13. SURAT AR-RAA'D
(Imeteremka
Madina)
"Surat
Ar Raa'd" ni Sura ya Madina, na imeitwa "Raa'd" kwa kusimuliwa
kwamba Radi (inamsabihi) inamtakasa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na hisabu za Aya
zake ni arubaini na tatu. Imeanza Sura hii kwa kubainisha cheo cha , na kwamba
imeteremshwa kwa Wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kisha ikabainisha uwezo wa
Mwenyezi Mungu Mtukufu katika ulimwengu wote, na ikazindua kueleza mambo yaliyo
umbwa na yenye manufaa. Kisha ikatoka kubainisha uwezo wake Mwenyezi Mungu wa
kuumba, ikaingia kubainisha uwezo wake kurejesha tena na kufufua, na ujuzi wa
Mwenyezi Mungu Mtukufu wa kila kitu, na kubainisha kudra yake ya kuadhibu
duniani, na kwa hivyo yaweza kukisiwa adhabu ya Akhera. Kisha Sura hii
ikaelekeza nadhari zizingatie maajabu ya ulimwengu yaliyo zagaa. Baada ya hayo
Mwenyezi Mungu Mtukufu amezieleza hali za watu katika kupokea kwao uwongofu wa
Qur'ani. Kisha akataja sifa za Waumini katika makhusiano yao ya kibinaadamu, na
tabia za makafiri na karaha yao kushikilia kutaka miujiza isiyo kuwa hii
Qur'ani juu ya ubora wake wa cheo, na ikataja kejeli zao kwa Mtume wao. Na
ikamueleza Mtume kuwa Mitume wa kabla yake pia walifanyiwa kejeli! Na kwamba
Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwenye kusimamia vitu vyote na nafsi zote, na kwamba
Yeye ni Mwenye kumlipa kila mtu kwa anavyo stahiki, na kwamba Qur'ani ndio
muujiza mkubwa kabisa utakao baki mpaka Siku ya Kiyama, na kwamba Mwenyezi
Mungu Mtukufu ndiye anaye wapa nguvu Mitume wake kwa miujiza aitakayo. Na ikiwa
hao washirikina wanakanya Utume wa Nabii huyu, basi Mwenyezi Mungu Mwenyewe
anashuhudia ukweli wake, na Yeye ni Mwenye kutosheleza kwa hayo.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Alif
Lam Mym Ra. (A.L.M.R.) Hizi ni Ishara za Kitabu. Na uliyo teremshiwa kutoka kwa
Mola wako Mlezi ni Haki. Lakini wengi wa watu hawaamini.
2.
Mwenyezi Mungu aliye ziinua mbingu bila ya nguzo mnazo ziona, ametawala kwenye
Ufalme wake, na amefanya jua na mwezi yamt'ii, kila kimoja kinakwenda kwa
kiwango maalumu. Anayapanga mambo, na anazipambanua Ishara ili mpate kuwa na
yakini kukutana na Mola wenu Mlezi.
3. Na ndiye aliye itandaza ardhi na akaweka humo milima na
mito. Na katika kila matunda
akafanya dume na jike. Huufunika usiku juu ya mchana. Hakika katika haya zimo
Ishara kwa watu wanao fikiri.
4. Na katika
ardhi vimo vipande vilivyo karibiana, na zipo bustani za mizabibu, na mimea
mingine, na mitende yenye kuchipua kwenye shina moja na isio chipua kwenye
shina moja, nayo inatiliwa maji yale yale. Na tunaifanya baadhi yao bora kuliko
mengine katika kula. Hakika katika hayo zimo ishara kwa watu wanao tia mambo
akilini.
5. Na kama
ukistaajabu, basi cha ajabu zaidi ni huo usemi wao: Ati tukisha kuwa mchanga
kweli tutakuwa katika umbo jipya? Hao ndio walio mkufuru Mola wao Mlezi. Na hao
ndio watao kuwa na makongwa shingoni mwao, na hao ndio watu wa Motoni. Humo watadumu.
6. Na
wanakuhimiza ulete maovu kabla ya mema, hali ya kuwa zimekwisha pita kabla yao
adhabu za kupigiwa mfano. Na hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye msamaha kwa watu
juu ya udhalimu wao. Na hakika Mola wako Mlezi ni Mkali wa kuadhibu.
7. Na wale
walio kufuru husema: Mbona hakuteremshiwa muujiza kutoka kwa Mola wake Mlezi?
Hakika wewe ni Mwonyaji, na kila kaumu ina wa kuwaongoa.
8.
