51 - 100
51. Na
Mwenyezi Mungu amesema: Msiwe na miungu wawili! Hakika Yeye ni Mungu Mmoja. Basi
niogopeni Mimi tu!
52. Na ni vyake Yeye viliomo katika mbingu na ardhi. Na
Dini ni yake Yeye daima. Je! Mtamcha mwengine asiye kuwa Mwenyezi Mungu?
53. Na neema yoyote mliyo nayo inatoka kwa Mwenyezi Mungu.
Kisha yakikuguseni madhara mnamyayatikia Yeye.
54. Na anapo kuondosheeni madhara mara kundi moja miongoni
mwenu linamshirikisha Mola wao Mlezi,
55. Wakizikataa neema tulizo wapa. Basi stareheni. Mtakuja
jua!
56. Na hao ambao hata hawawajui wanawawekea sehemu ya
tunavyo waruzuku. Wallahi! Bila ya shaka mtasailiwa kwa hayo mliyo kuwa
mnayazua!
57. Na wanamfanyia Mwenyezi Mungu ati ana mabinti,
Subhanahu, Aliye takasika! Na wao wenyewe, ati ndio wawe na hayo wanayo
yatamani!
58. Na mmoja wao akibashiriwa kwa msichana, uso wake
unasawijika, naye kajaa chuki.
59. Anajificha asionekane na watu kwa ubaya wa aliyo
bashiriwa! Je, akae naye juu ya fedheha hiyo au amfukie udongoni? Tazama uovu
wa wanavyo hukumu!
60. Hali ya wasio iamini Akhera ni ovu; na Mwenyezi Mungu
ndiye Mwenye sifa tukufu. Naye ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
61. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wachukulia watu kwa
mujibu wa dhulma zao, basi asingeli mwacha hapa hata mnyama mmoja. Lakini
anawaakhirisha mpaka muda ulio wekwa. Na unapo fika muda wao hawatakawilia hata
saa moja wala hawatatangulia.
62. Na wanampa Mwenyezi Mungu wanavyo vichukia wao, na
ndimi zao zinasema uwongo kwamba wao watapata mema. Hapana shaka hakika
wamewekewa Moto, nao wataachwa humo.
63.
Wallahi! Sisi tulituma Mitume kwa umati zilizo kuwa kabla yako, lakini Shetani
aliwapambia vitendo vyao. Kwa hivyo leo yeye ndiye rafiki yao; nao watapata
adhabu chungu.
64. Na
hatukukuteremshia Kitabu isipo kuwa uwabainishie yale ambayo wanakhitalifiana,
na kiwe Uwongofu na Rehema kwa watu wanao amini.
65. Na
Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni na kwa hayo akaihuisha ardhi
baada ya kufa kwake. Kwa hakika katika hayo imo Ishara kwa watu wanao sikia.
66. Na
hakika katika nyama hoa nyinyi mna mazingatio. Tunakunywesheni katika vile
viliomo matumboni mwao, vikatoka baina ya mavi na damu, maziwa safi mazuri kwa
wanywao.
67. Na
kutokana na matunda ya mitende na mizabibu mnatengeneza ulevi na riziki nzuri.
Hakika katika hayo ipo Ishara kwa wanao tumia akili.
68. Na
Mola wako Mlezi amemfunulia nyuki: Jitengenezee majumba yako katika milima,na
katika miti, na katika wanayo jenga watu.
69. Kisha
kula katika kila matunda, na upite katika njia za Mola wako Mlezi zilizo fanywa
nyepesi kuzipita. Na kutoka matumbo yao kinatoka kinywaji chenye rangi mbali
mbali; ndani yake kina matibabu kwa wanaadamu. Hakika katika haya ipo Ishara
kwa watu wanao fikiri.
70. Na
Mwenyezi Mungu amekuumbeni; kisha anakufisheni. Na miongoni mwenu wapo wanao rudishwa
kwenye umri mbaya kabisa, hata akawa asijue kitu baada ya ujuzi alio kuwa nao.
Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi na Mweza.
71. Na
Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika riziki. Na
wale walio fadhilishwa hawarudishi riziki zao kwa wale ilio wamiliki mikono yao
ya kulia ili wawe sawa katika riziki hiyo. Basi je, wanazikataa neema za
Mwenyezi Mungu?
72. Na
Mwenyezi Mungu amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na akakujaalieni kutoka kwa
wake zenu wana na wajukuu, na akakuruzukuni vitu vizuri vizuri. Basi je, wanaamini
upotovu na wanazikataa neema za Mwenyezi Mungu?
73. Na
badala ya Mwenyezi Mungu wanawaabudu wasio wamilikia riziki kutoka mbinguni
wala kwenye ardhi, wala hawawezi kitu.
74. Basi
msimpigie Mwenyezi Mungu mifano. Hakika Mwenyezi Mungu anajua, na nyinyi
hamjui.
75.
Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa mtumwa aliye milikiwa, asiye weza kitu, na
mwingine tuliye mruzuku riziki njema inayo toka kwetu, naye akawa anatoa katika
riziki hiyo kwa siri na dhaahiri. Je, hao watakuwa sawa? Alhamdu Lillahi!
Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui.
