101 - 111
101. Na kwa yakini tulimpa Musa ishara tisa zilizo wazi.
Waulize Wana wa Israili alipo wafikia, na Firauni akawaambia: Hakika mimi
nakuona wewe Musa umerogwa!
102. Musa akasema: Wewe unajua bila ya shaka kuwa haya
hakuyateremsha ila Mola Mlezi wa mbingu na ardhi ili kuwa ni ushahidi wa
kuonekana. Na hakika mimi bila ya shaka nakuona wewe, Firauni, kuwa umekwisha
angamia.
103. Basi Firauni akataka kuwafukuza katika nchi. Kwa hivyo
tukamzamisha yeye na walio kuwa pamoja naye wote.
104. Na tukawaambia baada yake Wana wa Israili: Kaeni
katika nchi. Itapo kuja ahadi ya Akhera tutakuleteni nyote pamoja.
105. Na kwa Haki tumeiteremsha, na kwa Haki imeteremka. Na
hatukukutuma ila uwe mbashiri na mwonyaji.
106. Na Qur'ani tumeigawanya sehemu mbali mbali ili
uwasomee watu kwa kituo, na tumeiteremsha kidogo kidogo.
107. Sema: Iaminini au msiiamini. Hakika wale walio pewa
ilimu kabla yake, wanapo somewa hii, huanguka kifudifudi wanasujudu.
108. Na wanasema: Subhana Rabbina, Ametakasika Mola wetu
Mlezi! Hakika ahadi ya Mola wetu Mlezi lazima itimizwe!
109. Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na
inawazidisha unyenyekevu.
110. Sema: Mwombeni Allah (Mwenyezi Mungu), au mwombeni
Rahman (Mwingi wa Rehema), kwa jina lolote mnalo mwita. Kwani Yeye ana majina
mazuri mazuri. Wala usitangaze Sala yako kwa sauti kubwa, wala usiifiche kwa
sauti ndogo, bali shika njia ya kati na kati ya hizo.
111. Na sema: Alhamdulillah, Himdi zote ni za Mwenyezi
Mungu ambaye hana mwana, wala hana mshirika katika ufalme, wala hana rafiki wa
kumsaidia kwa sababu ya udhaifu wake. Na mtukuze kwa utukufu mkubwa.
|