101 - 128
101. Na tunapo badilisha Ishara pahala pa Ishara nyengine,
na Mwenyezi Mungu anajua anayo teremsha, wao husema: Wewe ni mzushi. Bali wengi wao hawajui kitu.
102. Sema:
Ameiteremsha hii Roho takatifu kutokana na Mola wako Mlezi kwa haki, ili
awathibitishe wale walio amini, na kuwa ni uwongofu, na ni bishara kwa
Waislamu.
103. Na
Sisi hakika tunajua kwamba wanasema: Yuko mtu anaye mfundisha. Lugha ya huyo
wanaye muelekezea ni ya kigeni, na hii ni lugha ya Kiarabu mbayana.
104.
Hakika wasio ziamini Ishara za Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu hawaongoi, nao
watapata adhabu chungu.
105. Wanao
zua uwongo ni wale tu wasio ziamini Ishara za Mwenyezi Mungu. Na hao
ndio waongo.
106. Anaye mkataa Mwenyezi Mungu baada ya kuamini kwake -
isipo kuwa aliye lazimishwa na hali ya kuwa moyo wake umetua juu ya Imani,
lakini aliye kifungulia kifua chake kukataa - basi hao ghadhabu ya Mwenyezi
Mungu ipo juu yao, na wao watapata adhabu kubwa.
107. Hayo ni kwa sababu wameyapenda zaidi maisha ya duniani
kuliko ya Akhera, na kwa sababu Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
108. Hao ndio Mwenyezi Mungu ameziziba nyoyo zao na masikio
yao na macho yao. Na hao ndio walio ghafilika.
109. Hapana shaka ya kwamba hao ndio wenye kukhasiri
Akhera.
110. Kisha hakika Mola wako Mlezi, kwa wale walio hama
makwao baada ya kuteswa, kisha wakapigania Dini na wakasubiri, bila ya shaka
Mola wako Mlezi baada ya hayo ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
111. Siku ambayo kila nafsi itakuja jitetea, na kila nafsi italipwa
sawa sawa na a'mali ilizo zifanya, nao hawatadhulumiwa.
112. Na Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mji ulio kuwa na
amani na utulivu, riziki yake ikiufikia kwa nafasi kutoka kila mahali. Lakini
ukazikufuru neema za Mwenyezi Mungu; kwa hivyo Mwenyezi Mungu akauvika vazi la
njaa na khofu kwa sababu ya yale waliyo kuwa wakiyafanya.
113. Na alikwisha wajia Mjumbe wa miongoni mwao wenyewe.
Lakini wakamkanusha; basi iliwafika adhabu hali ya kuwa wamedhulumu.
114. Basi kuleni katika vile alivyo kupeni Mwenyezi Mungu,
vilivyo halali na vizuri. Na shukuruni neema za Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli
mnamuabudu Yeye.
115. Amekuharimishieni nyamafu tu, na damu, na nyama ya
nguruwe, na mnyama aliye chinjwa kwa ajili isiyo kuwa ya Mwenyezi Mungu. Lakini
anaye lazimishwa bila ya kuasi, wala kuruka mipaka, basi hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
116. Wala msiseme uwongo, kwa kuropokwa na ndimi zenu:
Hichi halali, na hichi haramu - mkimzulia uwongo Mwenyezi Mungu. Hakika wanao
mzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawatafanikiwa.
117. Ni starehe ndogo, nao watapata adhabu chungu.
118. Na Mayahudi tuliwaharimishia yale tuliyo kuhadithia
zamani. Na Sisi hatukuwadhulumu, bali walikuwa wakijudhulumu wenyewe.
119. Kisha hakika Mola wako Mlezi kwa walio tenda uovu kwa
ujinga, kisha wakatubia baada ya hayo na wakatenda mema; bila ya shaka Mola
wako Mlezi baada ya hayo ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
120. Hakika Ibrahim alikuwa mfano mwema, mnyenyekevu kwa
Mwenyezi Mungu, mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
121. Mwenye kuzishukuru neema zake, Mwenyezi Mungu. Yeye
kamteuwa, na akamwongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka.
122. Na tukampa wema duniani, na hakika Akhera atakuwa
miongoni mwa watu wema.
123. Kisha tukakufunulia ya kwamba ufuate mila ya Ibrahim,
mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
124. Hakika siku ya Sabato (Jumaamosi) waliwekewa wale
walio khitalifiana kwa ajili yake. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka
atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyo kuwa wakikhitalifiana.
125. Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa
hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola
wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye
wajua zaidi walio ongoka.
126. Na mkilipiza basi lipizeni sawa na vile mlivyo
adhibiwa. Na ikiwa mtasubiri, basi hakika hivyo ni bora zaidi kwa wanao subiri.
127. Na subiri. Na kusubiri kwako kusiwe ila kwa sababu ya
Mwenyezi Mungu tu. Wala usiwahuzunikie; wala usiwe katika dhiki kwa hila wanazo
zifanya.
128. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kumcha, na
watendao mema.
|