1 - 50
1. Alif
Lam Ra. Hiki ni Kitabu ambacho Aya zake zimewekwa wazi, kisha zikapambanuliwa,
kilicho toka kwa Mwenye Hikima na Mwenye Khabari,
2. Ili
msimuabudu isipo kuwa Allah, Mwenyezi Mungu. Hakika mimi kwenu ni mwonyaji na
mbashiri nitokae kwake.
3. Na ili
mumwombe msamaha Mola wenu Mlezi, kisha mtubie kwake. Atakustarehesheni starehe
nzuri mpaka muda maalumu. Na atampa kila mwenye fadhila, fadhila yake. Na ikiwa
mtakengeuka basi mimi nakukhofieni adhabu ya hiyo Siku Kubwa.
4. Marejeo
yenu ni kwa Mwenyezi Mungu tu. Naye ni Muweza wa kila kitu.
5. Hebu
angalia! Ati wanafunika vilivyomo vifuani mwao ili wamfiche Mwenyezi Mungu!
Jueni kuwa wanapo jigubika nguo zao Yeye anajua wanayo yaficha na wanayo
yatangaza. Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
6. NA
HAKUNA mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Naye
anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu chenye kubainisha.
7. Na Yeye
ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Na Kiti chake cha Enzi
kilikuwa juu ya maji, ili akufanyieni mtihani ajuulikane ni nani miongoni mwenu
mzuri zaidi wa vitendo. Na wewe ukisema: Nyinyi hakika mtafufuliwa baada ya
kufa; wale walio kufuru husema: Hayakuwa haya ila ni uchawi uliyo wazi.
8. Na
tukiwacheleweshea adhabu mpaka muda ulio kwisha hisabiwa wao husema: Nini
kinacho izuia hiyo adhabu? Jueni! Siku itakapo wajia basi haitoondolewa hiyo
kwao. Na yatawazunguka yale waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha.
9. Na
tukimwonjesha mtu rehema inayo toka kwetu, kisha tukamwondolea, hukata tamaa
akakufuru.
10. Na
tukimwonjesha neema baada ya madhara yaliyo mpata husema: Taabu zimekwisha
niondokea. Hakika yeye hujitapa na kutafakhari.
11. Ila wale walio subiri wakatenda mema. Hao watapata
msamaha na ujira mkubwa.
12. Basi labda utaacha baadhi ya yale yaliyo funuliwa
kwako, na kifua kitaona dhiki kwa hayo, kwa sababu wanasema: Mbona
hakuteremshiwa khazina, au wakaja naye Malaika? Wewe ni mwonyaji tu, na
Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa kila kitu.
13. Au wanasema: Ameizua? Sema: Basi leteni Sura kumi
zilizo zuliwa mfano wa hii, na waiteni muwawezao badala ya Mwenyezi Mungu,
ikiwa mnasema kweli.
14. Na wasipo kuitikieni, basi jueni ya kwamba (hii
Qur'ani) imeteremshwa kwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu, na kwamba hapana mungu ila
Yeye. Basi je! Nyinyi ni Waislamu?
15. Wanao taka
maisha ya dunia na pumbao lake tutawalipa humo vitendo vyao kaamili. Na wao humo hawatopunjwa.
16. Hao
ndio ambao hawatakuwa na kitu Akhera ila Moto, na yataharibika waliyo yafanya,
na yatapotea bure waliyo kuwa wakiyatenda.
17. Basi
je, mtu aliye na dalili wazi itokayo kwa Mola wake Mlezi, inayo fuatwa na
shahidi anaye toka kwake, na kabla yake kilikuwa Kitabu cha Musa kilicho kuwa
mwongozi na rehema - hao wanamuamini, na anaye mkataa katika makundi, basi Moto
ndio pahala pa miadi yao. Basi usiwe na shaka juu ya hayo. Hii ni Haki itokayo
kwa Mola wako Mlezi; lakini watu wengi hawaamini.
18. Na
nani aliye dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo? Hao
watahudhurishwa mbele ya Mola wao Mlezi, na mashahidi watasema: Hawa ndio walio
mtungia uwongo Mola wao Mlezi. Laana ya Mwenyezi Mungu iwapate walio dhulumu,
19. Ambao
wanazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanaitakia ipotoke, na wanaikataa Akhera.
20. Hao
hawawezi kushinda katika ardhi, wala hawana walinzi isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Watazidishiwa
adhabu. Hawakuwa wakiweza kusikia wala hawakuwa wakiona.
21. Hao
ndio walio zikhasiri nafsi zao, na yakawapotea waliyo kuwa wakiyazua.
22. Bila
ya shaka hakika wao ndio wenye kukhasiri huko Akhera.
23. Hakika
wale walio amini,na wakatenda mema, na wakanyenyekea kwa Mola wao Mlezi, hao
ndio watu wa Peponi, na humo watadumu.
24. Mfano wa
makundi mawili ni kama kipofu kiziwi, na mwenye kuona na anasikia. Je, wawili
hawa wanakuwa sawa kwa kufananishwa? Basi, je, hamfikiri?
25. Na
Sisi tulimtuma Nuhu kwa watu wake, akawaambia: Hakika mimi ni mwonyaji kwenu
ninaye bainisha,
26. Ya
kwamba msimuabudu isipo kuwa Mwenyezi Mungu tu. Hakika mimi ninakukhofieni
adhabu ya Siku Chungu.
27. Na
wakasema wakuu walio kufuru katika kaumu yake: Hatukuoni wewe ila ni mtu tu
kama sisi, wala hatukuoni wamekufuata ila wale walio kuwa kwetu watu duni,
wasio kuwa na akili. Wala hatukuoneni kuwa mna ubora wowote kutushinda sisi. Bali
tuna hakika nyinyi ni waongo.