Mwenyezi Mungu anajua mimba abebayo kila mwanamke, na kinacho punguka na kuzidi
matumboni. Na kila kitu kwake ni kwa kipimo.
9. Yeye
ndiye Mwenye kujua yanayo onekana na yasio onekana; Mkuu Aliye tukuka.
10. Ni
sawa anaye ficha kauli yake kati yenu na anaye idhihirisha, na anaye jibanza
usiku na anaye tembea jahara mchana.
11. Kila
mtu analo kundi la malaika mbele yake na nyuma yake linamlinda kwa amri ya
Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili
wao yaliyomo naf- sini mwao. Na Mwenyezi Mungu anapo watakia watu adhabu hakuna
cha kuzuia wala hawana mlinzi yeyote badala yake.
12. Yeye
ndiye anaye kuonyesheni umeme kwa khofu na tamaa, na huyaleta mawingu mazito.
13. Na
radi inamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumhimidi, na Malaika pia, kwa kumkhofu.
Naye hupeleka mapigo ya radi yakampata amtakaye. Nao wanabishana juu ya
Mwenyezi Mungu. Na Yeye ni
Mwenye adhabu kali!
14. Wa kuombwa
kweli ni Yeye tu. Na hao wanao waomba badala yake hawawajibu chochote; bali ni
kama mwenye kunyoosha viganja vyake kwenye maji ili yafike kinywani mwake,
lakini hayafiki. Na maombi ya makafiri hayako ila katika upotovu.
15. Na viliomo
mbinguni na katika ardhi vinamsujudia Mwenyezi Mungu tu vikitaka visitake. Na
pia vivuli vyao asubuhi na jioni.
16. Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu na ardhi? Sema:
Mwenyezi Mungu. Sema: Basi je, mnawafanya wenginewe badala yake kuwa ni walinzi,
nao hawajifai wenyewe kwa jema wala baya? Sema: Hebu kipofu na mwenye kuona
huwa sawa? Au hebu huwa sawa giza na mwangaza? Au wamemfanyia Mwenyezi Mungu
washirika walio umba kama alivyo umba Yeye, na viumbe hivyo vikawadanganyikia?
Sema: Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu. Na Yeye ni Mmoja Mwenye kushinda!
17. Ameteremsha
maji kutoka mbinguni. Na mabonde yakamiminika maji kwa kadiri yake. Na mafuriko
yakachukua mapovu yaliyo kusanyika juu yake. Na kutokana na wanavyo yayusha
katika moto kwa kutaka mapambo au vyombo hutokea povu vile vile. Namna hivyo
Mwenyezi Mungu ndivyo anavyo piga mifano ya Haki na baat'ili. Basi lile
povu linapita kama takataka tu basi. Ama kinacho wafaa watu hubakia kwenye
ardhi. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo piga mifano.
18. Walio muitikia Mola wao Mlezi watapata wema. Na wasio muitikia,
hata wangeli kuwa navyo vyote viliomo katika ardhi na mfano wa hivyo, bila ya
shaka wangeli vitoa kujikombolea! Hao watapata hisabu mbaya kabisa, na makao
yao ni Jahannamu. Na hapo ni pahala pabaya mno!
19. Je! Anaye jua ya kwamba yaliyo teremshwa kwako kutoka
kwa Mola wako Mlezi ni Haki ni sawa na aliye kipofu? Wenye akili ndio wanao
zingatia,
20. Wale ambao wanatimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu, wala
hawavunji maagano.
21. Na wale ambao huyaunga aliyo amrisha Mwenyezi Mungu
yaungwe, na wanaikhofu hisabu mbaya.
22. Na ambao husubiri kwa kutaka radhi ya Mola wao Mlezi,
na wakashika Sala, na wakatoa, kwa siri na kwa uwazi, katika tulivyo wapa; na
wakayaondoa maovu kwa wema. Hao ndio watakao pata malipo ya Nyumba ya Akhera.
23. Nayo ni Bustani za milele, wataziingia wao na walio
wema miongoni mwa baba zao, na wake zao, na vizazi vyao. Na Malaika
wanawaingilia katika kila mlango.
24.(Wakiwaambia) Assalamu Alaikum! Amani iwe juu yenu, kwa
sababu ya mlivyo subiri! Basi ni mema mno malipo ya Nyumba ya Akhera.
25. Na wale wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya
kuzifunga, na wanakata aliyo amrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanafanya
fisadi katika nchi: hao ndio watakao pata laana, na watapata Nyumba mbaya.
26. Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye, na
humkunjia kwa kipimo. Na wamefurahia maisha ya dunia. Na uhai wa dunia kwa
kulingana na Akhera si kitu ila ni starehe ndogo.
27. Na wanasema walio kufuru: Kwa nini hakuteremshiwa
muujiza kutoka kwa Mola wake Mlezi. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu humwacha
kupotea amtakaye, na humwongoa anaye elekea kwake,
28. Wale walio amini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka
Mwenyezi Mungu. Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua!
29. Wale walio amini na wakatenda mema watakuwa na raha na
marejeo mazuri.
30. Ndio kama hivi tumekutuma kwa umma ambao wamekwsiha
pita kabla yao umati nyengine, ili uwasomee tunayo kufunulia, na wao
wanamkufuru Rahmani, Mwingi wa Rehema! Sema: Yeye ndiye Mola wangu Mlezi.
Hapana mungu isipo kuwa Yeye. Juu yake nimetegemea, na kwake ndio marejeo
yangu!
31. Na kama ingeli kuwako Qur'ani ndiyo inayo endeshewa
milima, na kupasuliwa ardhi, na kusemeshewa wafu, (basi ingeli kuwa Qur'ani
hii). Bali mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Je, hawajajua walio amini kwamba
lau kuwa Mwenyezi Mungu ange penda bila ya shaka angeli waongoa watu wote? Wala
walio kufuru hawaachi kusibiwa na balaa kwa waliyo yatenda, au ikawateremkia
karibu na nyumbani kwao, mpaka ifike ahadi ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi
Mungu havunji miadi yake.
32. Na hakika walifanyiwa kejeli Mitume walio kuwa kabla
yako. Na nikawapururia wale walio kufuru, kisha nikawashika! Basi ilikuwaje
adhabu yangu!
33. Je! Anaye isimamia kila nafsi kwa yale iliyo
yachuma...? Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu kuwa na washirika! Sema watajeni. Au
ndio mnampa khabari ya yale asiyo yajua katika ardhi; au ni maneno matupu? Bali
walio kufuru wamepambiwa vitimbi vyao na wamezuiliwa njia. Na ambaye Mwenyezi
Mungu amemwacha apotee basi hana wa kumwongoa.
34. Wanayo adhabu katika maisha ya dunia, na adhabu ya
Akhera hapana shaka ina mashaka zaidi. Na wala hawatakuwa na wa kuwalinda na
Mwenyezi Mungu.
35. Mfano wa Bustani waliyo ahidiwa wachamngu, kati yake
inapita mito, matunda yake ni ya daima, na pia kivuli chake. Huu ndio mwisho wa
wale walio walio jilinda. Na mwisho wa makafiri ni Moto.
36. Na tulio wapa Kitabu wanafurahia uliyo teremshiwa. Na
katika makundi mengine wapo wanao yakataa baadhi ya haya. Sema: Nimeamrishwa
nimuabudu Mwenyezi Mungu, na wala nisimshirikishe. Kuendea kwake Yeye ndiyo
ninaita, na kwake Yeye ndio marejeo yangu.
37. Na ndio kama hivi tumeiteremsha Qur'ani kuwa ni hukumu
kwa lugha ya Kiarabu. Na ukifuata matamanio yao baada ya kukujia ilimu hii,
hutakuwa na rafiki wala mlinzi mbele ya Mwenyezi Mungu.
38. Na hakika Sisi tulikwisha watuma Mitume kabla yako, na
tukajaalia wawe na wake na dhuriya. Na haiwi kwa Mtume kuleta miujiza isipo
kuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kila kipindi kina hukumu yake. 39.
Mwenyezi Mungu hufuta na huthibitisha ayatakayo. Na asili ya hukumu zote iko
kwake.
40. Na ikiwa tukikuonyesha baadhi ya tuliyo waahidi au
tukakufisha kabla yake, juu yako wewe ni kufikisha ujumbe na juu yetu ni
hisabu.
41. Je! Hawakuona kwamba tunaifikia ardhi tukiipunguza
nchani mwake? Na Mwenyezi Mungu huhukumu, na hapana wa kupinga hukumu yake,
naye ni Mwepesi wa kuhisabu.
42. Na walipanga walio kuwa kabla yao, lakini Mwenyezi
Mungu ndiye Mwenye mipango yote. Yeye anajua inayo chuma kila nafsi. Na
makafiri watajua ni ya nani nyumba ya mwisho Akhera!
43. Na walio kufuru wanasema: Wewe hukutumwa. Sema:
Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi, na pia yule mwenye
ilimu ya Kitabu.
|