1 - 50
1. Kaf Ha Ya A'yn S'ad
2. Huu ni Ukumbusho wa rehema ya Mola wako Mlezi kwa mja
wake, Zakariya.
3. Alipo mwita Mola wake Mlezi kwa siri.
4. Akasema: Mola wangu Mlezi! Mafupa yangu yamedhoofika, na
kichwa kinameremeta kwa mvi; wala, Mola wangu Mlezi, sikuwa mwenye bahati mbaya
kwa kukuomba Wewe.
5. Na hakika mimi nawakhofia jamaa zangu baada yangu. Na
mke wangu ni tasa. Basi nipe mrithi kutoka kwako.
6. Atakaye nirithi mimi na awarithi ukoo wa Yaaqub. Ewe
Mola wangu Mlezi! Na umjaalie awe mwenye kuridhisha.
7. (Akaambiwa): Ewe Zakariya! Hakika Sisi tunakubashiria
mwana; jina lake ni Yahya. Hatujapata kumpa jina hilo yeyote kabla yake.
8. Akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Vipi nitakuwa na mwana na
hali mke wangu ni tasa, na mimi nimesha fikia ukongwe katika uzee?
9. Akasema: Ndio hivyo hivyo amesema Mola wako Mlezi: Haya
ni mepesi kwangu. Na hakika Mimi nilikwisha kuumba wewe zamani na hali hukuwa
kitu.
10. Akasema: Mola wangu Mlezi nijaalie Ishara. Akasema
Ishara yako ni kuwa hutasema na watu kwa masiku matatu, na hali ni mzima.
11. Basi akawatokea watu wake kutoka mihirabuni.
Akawaashiria: Msabihini Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni.
12. Ewe
Yahya! Kishike Kitabu kwa nguvu! Nasi tulimpa hikima angali mtoto.
13. Na tukampa huruma itokayo kwetu, na utakaso, na akawa
mchamungu.
14. Na akawa mwema kwa wazazi wake, wala hakuwa jabari
mua'si.
15. Na amani iwe juu yake siku ya kuzaliwa, na siku ya
kufa, na siku ya kufufuliwa.
16. Na mtaje Maryamu katika Kitabu, pale alipo jitenga na
jamaa zake mahali upande wa mashariki;
17. Na akaweka pazia kujikinga nao. Tukampelekea Roho wetu,
akajifananisha kwake sawa na mtu.
18. (Maryamu) akasema: Hakika mimi najikinga kwa Mwingi wa
Rehema aniepushe nawe, ukiwa ni mchamngu.
19. (Malaika) akasema: Hakika mimi ni mwenye kutumwa na Mola
wako Mlezi ili nikubashirie tunu ya mwana aliye takasika.
20. Akasema: Nitampataje mwana hali mwanaadamu yeyote
hajanigusa, wala mimi si kahaba?
21. (Malaika) akasema: Ndio hivyo hivyo! Mola wako Mlezi
amesema: Haya ni mepesi kwangu! Na ili tumfanye kuwa ni Ishara kwa watu, na
Rehema itokayo kwetu, na hilo ni jambo lilio kwisha hukumiwa.
22. Basi akachukua mimba yake, na akaondoka nayo mpaka
mahali pa mbali.
23. Kisha uchungu ukampeleka kwenye shina la mtende;
akasema: Laiti ningeli kufa kabla ya haya, na nikawa niliye sahaulika kabisa!
24. Pakatangazwa kutoka chini yake: Usihuzunike! Hakika
Mola wako Mlezi amejaalia chini yako kijito kidogo cha maji!
25. Na litikise kwako hilo shina la mtende, utakuangushia
tende nzuri zilizo mbivu.
26. Basi kula, na kunywa, na litue jicho lako. Na pindi
ukimwona mtu yeyote basi sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu
ya kufunga; kwa hivyo leo sitasema na mtu.
27. Akenda naye (mwanawe) kwa jamaa zake amembeba. Wakasema: Ewe Maryamu! Hakika umeleta kitu
cha ajabu!
28. Ewe
dada yake Harun! Baba yako hakuwa mtu muovu, wala mama yako hakuwa kahaba.
29. Akawaashiria (mtoto). Wakasema: Vipi tumsemeze aliye
bado mdogo yumo katika mlezi?
30. (Mtoto) akasema: Hakika mimi ni mtumwa wa Mwenyezi
Mungu. Amenipa Kitabu, na amenifanya Nabii.
31. Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo.
Na ameniusia Sala na Zaka maadamu ni hai,
32. Na nimtendee wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe
jeuri, mwovu.
33. Na amani iko juu yangu siku niliyo zaliwa, na siku
nitakayo kufa, na siku nitakayo fufuliwa kuwa hai.
34. Huyo ndiye Isa mwana wa Maryamu. Ndiyo kauli ya haki
ambayo wanaifanyia shaka.
35. Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwa na mwana, Subhanahu, Yeye
ametakasika! Anapo lihukumia jambo basi huliambia tu: Kuwa! Likawa.
36. Na
hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Basi
muabuduni Yeye. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
37. Lakini makundi yakakhitalifiana wao kwa wao. Basi ole
wao hao walio kufuru kwa kuhudhuria Siku iliyo kuu!
38. Watasikia na wataona vizuri vilioje Siku watakayo
tufikia! Lakini madhaalimu sasa wamo katika upotofu ulio dhaahiri.
39. Na waonye siku ya majuto itapo katwa amri. Nao wamo
katika ghafla, wala hawaamini.
40. Hakika Sisi tutairithi ardhi na walio juu yake. Na kwetu
watarejeshwa.
41. Na mtaje katika Kitabu Ibrahim. Hakika yeye alikuwa
mkweli, Nabii.
42. Alipo mwambia baba yake: Ewe baba yangu! Kwa nini
unaabudu visivyo sikia, na visivyo ona, na visivyo kufaa chochote?
43. Ewe
baba yangu! Kwa yakini imenifikia ilimu isiyo kufikia wewe. Basi nifuate
mimi, nami nitakuongoza Njia Iliyo Sawa.
44. Ewe
baba yangu! Usimuabudu Shet'ani. Hakika Shet'ani ni mwenye kumuasi Mwingi wa
Rehema.
45. Ewe
baba yangu! Hakika mimi naogopa isikupate adhabu inayo toka kwa Mwingi wa
Rehema ukaja kuwa mwenziwe Shet'ani.
46. (Baba)
akasema: Unaichukia miungu yangu, ewe Ibrahim? Kama huachi, basi lazima
nitakupiga mawe. Na niondokelee mbali kwa muda!
47. (Ibrahim) akasema: Salamun a'laika! Amani iwe juu yako!
Mimi nitakuombea msamaha kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ananihurumia sana.
48. Nami najitenga nanyi na hayo mnayo yaabudu badala ya
Mwenyezi Mungu. Na ninamwomba Mola wangu Mlezi; asaa nisiwe mwenye kukosa
bahati kwa kumwomba Mola wangu Mlezi.
49. Basi alipo jitenga nao na yale waliyo kuwa wakiyaabudu
badala ya Mwenyezi Mungu, tulimpa Is-haq na Yaaqub, na kila mmoja tukamfanya
Nabii.
50. Na tukawapa rehema zetu na tukawajaalia kupewa sifa za
kweli tukufu.
|