51 - 100
51. Tena je! Ikisha tokea mtaiamini? Je! Ndio sasa tena? Na
nyinyi mlikuwa mkiihimiza.
52. Kisha walio dhulumu wataambiwa: Onjeni adhabu ya
kudumu. Kwani mtalipwa isipo kuwa yale mliyo kuwa mkiyachuma?
53. Na wanakuuliza: Je! Ni kweli hayo? Sema: Ehe! Naapa kwa
Mola wangu Mlezi! Hakika hayo ni kweli, na wala nyinyi hamshindi!
54. Na lau kuwa kila nafsi iliyo dhulumu inamiliki kila
kiliomo duniani, bila ya shaka ingeli toa vyote kujikombolea. Na watakapo iona
adhabu wataficha majuto. Na patahukumiwa baina yao kwa uadilifu, nao
hawatadhulumiwa.
55. Jueni kuwa hakika vyote viliomo katika mbingu na katika
ardhi ni vya Mwenyezi Mungu. Jueni kuwa hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya
haki. Lakini wengi wao
hawajui.
56. Yeye
ndiye anaye fufua na anaye fisha. Na kwake mtarejeshwa.
57. Enyi
watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na poza kuponyesha
yaliyomo vifuani, na uwongofu, na rehema kwa Waumini.
58. Sema:
Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake! Basi nawafurahi kwa hayo.
Haya ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya.
59. Sema: Je! Mwaonaje zile riziki alizo kuteremshieni
Mwenyezi Mungu, nanyi mkafanya katika hizo nyengine haramu na nyengine halali.
Sema: Je! Mwenyezi Mungu amekuruhusuni, au mnamzulia Mwenyezi Mungu tu?
60. Na nini dhana ya wanao mzulia Mwenyezi Mungu kwa Siku
ya Kiyama? Hakika Mwenyezi Mungu ana fadhila juu ya watu, lakini wengi wao
hawashukuru.
61. Na huwi katika jambo lolote, wala husomi sehemu yoyote
katika Qur'ani, wala hamtendi kitendo chochote ila Sisi huwa ni mashahidi juu
yenu mnapo shughulika nayo. Na hakifichikani kwa Mola wako Mlezi chenye uzito
hata wa chembe katika ardhi na katika mbingu, wala kidogo kuliko hicho wala
kikubwa ila kimo katika Kitabu kilicho wazi.
62. Jueni kuwa vipenzi vya Mwenyezi Mungu hawatakuwa na
khofu wala hawatahuzunika.
63. Hao ni ambao wameamini na wakawa wanamcha Mungu.
64. Wao wana bishara njema katika maisha ya dunia na katika
Akhera. Hapana mabadiliko katika maneno ya Mwenyezi Mungu. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
65. Wala
yasikuhuzunishe maneno yao. Hakika utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu. Yeye
ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua.
66. Jueni
kuwa ni vya Mwenyezi Mungu vyote viliomo mbinguni na ardhinii. Na wala
hawawafuati hao wanao waomba badala ya Mwenyezi Mungu kuwa ni washirika wake. Wao
hawafuati ila dhana tu, na hawasemi ila uwongo.
67. Yeye ndiye aliye kujaalieni usiku mpate kutulia humo,
na mchana wa kuonea. Hakika katika haya zipo Ishara kwa watu wanao sikia.
68. Wamesema: Mwenyezi Mungu ana mwana. Subhanahu, Aliye
takasika! Yeye ni Mkwasi, Mwenye Kujitosheleza. Vyote viliomo katika mbingu na
katika ardhi ni vyake peke yake. Nyinyi hamna uthibitisho wowote wa haya! Mnamzulia Mwenyezi Mungu msiyo
yajua?
69. Sema:
Hao wanao mzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawatafanikiwa.
70. Hiyo
ni starehe ya katika dunia tu, kisha marejeo yao ni kwetu. Tena tutawaonjesha
adhabu kali kwa sababu ya kukufuru kwao.
71. Wasomee
khabari za Nuhu alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Ikiwa kukaa kwangu
nanyi na kukumbusha kwangu kwa Ishara za Mwenyezi Mungu kunakutieni mashaka
basi mimi namtegemea Mwenyezi Mungu. Nanyi tengezeni mambo yenu pamoja na
washirika wenu, na wala mambo yenu yasifichikane kwenu. Kisha nihukumuni, wala
msinipe muhula.
72. Lakini mkigeuka, basi mimi sikukuombeni ujira. Ujira
wangu hauko ila kwa Mwenyezi Mungu. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa Waislamu.
73. Wakamkanusha. Basi tukamwokoa, pamoja na walio kuwa naye,
katika jahazi. Na tukawafanya wao ndio walio bakia, na tukawazamisha walio
zikanusha Ishara zetu. Basi angalia vipi ulikuwa mwisho wa walio onywa.
74. Kisha baada yake tukawatuma Mitume kwa watu wao. Nao
wakawajia kwa Ishara zilizo wazi. Lakini hawakuwa wenye kuyaamini waliyo
yakanusha kabla yake. Ndio kama hivyo tunapiga muhuri juu ya nyoyo za warukao
mipaka.