76. Na
Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa watu wawili. Mmoja wao ni bubu, hawezi
chochote, naye ni mzigo kwa bwana wake. Popote anapo muelekeza haleti
kheri. Je! Huyo anaweza kuwa sawa na yule anaye amrisha uadilifu, naye yuko juu
ya Njia Iliyo Nyooka?
77. Na siri zote za katika mbingu na ardhi ziko kwa
Mwenyezi Mungu. Wala halikuwa jambo la Saa (ya Kiyama) ila kama kupepesa kwa
jicho, au akali ya hivyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
78. Na Mwenyezi Mungu amekutoeni matumboni mwa mama zenu,
hali ya kuwa hamjui kitu, na amekujaalieni masikio na macho na nyoyo ili mpate
kushukuru.
79. Je! Hawawaoni ndege walivyo wat'iifu katika anga la
mbingu? Hapana mwenye kuwashika isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Hakika katika haya
zipo ishara kwa watu wanao amini.
80. Na Mwenyezi Mungu amekujaalieni majumba yenu yawe ni
maskani yenu, na amekujaalieni kutokana na ngozi za wanyama nyumba mnazo ziona
nyepesi wakati wa safari zenu na wakati wa kutua kwenu. Na kutokana na sufi zao
na manyoya yao na nywele zao mnafanya matandiko na mapambo ya kutumia kwa muda.
81. Na Mwenyezi Mungu amekufanyieni vivuli katika vitu
alivyo viumba, na amekufanyieni maskani milimani, na amekufanyieni nguo za
kukingeni na joto, na nguo za kukingeni katika vita vyenu. Ndio hivyo
anakutimizieni neema zake ili mpate kut'ii.
82. Basi wakikengeuka lilio juu yako wewe ni kufikisha
ujumbe wazi wazi.
83. Wanazijua neema za Mwenyezi Mungu, kisha wanazikanusha;
na wengi wao ni makafiri.
84. Na siku tutakapo wainua kutokana na kila umma shahidi, kisha
hawataruhusiwa walio kufuru wala hawataachiliwa kutaka radhi.
85. Na walio dhulumu watakapo iona adhabu hawatapunguziwa
hiyo adhabu, wala hawatapewa muhula.
86. Na walio shirikisha watakapo waona hao walio
washirikisha na Mwenyezi Mungu, watasema: Mola wetu Mlezi! Hawa ndio
washirikishwa wetu ambao tulikuwa tukiwaabudu badala yako. Ndipo wale watakapo
watupia kauli: Hakika nyinyi ni waongo!
87. Na siku hiyo watasalimu amri mbele ya Mwenyezi Mungu,
na yatapotea waliyo kuwa wakiyazua.
88. Wale walio kufuru na kuzuilia Njia ya Mwenyezi Mungu
tutawazidishia adhabu juu ya adhabu, kwa walivyo kuwa wakifisidi.
89. Na (waonye) siku tutakapo wainua mashahidi katika kila
umma wakiwashuhudia kwa yanayo tokana na wao, na tutakuleta wewe uwe shahidi
juu ya hao. Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinacho bainisha kila kitu, na ni
uwongofu, na rehema, na bishara kwa Waislamu.
90. Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na
hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini
ili mpate kukumbuka.
91. Na timizeni ahadi ya Mwenyezi Mungu mnapo ahidi, wala
msivunje viapo baada ya kuvithibitisha, ilihali mmekwisha mfanya Mwenyezi Mungu
ndiye mdhamini wenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua myatendayo.
92. Wala msiwe kama mwanamke anaye uzongoa uzi wake baada
ya kwisha usokota ukawa mgumu. Mnavifanya viapo vyenu kuwa ni njia ya
kudanganyana baina yenu kwa kuwa ati taifa moja lina nguvu zaidi kuliko
jengine? Hakika Mwenyezi Mungu anakujaribuni kwa njia hiyo. Na bila ya shaka
atakubainishieni Siku ya Kiyama mliyo kuwa mkikhitalifiana.
93. Na Mwenyezi Mungu angeli taka, kwa yakini angeli kufanyeni
umma mmoja. Lakini anamwachia kupotea anaye mtaka, na anamwongoa amtakaye. Na
hakika mtaulizwa kwa yale mliyo kuwa mkiyafanya.
94. Wala msifanye viapo vyenu ni njia ya kudanganyana baina
yenu. Usije mguu ukateleza badala ya kuthibiti, na mkaonja maovu kwa sababu ya
kule kuzuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, na mkapata adhabu kubwa.
95. Wala msinunue ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa thamani
ndogo. Hakika kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ndicho bora kwenu, ikiwa mnajua.
96. Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu
ndivyo vitakavyo bakia. Na kwa yakini Sisi tutawapa walio subiri ujira wao kwa
bora ya waliyo kuwa wakiyatenda.
97. Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa
ni Muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo
kuwa wakiyatenda.
98. Na ukisoma Qur'ani mwombe Mwenyezi Mungu akulinde na
Shetani maluuni.
99. Hakika yeye hana madaraka juu ya walio amini na
wakamtegemea Mola wao Mlezi.
100. Hakika madaraka yake ni juu ya wanao mfanya rafiki
yao, na wale wanao fanya ushirika naye.
|