28. Akasema: Enyi watu wangu! Hebu fikirini! Ikiwa mimi
ninayo hoja wazi iliyo toka kwa Mola wangu Mlezi, na amenipa rehema kutoka
kwake, nayo ikakufichikieni; je, tukulazimisheni kuikubali hali nyinyi
mnaichukia?
29. Na enyi watu wangu! Mimi sikuombeni mali kwa ajili ya
haya. Mimi sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu; na mimi sitawafukuza walio amini.
Hakika wao watakutana na Mola wao Mlezi, lakini mimi nakuoneni mnafanya ujinga.
30. Na enyi watu wangu! Ni nani atakaye nisaidia kwa
Mwenyezi Mungu nikiwafukuza hawa? Basi je, hamfikiri?
31. Wala sikwambiini kuwa nina khazina za Mwenyezi Mungu;
wala kuwa mimi najua mambo ya ghaibu; wala sisemi: Mimi ni Malaika. Wala
siwasemi wale ambao yanawadharau macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa kheri
- Mwenyezi Mungu anajua yaliomo katika nafsi zao - hapo bila ya shaka ninge
kuwa miongoni mwa wenye kudhulumu.
32. Wakasema: Ewe Nuhu! Umejadiliana, na umekithirisha
kutujadili. Basi tuletee hayo unayo tuahidi, ukiwa miongoni mwa wasemao kweli.
33. Akasema: Mwenyezi Mungu atakuleteeni akipenda. Wala
nyinyi si wenye kumshinda.
34. Wala nasaha yangu haikufaini kitu nikitaka
kukunasihini, ikiwa Mwenyezi Mungu anataka kukuachieni mpotee. Yeye ndiye Mola
wenu Mlezi; na kwake mtarejeshwa.
35. Au ndio wanasema: Ameizua? Sema: Ikiwa nimeizua, basi
kosa hilo ni juu yangu, na mimi sikhusiki na makosa myatendayo.
36. Na akafunuliwa Nuhu akaambiwa: Hataamini yeyote katika
watu wako ila wale walio kwisha amini. Basi usisikitike kwa waliyo kuwa
wakiyatenda.
37. Na unda jahazi mbele ya macho yetu na kwa mujibu wa
ufunuo wetu. Wala usinisemeze kuwatetea walio dhulumu. Kwani hao bila ya shaka
watazamishwa.
38. Na akawa anaunda jahazi, na kila wakipita wakuu wa
kaumu yake wakimkejeli. Yeye akasema: Ikiwa nyinyi mnatukejeli na sisi
tunakukejelini kama mnavyo tukejeli.
39. Nanyi mtakuja jua ni nani itakaye mfikia adhabu ya
kumhizi, na itakaye mteremkia adhabu ya kudumu.
40.Hata ilipo kuja amri yetu, na tanuri ikafoka maji,
tulisema: Pakia humo wawili wawili, dume na jike, kutoka kila aina, na ahali
zako, isipo kuwa wale ambao imekwisha wapitia hukumu; na watu walio amini. Na
hawakuamini pamoja naye ila wachache tu.
41. Na akasema: Pandeni humo kwa Bismillahi, Kwa Jina la
Mwenyezi Mungu, kwenda kwake na kusimama kwake. Hakika Mola wangu Mlezi ni
Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
42. Ikawa inakwenda nao katika mawimbi kama milima. Na Nuhu
akamwita mwanawe naye alikuwa mbali: Ewe mwanangu! Panda pamoja nasi, wala
usiwe pamoja na makafiri.
43. Akasema: Nitakimbilia mlimani unilinde na maji. (Nuhu)
akasema: Leo hapana wa kulindwa na amri ya Mwenyezi Mungu ila aliye mrehemu mwenyewe.
Na wimbi likawatenganisha, akawa katika walio zama.
44. Na ikasemwa: Ewe ardhi! Meza maji yako. Na Ewe mbingu!
Jizuie. Basi maji yakadidimia chini, na amri ikapitishwa, na (jahazi)
likasimama juu ya (mlima) wa Al Juudiy. Na ikasemwa: Wapotelee mbali watu walio
dhulumu!
45. Na Nuhu alimwomba Mola wake Mlezi: Ee Mola Mlezi wangu!
Hakika mwanangu ni katika ahali zangu, na hakika ahadi yako ni haki. Na Wewe ni
Mwenye haki kuliko mahakimu wote.
46. Akasema: Ewe Nuhu! Huyu si katika ahali zako. Mwendo
wake si mwema. Basi usiniombe jambo usio na ujuzi nalo. Mimi nakuwaidhi usije
ukawa miongoni mwa wajinga.
47. Nuhu akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Mimi najikinga
kwako nisikuombe nisio na ujuzi nalo. Na kama hunisamehe na ukanirehemu,
nitakuwa katika walio khasiri.
48. Ikasemwa:
Ewe Nuhu! Shuka kwa salama itokayo kwetu, na baraka nyingi juu yako na juu ya
watu walio pamoja nawe. Na zitakuwapo kaumu tutakazo zistarehesha, na kisha
zitashikwa na adhabu chungu itokayo kwetu.
49. Hizi ni
katika khabari za ghaibu tunazo kufunulia. Hukuwa ukizijua wewe, wala watu
wako, kabla ya hii. Basi subiri! Hakika Mwisho ni wa wachamngu.
50. Na kwa kina
A'adi tulimtuma ndugu yao Hud. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni
Mwenyezi Mungu! Nyinyi hamna mungu isipo kuwa Yeye. Nyinyi si chochote ila ni
wazushi tu.
|