14. SURAT IBRAHIM
(Imeteremka
Makka)
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Alif
Lam Ra. (A.L.R.) Hichi ni Kitabu tulicho kiteremsha kwako ili uwatowe watu
kwenye giza uwapeleke kwenye muwangaza, kwa idhini ya Mola wao Mlezi,
uwafikishe kwenye Njia ya Mwenye nguvu, Msifiwa,
2. Naye ni
Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake Yeye vyote viliomo katika mbingu na ardhi. Na
ole wao makafiri kwa adhabu kali!
3. Wale
wanao fadhilisha maisha ya dunia kuliko Akhera, na wanawazuilia watu wasifuate
Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanataka kuipotosha. Hao wamepotelea mbali.
4. Na hatukumtuma Mtume ila kwa ulimi wa kaumu yake ili
apate kuwabainishia. Basi Mwenyezi Mungu humuacha akapotea amtakaye, na akamwongoa
amtakaye. Naye ni Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
5. Na tulimtuma Musa pamoja na miujiza yetu, tukamwambia:
Watoe watu wako kwenye giza uwapeleke kwenye mwangaza. Na uwakumbushe siku za
Mwenyezi Mungu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa kila mwenye kusubiri
akashukuru.
6. Na Musa alipo waambia watu wake: Kumbukeni neema ya
Mwenyezi Mungu aliyo kujaalieni, pale alipo kuokoeni kutokana na watu wa
Firauni walio kupeni adhabu mbaya kabisa, wakiwachinja wenenu wanaume, na
wakiwawacha hai wanawake. Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa unao toka kwa
Mola wenu Mlezi.
7. Na alipo tangaza Mola wenu Mlezi: Mkishukuru
nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.
8. Na Musa alisema: Mkikufuru nyinyi na wote waliomo
duniani, hakika Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Anajitosha, Msifiwa.
9. Je! Hazikukufikieni khabari za walio kabla yenu? Kaumu
ya Nuhu, na A'adi, na Thamud, na walio baada yao, ambao hapana awajuaye ila
Mwenyezi Mungu? Mitume wao waliwajia kwa hoja zilizo wazi, na wao wakarudisha
mikono yao kwenye vinywa vyao, wakasema: Hakika sisi tumeyakataa hayo mliyo
tumwa, na hakika sisi tuna shaka kubwa na mnayo tuitia.
10. Mitume wao wakasema: Ati pana shaka na Mwenyezi Mungu,
Muumba mbingu na ardhi? Yeye anakuiteni apate kukufutieni madhambi yenu, na
akupeni muhula mpaka muda ulio wekwa. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni
wanaadamu kama sisi. Mnataka kutuzuilia na waliyo kuwa wakiabudu baba zetu.
Basi tuleteeni hoja ilio wazi.
11. Mitume wao wakawaambia: Sisi kweli si chochote ila ni
wanaadamu kama nyinyi. Lakini Mwenyezi Mungu humfanyia hisani amtakaye katika
waja wake. Wala sisi hatuwezi kuleta uthibitisho ila kwa idhini ya Mwenyezi
Mungu. Na juu ya Mwenyezi Mungu ndio wategemee Waumini.
12. Na tuna nini hata tusimtegemee Mwenyezi Mungu, na hali
Yeye ametuongoa kwenye Njia zetu. Na hapana shaka sisi tutayavumilia hayo
maudhi mnayo tuudhi. Na juu ya Mwenyezi Mungu wategemee wanao tegemea.
13. Na walio kufuru wakawaambia Mitume wao: Tutakutoeni
katika nchi yetu, au mrudi katika mila yetu. Basi Mola wao Mlezi aliwaletea
wahyi: Hakika tutawaangamiza walio dhulumu!
14. Na tutakuwekeni katika ardhi baada yao. Haya ni kwa
anaye ogopa kusimamishwa mbele yangu, na akaogopa maonyo yangu.
15. Na wakaomba ushindi, na akashindwa kila jabari mkaidi,
16. Ambaye nyuma yake ipo Jahannamu, na atanywishwa maji ya
usaha.
17. Awe anayagugumia, wala hawezi kuyameza. Na mauti yawe
yanamjia kutoka kila upande, naye wala hafi. Na zaidi ya hayo ipo adhabu
nyengine kali vile vile.
18. Mfano wa walio mkufuru Mola wao Mlezi - vitendo vyao ni
kama jivu linalo peperushwa kwa nguvu za upepo katika siku ya mdharba. Hawawezi
kupata chochote katika waliyo yafanya. Huko ndiko kupotelea mbali!
19. Huoni kuwa Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa
Haki? Akitaka atakuondoeni na alete viumbe wapya!
20. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu si jambo gumu.
21. Na wote watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu. Wanyonge watawaambia
walio takabari: Sisi tulikuwa wafwasi wenu; basi hebu hamtuondolei kidogo hivi
katika adhabu ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Lau Mwenyezi Mungu angeli tuongoa
basi hapana shaka nasi tungeli kuongoeni. Ni mamoja kwetu tukipapatika au
tukisubiri; hatuna pa kukimbilia.
22. Na Shet'ani atasema itapo katwa hukumu: Hakika Mwenyezi
Mungu alikuahidini ahadi ya kweli. Nami nalikuahidini; lakini sikukutimizieni.
