Table of Contents | Words: Alphabetical - Frequency - Inverse - Length - Statistics | Help | IntraText Library

Qu'rani

IntraText CT - Text

  • 2. SURA AL- BAQARA
Previous - Next

Click here to show the links to concordance

2. SURA AL- BAQARA

(Imeteremka Madina)

Sura hii imeteremka Madina baada ya Hijra. Nayo ndiyo sura ndefu kuliko zote katika kwa mujibu wa mtungo wa Msahafu. Sura hii imeanzia kueleza kwa tafsili yale yaliyo malizikia Sura ya Al Faatiha. Imetaja kuwa Qur'ani ndiyo msingi wa uwongofu, na imewataja wale walio neemeshwa na Mwenyezi Mungu kwa kupata radhi zake, na wale walio kasirikiwa, nao ni makafiri na wanaafiki.
Sura imeeleza ukweli wa Qur'ani, na kwamba wito wake ni wa kweli usio na shaka. Kisha ikaingia kueleza namna tatu za watu: Waumini, Makafiri na Wanaafiki. Na ikataja Daa'wa, Mlingano, au Wito, kuwaita watu wamuabudu Mwenyezi Mungu pekee, na ikawaonya makafiri, na ikawapa bishara njema Waumini. Baadaye ikawaelekea Wana wa Israili khasa kwa kuwaita na kuwakumbusha siku za Mwenyezi Mungu, na kwa vituko vyao na Musa a.s. na kuwakumbusha khabari za Ibrahim na Ismail na walivyo ijenga Al Kaaba. Hayo yamechukua karibu nusu ya Sura. Mazungumzo yakawageukia Waumini wazingatie yaliyo wapata Mayahudi na Wakristo.
Mazungumzo yakaingia kuwasemeza watu wa Qur'ani kwa kuwakumbusha mambo ambayo umma wa Musa na umma wa Muhammad walivyo shirikiana katika kutukuzwa Ibrahim na kuongoka kwake na nasaba yake, na kwa kutaja kibla na mfano wa hayo.
Kisha yakaja mazungumzo juu ya Tawhid (Upweke wa Mwenyezi Mungu) na kukumbusha Ishara za Mwenyezi Mungu zenye kumuashiria Yeye. Na yakaja masimulizi juu ya ushirikina, na juu ya vyakula vilivyo harimishwa, na kwamba kuharimisha na kuhalalisha ni haki ya Mwenyezi Mungu peke yake.
Sura ikaingia kubainisha misingi ya wema, na kutaja baadhi ya hukumu za Saumu, na wasia, na kula mali ya watu kwa dhulma, na kisasi, na vita, na Hija, na ulevi, na kamari, na ndoa na talaka, na kunyonyesha, na eda na mengineyo. Hali kadhaalika yamezungumzwa mambo ya itikadi kwa jumla kama Utume, Tawhidi, kufufuliwa. Yametajwa mas-ala ya kutoa sadaka na Zaka, riba, biashara, kuandikiana madeni. Mwishoe Sura yakhitimisha kwa dua ya Waumini kumwomba Mola wao Mlezi awanusuru na awasaidie.
Sura hii imekusanya misingi kadhaa wa kadhaa. Miongoni mwayo ni:
Kwamba Njia ya Mwenyezi Mungu na kuishika Dini yake ni dharura kwa ajili ya kupata  mafanakio duniani na Akhera, na kwamba haielekei kwa mwenye akili kuwaita watu watende mema naye akajisahau mwenyewe; na ya kwamba yapasa kuchagua kheri kuliko shari, na kukhiari lilio bora kuliko lilio duni.
Na kwamba misingi ya Dini ni mitatu, nayo ni: Kumuamini Mwenyezi Mungu, Kuamini kufufuliwa, na Kutenda mema.
Na kwamba malipo ni kwa Imani na vitendo pamoja. Shuruti ya Imani ni kukiri kwa nafsi na kukubali kwa moyo kila alilo kuja nalo Mtume s.a.w., na kwamba wasio kuwa Waislamu hawatokuwa radhi na Waislamu mpaka Waislamu wafuate dini yao hao walio potea.
Na kwamba kwa jumla urafiki katika sharia yapasa uwe kwa wenye kushika Imani na uadilifu, sio kwa watu wa kufuru na dhulma, na kwamba Imani ya Dini ya Mwenyezi Mungu inalazimisha uwepo umoja na kuwafikiana, na kutofuata hayo huleta khitilafu na kutengana. Kwa ajili ya kupata mambo makuu inalazimu kutafuta msaada kwa Subira na Sala. Kufuata kipofu-pofu ni upotovu, na hupelekea ujinga na chuki za kitaifa.
Na kwamba Mwenyezi Mungu amewahalalishia waja wake vyakula vizuri na amewaharimishia vichache vilivyo viovu; wala haijuzu kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu kuhalalisha au kuharimisha kitu. Na vilivyo harimishwa huhalalishiwa mwenye dharura, kwa sababu dharura huruhusu vilivyo katazwa, na dharura hupimwa kwa kadiri yake. Dini imejengwa juu ya wepesi na kuondoa mikazo. Kwani Mwenyezi Mungu hailazimishi nafsi ila kwa kiasi ya uwezo wake, wala hawaamrishi waja wake ila kwa wanalo liweza. Ni haramu, haijuzu mtu kujipelekea nafsi yake kwenye maangamizo. Kila jambo hutafutwa kwa sababu zake na njia zake zitakao fikilia. Kulazimisha katika dini kunakatazwa. Kupigana vita ni kwa ajili ya kujilinda, na kwa ajili ya kuhifadhi uhuru wa dini, na kuulinda utukufu wa Uislamu katika miji yake.
Na kwamba Muislamu anayo haki ya kutaka sehemu yake katika dunia, kama anavyo tekeleza wajibu wake kwa ajili ya Akhera, na kwamba kutimiza haja na kuleta maslaha ni miongoni mwa makusudio ya Sharia.
Na kwamba Imani na Subira ni sababu mbili zinazo wapelekea wachache walio waadilifu kuwashinda wengi wenye kudhulumu, na kula mali ya watu kwa upotovu ni haramu, na mwanaadamu analipwa kwa vitendo vyake mwenyewe si kwa vitendo vya mwenginewe, na hikima ya utungaji sharia inafahamiwa na akili iliyo kaa sawa kwa kuwa ndani yake mna haki na uadilifu na maslaha ya waja.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU




Previous - Next

Table of Contents | Words: Alphabetical - Frequency - Inverse - Length - Statistics | Help | IntraText Library

Best viewed with any browser at 800x600 or 768x1024 on Tablet PC
IntraText® (V89) - Some rights reserved by EuloTech SRL - 1996-2007. Content in this page is licensed under a Creative Commons License