1 - 50
1. Amri ya Mwenyezi Mungu itafika tu. Basi msiihimize.
Ametakasika na Ametukuka na wanayo mshirikisha nayo.
2. Huwateremsha Malaika na Roho kwa amri yake juu ya
amtakaye katika waja wake ili nyinyi muonye kwamba hapana mungu ila Mimi, basi
nicheni Mimi.
3. Ameziumba mbingu na ardhi kwa Haki. Ametukuka na wanayo shirikisha.
4. Amemuumba mtu kwa tone la manii. Naye mara amekuwa
mshindani dhaahiri.
5. Na nyama hoa amekuumbieni. Katika hao mna vifaa vya
kutia joto, na manufaa mengineyo, na baadhi yao mnawala.
6. Na wanakupeni furaha pale mnapo warudisha jioni na mnapo
wapeleka malishoni asubuhi.
7. Na hubeba mizigo yenu kupeleka kwenye miji msiyo weza
kuifikia ila kwa mashaka ya nafsi. Hakika Mola wenu Mlezi ni Mpole na Mwenye
kurehemu.
8. Na farasi, na nyumbu, na punda ili muwapande, na kuwa ni
pambo. Na ataumba msivyo vijua.
9. Na ni juu ya Mwenyezi Mungu kuelekeza Njia. Na zipo njia
za upotovu. Na angeli penda angeli kuongoeni nyote.
10. Yeye ndiye anaye kuteremshieni maji kutoka mbinguni.
Katika hayo nyinyi mnapata ya kunywa, na miti ya kulishia.
11. Kwa hayo Yeye anaizalisha kwa ajili yenu mimea, na
mizaituni, na mitende, na mizabibu, na kila namna ya matunda. Hakika katika
haya zipo ishara kwa watu wanao fikiri.
12. Na amefanya ukutumikieni usiku na mchana, na jua na
mwezi, na nyota zikutumikieni kwa amri yake. Hakika katika hayo zipo ishara kwa
watu wenye akili.
13. Na hivi alivyo vieneza katika ardhi vya rangi mbali
mbali. Hakika katika hayo ipo ishara kwa watu wanao waidhika.
14. Yeye ndiye aliye ifanya bahari ikutumikieni, ili
kutokana na humo mpate kula nyama laini, na mtoe humo mapambo mnayo yavaa. Na
unaona marikebu zikikata maji humo, ili mtafute fadhila yake, na mpate
kushukuru.
15. Na kaweka katika ardhi milima ili ardhi isiyumbe yumbe
nanyi. Na mito, na njia ili mpate kuongoka.
16. Na alama nyengine. Na kwa nyota wao wanajiongoza.
17. Ati anaye umba ni kama asiye umba? Basi hebu,
hamkumbuki?
18. Na mkizihisabu neema za Mwenyezi Mungu, hamwezi
kuzidhibiti. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira, Mwenye kurehemu.
19. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yaficha na mnayo
yatangaza.
20. Na wale wanao waomba wasio kuwa Mwenyezi Mungu hawaumbi
kitu, bali wao wameumbwa.
21. Ni wafu si wahai, na wala hawajui watafufuliwa lini.
22. Mungu wenu ni Mungu Mmoja. Lakini wasio iamini Akhera
nyoyo zao zinakataa, nao wanajivuna.
23. Hapana shaka kuwa hakika Mwenyezi Mungu anayajua wanayo
yaficha na wanayo yatangaza. Kwa hakika Yeye hawapendi wanao jivuna.
24. Na wanapo ambiwa: Kateremsha nini Mola wenu Mlezi?
Husema: Hadithi za kubuni za watu wa kale!
25. Ili wabebe mizigo yao kwa ukamilifu Siku ya Kiyama, na
sehemu ya mizigo ya wale wanao wapoteza bila ya kujua. Angalia, ni maovu mno
hayo wanayo yabeba!
26. Walipanga vitimbi walio kuwa kabla yao, Mwenyezi Mungu
akayasukua majengo yao kwenye misingi, dari zikawaporomokea juu yao, na adhabu
ikawajia kutoka wasipo kujua.
27. Kisha Siku ya Kiyama atawahizi na atasema: Wako wapi
hao washirika wangu ambao kwao mkiwakutisha (Manabii) mashaka? Watasema walio
pewa ilimu: Hakika leo ndiyo hizaya na adhabu itawashukia makafiri,
28. Ambao Malaika waliwafisha nao wamejidhulumu nafsi zao! Basi
watasalimu amri, waseme: Hatukuwa tukifanya uovu wowote. (Wataambiwa): Kwani!