Na sikuwa na mamlaka juu yenu, isipo kuwa nilikuiteni, nanyi mkaniitikia. Basi
msinilaumu mimi, bali jilaumuni wenyewe. Mimi siwezi kuwa mtetezi wenu, wala
nyinyi hamwezi kuwa watetezi wangu. Hakika mimi nilikataa tangu zamani
kunishirikisha na Mwenyezi Mungu. Hakika madhaalimu watakuwa na adhabu chungu.
23. Na walio amini na wakatenda mema wataingizwa katika
Mabustani yapitayo mito kati yake, wadumu humo kwa idhini ya Mola wao Mlezi.
Maamkio yao humo yatakuwa: Salaam!
24. Hebu hukuona vipi Mwenyezi Mungu alivyo piga mfano wa
neno zuri? Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako
mbinguni.
25. Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake Mlezi.
Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka.
26. Na mfano wa neno ovu ni kama mti muovu, ulio ng'olewa
juu ya ardhi. Hauna imara.
27. Mwenyezi Mungu huwatia imara wenye kuamini kwa kauli ya
imara katika maisha ya dunia na katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwaacha
kupotea hao wenye kudhulumu. Na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo.
28. Hebu hukuwaona wale walio badilisha neema ya Mwenyezi
Mungu kwa kufuru, na wakawafikisha watu wao kwenye nyumba ya maangamizo?
29. Nayo ni Jahannamu! Maovu yaliyoje makaazi hayo!
30. Na walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili wapoteze
watu kwenye Njia yake. Sema: Stareheni! Kwani marejeo yenu ni Motoni!
31. Waambie waja wangu walio amini, washike Sala, na watoe
katika tulivyo waruzuku, kwa siri na dhaahiri, kabla haijafika Siku isiyo kuwa
na biashara wala urafiki.
32. Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi, na
akateremsha maji kutoka mbinguni. Na kwa hayo akatoa matunda kuwa ni riziki
yenu. Na akafanya yakutumikieni majahazi yanayo pita baharini kwa amri yake, na
akaifanya mito ikutumikieni.
33. Na akalifanya jua na mwezi kwa manufaa yenu daima
dawamu, na akaufanya usiku na mchana kwa manufaa yenu.
34. Na akakupeni kila mlicho muomba. Na mkihisabu neema za
Mwenyezi Mungu hamwezi kuzidhibiti. Hakika mwanaadamu ni dhaalimu mkubwa,
mwenye kuzikufuru neema.
35. Na Ibrahim alipo sema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ujaalie
mji huu uwe wa amani, na uniepushe mimi na wanangu na kuabudu masanamu.
36. Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hayo yamewapoteza watu
wengi. Basi aliye nifuata mimi huyo ni wangu, na aliye niasi, hakika Wewe ni
Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
37. Mola wetu Mlezi! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya
dhuriya zangu katika bonde lisilo kuwa na mimea, kwenye Nyumba yako Takatifu,
ewe Mola wetu Mlezi, ili washike Sala. Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee
kwao, na waruzuku matunda, ili wapata kushukuru.
38. Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe unajua tunayo yaficha
na tunayo yatangaza. Na hapana kitu kinacho fichikana kwa Mwenyezi Mungu katika
ardhi wala katika mbingu.
39. Alhamdulillahi! Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu aliye
nipa juu ya uzee wangu Ismail na Is-haq. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye
kusikia maombi.
40. Mola wangu Mlezi! Nijaalie niwe mwenye kushika Sala, na
katika dhuriya zangu pia. Ewe Mola wetu Mlezi, na ipokee dua yangu.
41. Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote
wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu.
42. Wala usidhani Mwenyezi Mungu ameghafilika na wanayo
yafanya madhaalimu. Hakika Yeye anawaakhirisha tu mpaka siku yatapo kodoka
macho yao.
43. Nao wako mbioni, vichwa juu, na macho hayapepesi, na
nyoyo zao tupu.
44. Na waonye watu siku itapo wajia adhabu, na walio dhulumu
waseme: Ewe Mola wetu Mlezi! Tuakhirishe muda kidogo tuitikie wito wako na
tuwafuate Mitume. Kwani nyinyi si mliapa zamani kwamba hamtaondokewa?
45. Na mkakaa katika maskani zile zile za walio zidhulumu
nafsi zao. Na ikakudhihirikieni jinsi tulivyo watendea. Nasi tukakupigieni
mifano mingi.
46. Na kwa hakika walifanya vitimbi vyao, na vitimbi vyao
anavijua Mwenyezi Mungu. Wala vitimbi vyao si vya kuondosha milima.
47. Basi usimdhanie Mwenyezi Mungu kuwa ni mwenye
kuwavunjia ahadi yake Mitume wake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushinda, na
ni Mwenye kulipiza.
48. Siku itapo geuzwa ardhi iwe ardhi nyengine, na mbingu
pia. Nao watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu Mmoja, Mwenye nguvu.
49. Na utaona wakhalifu siku hiyo wamefungwa katika
minyororo;
50 Nguo zao zitakuwa za lami, na Moto utazigubika nyuso
zao.
51. Ili Mwenyezi Mungu ailipe kila nafsi kwa yale iliyo
yachuma. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
52. Hili ni Tangazo liwafikie watu, liwaonye, na wapate
kujua kuwa hakika Yeye ni Mungu Mmoja, na wapate kukumbuka wenye akili.
|