75. Kisha baada yao tukamtuma Musa na Haruni kwa Firauni na
waheshimiwa wake, kwa Ishara zetu. Wakajivuna, na wakawa watu wakosefu.
76. Basi ilipo wajia Haki kutoka kwetu walisema: Hakika huu
ni uchawi dhaahiri.
77. Akasema Musa: Mnasema hivi juu ya Haki ilipo kujieni? Huu ni uchawi? Na wachawi hawafanikiwi!
78. Wakasema:
Je! Umetujia ili utuachishe tuliyo wakuta nayo baba zetu, na mpate nyinyi wawili
ukubwa katika nchi? Wala sisi hatukuaminini nyinyi.
79. Na Firauni akasema: Nileteeni kila mchawi mjuzi!
80. Basi walipo kuja wachawi, Musa aliwaambia: Tupeni
mnavyo tupa!
81. Walipo tupa, Musa alisema: Mliyo leta ni uchawi. Hakika
Mwenyezi Mungu haitengenezi kazi ya waharibifu.
82. Na Mwenyezi Mungu huhakikisha Haki kwa maneno yake,
hata wanga chukia wakosefu
83. Basi hawakumuamini Musa isipo kuwa baadhi ya vijana vya
kaumu yake, kwa kumwogopa Firauni na wakuu wao wasiwatese. Kwani hakika Firauni
alikuwa jeuri katika nchi. Na kwa yakini alikuwa miongoni mwa walio pita kiasi.
84. Na Musa alisema: Enyi watu wangu! Ikiwa nyinyi
mmemuamini Mwenyezi Mungu, basi mtegemeeni Yeye, ikiwa nyinyi ni Waislamu.
85. Wakasema: Tunamtegemea Mwenyezi Mungu. Ewe Mola wetu
Mlezi! Usitufanye wenye kutiwa misukosuko na hao watu madhaalimu.
86. Na utuokoe kwa rehema yako na watu makafiri.
87. Na tukampelekea Musa na ndugu yake wahyi huu:
Watengenezeeni majumba watu wenu katika Misri na zifanyeni nyumba zenu ndio
mwahali mwa ibada, na mshike Sala, na wabashirie Waumini.
88. Na Musa akasema: Mola wetu Mlezi! Hakika wewe umempa
Firauni na wakuu wake mapambo na mali katika maisha ya dunia. Hivyo wanapoteza
watu na Njia yako. Mola wetu Mlezi! Yafutilie mbali mali yao na zifunge nyoyo
zao, wasiamini mpaka waione adhabu chungu.
89. Mwenyezi Mungu akasema: Maombi yenu yamekubaliwa. Basi
simameni sawa sawa, wala msifuate njia za wale wasio jua.
90. Tukawavusha bahari Wana wa Israili, na Firauni na
askari wake wakawafuatia kwa dhulma na uadui. Hata Firauni alipo kuwa anataka
kuzama akasema: Naamini kuwa hapana mungu ila yule waliye muamini Wana wa
Israili, na mimi ni miongoni mwa walio nyenyekea!
91. Ala! Sasa? Na hali uliasi kabla yake na ukawa miongoni
mwa mafisadi!
92. Leo, basi, tutakuokoa kwa mwili wako, ili uwe Ishara
kwa ajili ya walio nyuma yako. Na hakika watu wengi wameghafilika na Ishara
zetu.
93. Na hakika tuliwaweka Wana wa Is raili kikao chema, na
tukawaruzuku vitu vizuri. Nao hawakukhitalifiana mpaka ilipo wafikia ilimu.
Hakika Mola wako Mlezi atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyo
kuwa wakikhitalifiana.
94. Na ikiwa unayo shaka katika tuliyo kuteremshia, basi
waulize wasomao Kitabu kabla yako. Kwa yakini imekwisha kujia Haki kutoka kwa
Mola wako Mlezi. Basi usiwe miongoni mwa wenye shaka.
95. Na kabisa usiwe miongoni mwa wale wanao zikanusha
Ishara za Mwenyezi Mungu, usije kuwa katika walio khasiri.
96. Hakika wale ambao neno la Mola wako Mlezi limekwisha
thibitika juu yao, hawataamini,
97. Ijapo kuwa itawajia kila Ishara, mpaka waione adhabu
iliyo chungu.
98. Kwa nini usiwepo mji mmoja ukaamini na Imani yake
ikawafaa - isipo kuwa kaumu Yunus? Waliamini na Sisi tukawaondolea adhabu ya
hizaya katika maisha ya dunia, na tukawastarehesha kwa muda.
99. Angeli taka Mola wako Mlezi wangeli amini wote waliomo
katika ardhi. Je, wewe utawalazimisha watu kwa nguvu mpaka wawe Waumini?
100. Na hawezi mtu kuamini ila kwa idhini ya Mwenyezi
Mungu. Naye hujaalia adhabu iwafike wasio tumia akili zao.
|