1 - 50
1. Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye amemteremshia
mja wake Kitabu, wala hakukifanya kina upogo.
2. Kimenyooka sawa, ili kitoe onyo kali kutoka kwake, na
kiwabashirie Waumini watendao mema kwamba watapata ujira mzuri.
3. Wakae humo milele.
4. Na kiwaonye wanao nena: Mwenyezi Mungu ana mwana.
5. Wao hawana ujuzi wa jambo hili, wala baba zao. Ni neno
kuu hilo litokalo vinywani mwao. Hawasemi ila uwongo tu.
6. Huenda ukajihiliki nafsi yako kwa ajili yao,
kuwasikitikia kwa kuwa hawayaamini mazungumzo haya!
7. Kwa hakika tumevifanya vilioko juu ya ardhi kuwa ni
pambo lake ili tuwafanyie mtihani, ni nani kati yao wenye vitendo vizuri zaidi.
8. Na hakika Sisi tutavifanya vyote vilio juu ya ardhi kuwa
kama nchi ilio pigwa na ukame.
9. Bali unadhani ya kwamba wale Watu wa Pangoni na
Maandishi walikuwa ni ajabu miongoni mwa ishara zetu?
10. Vijana hao walipo kimbilia kwenye pango walisema: Mola
wetu Mlezi! Tupe rehema itokayo kwako, na tutengezee uwongofu katika jambo
letu.
11. Tukayaziba masikio yao kuwalaza humo pangoni kwa muda
wa miaka kadhaa wa kadhaa.
12. Kisha tukawazindua ili tujue ni lipi katika makundi
mawili lilio hisabu sawa muda walio kaa.
13. Sisi tunakusimulia khabari zao kwa kweli. Hakika wao
walikuwa ni vijana walio muamini Mola wao Mlezi. Na Sisi tukawazidisha
uwongofu.
14. Na tukazitia nguvu nyoyo zao walipo simama na wakasema:
Mola wetu Mlezi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi. Hatutamwita mwenginewe kabisa
badala yake kuwa ni Mungu. Hivyo itakuwa tumesema jambo la kuvuka mpaka.
15. Hawa watu wetu wameshika miungu mingine badala yake
Yeye. Kwa nini basi hawawatolei uthibitisho ulio dhaahiri? Na nani aliye
dhaalimu zaidi kuliko anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu?
16. Na mkijitenga nao na vile wanavyo viabudu badala ya
Mwenyezi Mungu, basi kimbilieni pangoni, akufungulieni Mola wenu Mlezi rehema
yake, na akutengenezeeni ya kukufaeni katika mambo yenu.
17. Na unaliona jua linapo chomoza linainamia kuliani mwao
kutoka hapo pangoni; na linapo kuchwa linawakwepa kushotoni, na wao wamo katika
uwazi wa pango. Hizo ni katika ishara za Mwenyezi Mungu. Ambaye Mwenyezi Mungu
anamwongoa basi huyo ni mwenye kuongoka. Na anaye muacha kupotea basi
hutampatia mlinzi wala mwongozi.
18. Nawe utawadhania wamacho, na hali wamelala. Nasi
tunawageuza kulia na kushoto. Na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele
kizingitini. Kama ungeli watokea hapana shaka ungeli geuka kuwakimbia, nawe
umejaa khofu.
19. Na kwa namna hii tuliwainua usingizini wapate kuulizana
wao kwa wao. Alisema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku.
Wakasema: Mola wenu Mlezi anajua zaidi muda mlio kaa. Hebu mtumeni mmoja wenu
na hizi fedha zenu ende mjini, akatazame chakula chake kipi kilicho bora kabisa
akuleteeni cha kukila. Naye afanye mambo hayo kwa busara, wala asikutajeni
kabisa kwa yeyote.
20. Kwani wao
wakikutambueni watakupigeni mawe, au watakurudisheni katika dini yao; na hapo
hamtafanikiwa kabisa!
21. Na namna
hivi tuliwa juulisha kwa watu wapate kujua ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni
ya kweli, na kwamba Saa haina shaka. Walipo kuwa wakigombania jambo lao wao kwa
wao walisema: Jengeni jengo juu yao. Mola wao Mlezi anawajua vyema. Wakasema
walio shinda katika shauri yao: Bila ya shaka tutawajengea msikiti juu yao.
22. Watasema:
Walikuwa watatu, wa nne wao ni mbwa wao. Na wanasema: Walikuwa watano, wa sita
wao ni mbwa wao. Wanavurumisha ovyo. Na wanasema: Walikuwa saba, na wa nane wao
ni mbwa wao. Sema: Mola wangu Mlezi ndiye anaye jua sawa sawa hisabu yao. Hawawajui ila wachache tu. Basi usibishane
juu yao ila kwa mabishano ya juu juu tu hivi. Wala usiulize khabari zao kwa
yeyote yule.
23. Wala usisema
kamwe kwa jambo lolote lile: Hakika nitalifanya hilo kesho -
24. Isipo kuwa Mwenyezi
Mungu akipenda. Na mkumbuke Mola wako Mlezi pale unapo sahau, na sema: Asaa
Mola wangu Mlezi ataniongoa kwenye uwongozi ulio karibu zaidi kuliko huu.
25. Na walikaa
katika pango lao miaka mia tatu, na wakazidisha tisa.
26. Sema:
Mwenyezi Mungu anajua zaidi muda walio kaa. Ni zake tu siri za mbingu na ardhi.