Hakika Mwenyezi Mungu anajua sana mliyo kuwa mkiyatenda.
29. Basi ingieni milango ya Jahannamu, humo mdumu. Ni maovu
mno makaazi ya wafanyao kiburi!
30. Na wataambiwa walio mcha Mungu: Mola wenu Mlezi
kateremsha nini? Watasema: Kheri. Walio fanya wema katika dunia hii watapata
wema. Na nyumba ya Akhera ni bora zaidi, na njema mno nyumba ya wachamngu.
31. Bustani za milele wataziingia; iwe inapita kati yake
mito. Humo watapata watakacho.
Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu awalipavyo wenye kumcha.
32. Wale
ambao Malaika huwafisha katika hali njema, wanawaambia: Amani iwe juu yenu!
Ingieni Peponi kwa sababu ya yale mliyo kuwa mkiyatenda.
33.
Wanangojea jengine hawa ila Malaika wawafikie, au iwafikie amri ya Mola wako
Mlezi? Kama hivyo walitenda walio kuwa kabla yao. Na Mwenyezi Mungu
hakuwadhulumu, lakini walijidhulumu wenyewe.
34. Basi
ukawafikia uovu wa waliyo yatenda, na waliyo kuwa wakiyakejeli yakawazunguka.
35. Na
washirikina wanasema: Mwenyezi Mungu angeli taka tusingeli abudu chochote
badala yake, sisi wala baba zetu, wala tusingeli harimisha chochote bila ya
Yeye. Kama hivyo walifanya walio kuwa kabla yao. Basi lipo lolote juu ya Mitume
isipo kuwa kubalighisha kwa uwazi?
36. Na kwa
hakika kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na
muepukeni Shetani. Basi kati yao wapo alio waongoa Mwenyezi Mungu. Na kati yao
wapo ambao ulio wathibitikia upotovu. Basi tembeeni katika ardhi, muangalie
ulikuwaje mwisho wa wanao kanusha.
37. Hata
ukiwa na pupa ya kutaka kuwaongoa, lakini Mwenyezi Mungu hamwongoi yule anaye
shikilia kupotea. Wala hawatapata wa kuwanusuru.
38. Na
wanaapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa viapo vyao kwamba Mwenyezi Mungu hatomfufua
aliye kufa. Kwani! Ni ahadi iliyo juu yake kikweli; lakini watu wengi hawajui.
39. Ili
kuwabainishia yale waliyo khitalifiana, na ili wajue walio kufuru kwamba wao
walikuwa ni waongo.
40. Kauli
yetu kwa kitu tunacho kitaka kiwe, ni kukiambia: Kuwa! Basi kinakuwa.
41. Na wale
walio hama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu baada ya kudhulumiwa, bila ya shaka
tutawaweka duniani kwa wema; na ujira wa Akhera ni mkubwa zaidi; laiti kuwa
wanajua!
42. Wale
wanao subiri na wakamtegemea Mola wao Mlezi.
43. Nasi
hatukuwatuma kabla yako ila watu wanaume tulio wapa Wahyi (Ufunuo). Basi
waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui
44. Kwa
Ishara wazi na Vitabu. Nasi tumekuteremshia wewe Ukumbusho ili uwabainishie
watu yaliyo teremshwa kwao, wapate kufikiri.
45. Je!
Wameaminisha wanao fanya vitimbi vya uovu kwamba Mwenyezi Mungu hatawadidimiza
katika ardhi, na haitawafika adhabu kutoka wasipo pajua?
46. Au
hatawashika katika nyendo zao, na wala hawataponyoka?
47. Au
hatawashika kwa kitisho na kuwapunguza kidogo kidogo? Hakika Mola wenu Mlezi ni
Mwenye huruma, Mwenye kurehemu.
48. Je!
Hawavioni vitu alivyo viumba Mwenyezi Mungu - vivuli vyao vinaelekea kushotoni
na kuliani, kumsujudia Mwenyezi Mungu na vikinyenyekea?
49. Na
vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi, tangu wanyama mpaka Malaika,
vinamsujuidia Mwenyezi Mungu, na wala havitakabari.
50.
Vinamkhofu Mola wao Mlezi aliye juu yao, na vinafanya vinavyo amrishwa.
|