi huwakejeli. Mwenyezi Mungu atawakejeli wao! Nao
watapata adhabu chungu!
80.
Waombee msamaha au usiwaombee. Hata ukiwaombea msamaha mara sabiini, Mwenyezi
Mungu hatawasamehe. Hayo ni kwa sababu ya kuwa wao wamemkataa Mwenyezi Mungu na
Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotofu.
81.
Walifurahi walio achwa nyuma kwa kule kubakia kwao nyuma na kumuacha Mtume wa
Mwenyezi Mungu. Na walichukia kupigana Jihadi kwa mali zao na nafsi zao, na
wakasema: Msitoke nje katika joto! Sema: Moto wa Jahannamu una joto zaidi,
laiti wangeli fahamu!
82. Basi nawacheke kidogo; watalia sana. Hayo ni malipo ya
yale waliyo kuwa wakiyachuma.
83. Basi Mwenyezi Mungu akikurudisha kwenye kikundi kimoja
miongoni mwao - na wakakutaka idhini ya kutoka - sema: Nyinyi hamtatoka pamoja
nami kabisa, wala hamtapigana na adui pamoja nami. Nyinyi mliridhia kukaa nyuma
mara ya kwanza, basi kaeni pamoja na hao watakao bakia nyuma.
84. Wala usimsalie kabisa yeyote katika wao akifa, wala
usisimame kaburini kwake. Hakika hao wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake,
na wakafa na hali ni wapotofu.
85. Wala zisikushitue mali zao na watoto wao. Mwenyezi
Mungu anataka kuwaadhibu kwa hayo katika dunia; na zitoke roho zao na hali wao
ni makafiri.
86. Na inapo teremshwa Sura isemayo: Muaminini Mwenyezi
Mungu na piganeni Jihadi pamoja na Mtume wake, wale wenye nguvu miongoni mwao
hukutaka ruhusa na husema: Tuache tuwe pamoja na wanao kaa nyuma!
87. Wameridhia kuwa pamoja na wabakiao nyuma, na nyoyo zao
zikapigwa muhuri; kwa hivyo hawafahamu.
88. Lakini Mtume na wale walio amini pamoja naye waliwania
Jihadi kwa mali zao na nafsi zao. Hao ndio watakao pata kheri nyingi, na hao
ndio wenye kufanikiwa.
89. Mwenyezi Mungu amewatengenezea Bustani zipitazo mito
kati yake, wadumu humo. Huko ndiko
kufuzu kukubwa.
90. Na walikuja
wenye kutoa udhuru katika Mabedui ili wapewe ruhusa, na wakakaa wale walio
mwambia Mwenyezi Mungu na Mtume wake uwongo. Itawafika walio kufuru katika wao
adhabu chungu.
91. Hapana
lawama kwa wanyonge, wagonjwa, na wasio pata cha kutumia, maadamu wanamsafia
niya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hapana njia ya kuwalaumu wanao fanya wema.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
92. Wala wale
walio kujia ili uwachukue ukasema: Sina kipando cha kukuchukueni. Tena wakarudi
na macho yao yanamiminika machozi kwa huzuni ya kukosa cha kutoa.
93. Ipo njia ya
kuwalaumu wale wanao kuomba ruhusa wasende vitani na hali wao ni matajiri.
Wameridhia kuwa pamoja na wanao bakia nyuma. Na Mwenyezi Mungu amewapiga muhuri
juu ya nyoyo zao. Kwa hivyo hawajui.
94.
WATAKUTOLEENI UDHURU mtapo warudia. Sema: Msitoe udhuru; hatukuaminini.
Mwenyezi Mungu amekwisha tueleza khabari zenu. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake
wataviona vitendo vyenu. Kisha mtarudishwa kwa Mjuzi wa ya siri na ya dhaahiri;
naye atakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
95. Watakuapieni
kwa Mwenyezi Mungu mtakapo rudi kwao ili muwaachilie mbali. Basi
waachilieni mbali. Hakika hao ni najsi, na makaazi yao ni Jahannamu, kuwa ni
malipo kwa waliyo kuwa wakiyachuma.
96. Wanakuapieni ili muwe radhi nao. Basi hata mkiwa radhi
nao nyiye, Mwenyezi Mungu hawi radhi na watu wapotofu.
97. Mabedui wamezidi sana katika ukafiri na unaafiki, na
wameelekea zaidi kutojua mipaka ya aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu juu ya Mtume
wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima.
98. Na katika Mabedui hao wapo wanao fikiri kuwa wanayo
yatoa ni gharama ya bure, na wanakungojeleeni mambo yakugeukieni. Mageuko maovu
yatakuwa juu yao! Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
99. Na katika Mabedui wapo wanao muamini Mwenyezi Mungu na
Siku ya Mwisho, na wanaitakidi kuwa wanayo yatoa ndiyo ya kuwasogeza kwa
Mwenyezi Mungu na ya kuwapatia dua za Mtume. Naam! Hayo ni kweli mambo ya kuwasogeza.
Mwenyezi Mungu atawaingiza katika rehema yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
maghfira Mwenye kurehemu.
100. Na wale walio tangulia, wa kwanza, katika Wahajiri na
Ansari, na walio wafuata kwa wema, Mwenyezi Mungu ameridhika nao, na wao
wameridhika naye; na amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo
milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
|