Kuona kulioje na kusikia kwake! Hawana mlinzi isipo kuwa Yeye, wala
hamshirikishi yeyote katika hukumu yake.
27. Na soma
uliyo funuliwa katika Kitabu cha Mola wako Mlezi. Hapana wa kubadilisha maneno
yake. Wala nawe hutapata makimbilio isipo kuwa kwake.
28. Na isubirishe
nafsi yako pamoja na wanao muomba Mola wao Mlezi asubuhi na jioni, hali ya kuwa
wanataka radhi yake. Wala macho yako yasiwaruke kwa kutaka pambo la maisha ya
dunia. Wala usimt'ii tuliye mghafilisha moyo wake asitukumbuke, na akafuata
matamanio yake yakawa yamepita mpaka.
29. Na sema: Hii
ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae. Hakika Sisi
tumewaandalia wenye kudhulumu Moto ambao utawazunguka kama khema. Na wakiomba
msaada watasaidiwa kwa kupewa maji kama mafuta yaliyo tibuka. Yatayo wababua
nyuso zao. Kinywaji hicho ni kiovu mno! Na matandiko hayo ya kupumzikia ni
maovu mno!
30. Hakika wale
walio amini na wakatenda mema - hakika Sisi hatupotezi ujira wa anaye tenda
mema.
31. Hao watapata Bustani za milele, zinazo pita mito kati
yake. Humo watapambwa kwa mavazi ya mikononi ya dhahabu, na watavaa nguo za
kijani za hariri na at'ilasi, huku wakiegemea humo juu ya makochi. Ni malipo
bora hayo! Na matandiko mazuri mno ya kupumzikia!
32. Na wapigie mfano wa watu wawili: mmoja wao tulimpa
vitalu viwili vya mizabibu, na tukavizungushia mitende, na kati yake tukatia
mimea ya nafaka.
33. Na hivyo vitalu viwili vikitoa mazao yake, wala hapana
kitu katika hayo kilicho tindikia. Na ndani yake tukapasua mito.
34. Naye alikuwa na mazao mengi. Basi akamwambia mwenzake
naye akibishana naye: Mimi nimekushinda wewe kwa mali na nguvu za watu!
35. Na akaingia kitaluni kwake, naye hali anajidhulumu
nafsi yake. Akasema: Sidhani kabisa kuwa haya yataharibika.
36. Wala sidhani kuwa hiyo Saa (ya Kyama) itatokea. Na
ikiwa nitarudishwa kwa Mola wangu Mlezi, bila ya shaka nitapata marejeo bora
zaidi kuliko haya.
37. Mwenzake akamwambia kwa kubishana naye: Je! Unamkufuru
aliye kuumba kutokana na udongo, tena kutokana na tone la manii, kisha
akakufanya mtu kaamili?
38. Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi. Wala
simshirikishi na yeyote.
39. Na lau kuwa ulipo ingia kitaluni kwako ungeli sema:
Mashaallah! Alitakalo Mwenyezi Mungu huwa! Hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu.
Ikiwa unaniona mimi nina mali kidogo na watoto kuliko wewe,
40. Basi huenda Mola wangu Mlezi akanipa kilicho bora kuliko
kitalu chako, naye akapitisha kudra yake kutoka mbinguni kukilitea hicho chako,
na kikageuka ardhi tupu inayo teleza.
41. Au
maji yake yakadidimia wala usiweze kuyagundua.
42.
Yakateketezwa matunda yake, akabaki akipindua pindua viganja vyake, kwa vile
alivyo yagharimia, na miti imebwagika juu ya chanja zake. Akawa anasema: Laiti
nisingeli mshiriki Mola wangu Mlezi na yeyote!
43. Wala
hakuwa nacho kikundi cha kumsaidia badala ya Mwenyezi Mungu, wala mwenyewe
hakuweza kujisaidia.
44. Huko
ulinzi ni wa Mwenyezi Mungu wa Haki tu. Yeye ndiye mbora wa malipo, na mbora wa
matokeo.
45. Na
wapigie mfano wa maisha ya dunia. Hayo ni kama maji tunayo yateremsha kutoka
mbinguni, yakachanganyika na mimea ya ardhi, kisha hiyo mimea ikawa vibuwa
vinavyo peperushwa na upepo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila
kitu.
46. Mali na wana ni pambo la maisha ya dunia. Na mema yanayo
bakia ni bora mbele ya Mola wako Mlezi kwa malipo, na bora kwa matumaini.
47. Na siku tutapo iondoa milima na ukaiona ardhi iwazi, na
tukawafufua - wala hatutamwacha hata mmoja kati yao -
48. Na wakahudhurishwa mbele ya Mola wako Mlezi kwa safu
(wakaambiwa): Mmetujia kama tulivyo kuumbeni mara ya kwanza! Bali mlidai kwamba
hatutakuwekeeni miadi.
49. Na
kitawekwa kitabu. Basi utawaona wakosefu wanavyo ogopa kwa yale yaliomo humo. Na
watasema: Ole wetu! Kitabu hichi kina nini! Hakiachi dogo wala kubwa ila
huliandika? Na watayakuta yote waliyo yatenda yamehudhuria hapo. Na Mola wako
Mlezi hamdhulumu yeyote.
50. Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam! Walimsjudia
isipo kuwa Iblisi. Yeye alikuwa miongoni mwa majini, na akavunja amri ya Mola
wake Mlezi. Je! Mnamshika yeye na dhuriya zake kuwa marafiki badala yangu, hali
wao ni adui zenu? Ni ovu mno badala hii kwa wenye kudhulumu.
|