51 - 100
51. Na hakika tulikwisha mpa Ibrahim uwongofu wake zamani,
na tulikuwa tunamjua.
52. Alipo mwambia baba yake na watu wake: Ni nini haya
masanamu mnayo yashughulikia kuyaabudu?
53. Wakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu.
54. Akasema: Bila ya shaka nyinyi na baba zenu mmekuwa
katika upotofu ulio dhaahiri.
55. Wakasema: Je! Umetujia kwa maneno ya kweli au wewe ni
katika wachezao tu?
56. Akasema: Bali Mola wenu Mlezi ni Mola Mlezi wa mbingu
na ardhi ambaye ndiye aliye ziumba. Na mimi ni katika wenye kuyashuhudia hayo.
57. Na Wallahi! Nitayafanyia vitimbi masanamu yenu haya
baada ya mkisha geuka kwenda zenu.
58. Basi akayavunja vipande vipande, ila kubwa lao, ili wao
walirudie.
59. Wakasema: Nani aliye ifanyia haya miungu yetu? Hakika
huyu ni katika walio dhulumu.
60. Wakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja. Anaitwa
Ibrahim.
61. Wakasema: Mleteni mbele ya macho ya watu, wapate
kumshuhudia!
62. Wakasema: Je! Wewe umeifanyia haya miungu yetu, ewe
Ibrahim?
63. Akasema: Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao. Basi
waulizeni ikiwa wanaweza kutamka.
64. Basi wakajirudi nafsi zao, wakasema: Hakika nyinyi
mlikuwa madhaalimu!
65. Kisha wakarejea kwenye ule ule upotovu wao wakasema:
Wewe unajua kwamba hawa hawesemi.
66. Akasema: Basi nyinyi mnawaabudu asiye kuwa Mwenyezi
Mungu wasio kufaini kitu wala kukudhuruni?
67. Aibu yenu nyinyi na hivyo mnavyo viabudu badala ya
Mwenyezi Mungu! Basi nyinyi hamtii akilini?
68. Wakasema: Mchomeni moto, na muinusuru miungu yenu,
ikiwa nyinyi ni watendao jambo!
69. Sisi tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa
Ibrahim!
70. Wao walimkusudia maovu, lakini Sisi tukawafanya wao
ndio walio khasiri.
71. Na tukamwokoa yeye na Luut'i tukawapeleka kwenye nchi
tulio ibariki kwa ajili ya walimwengu wote.
72. Naye tukampa Is-haq, na Yaaqub kuwa ni ziada. Na wote
tukawajaalia wawe watu wema.
73. Na tukawafanya maimamu wakiongoa watu kwa amri yetu. Na
tukawafunulia watende kheri, na washike Sala, na watoe Zaka; na walikuwa
wanatuabudu Sisi tu.
74. Na Luut'i tukampa hukumu na ilimu na tukamwokoa na ule
mji ulio kuwa ukifanya maovu. Hakika hao walikuwa watu wabaya, wachafu.
75. Na tukamuingiza katika rehema yetu. Hakika yeye ni
miongoni mwa watenda mema.
76. Na Nuhu alipo ita zamani, nasi tukamuitikia, na
tukamwokoa yeye na watu wake kutokana na shida kubwa.
77. Na tukamnusuru na watu walio zikanusha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu wabaya. Basi
tukawazamisha wote.
78. Na Daud na Suleiman walipo kata hukumu katika kadhiya
ya konde walipo lisha humo mbuzi wa watu usiku. Na Sisi tulikuwa wenye
kushuhudia hukumu yao hiyo.
79. Tukamfahamisha Suleiman. Na kila mmoja wao tulimpa
hukumu na ilimu. Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imnyenyekee
na imtakase Mwenyezi Mungu. Na Sisi ndio tulio fanya hayo.
80. Na tukamfundisha kuunda mavazi ya vita kwa ajili yenu
ili yakuhifadhini katika kupigana kwenu. Je! Mtakuwa wenye kushukuru?
81. Na
tukamsahilishia Suleiman upepo wa kimbunga wendao kwa amri yake kwenye ardhi
tuliyo ibarikia. Na Sisi ndio tunao jua kila kitu.
82. Na pia mashet'ani wanao mpigia mbizi na kufanya kazi
nyenginezo. Na Sisi tulikuwa walinzi wao.
83. Na Ayyubu, alipo mwita Mola wake Mlezi, akasema: Mimi
yamenipata madhara. Na Wewe ndiye unaye rehemu kuliko wote wanao rehemu.
84. Basi tukamwitikia, na tukamwondolea madhara aliyo kuwa
nayo, na tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao kuwa ni rehema inayo toka
kwetu, na ukumbusho kwa wafanyao ibada.
85. Na Ismail, na Idris, na Dhulkifli - wote walikuwa
miongoni mwa wanao subiri.
86. Na tukawaingiza katika rehema yetu. Hakika wao walikuwa
katika watu wema.
87. Na Dhun-Nun alipoondoka hali ameghadhibika, na akadhani
ya kwamba hatutakuwa na uwezo juu yake. Basi aliita katika giza: Hapana mungu
isipo kuwa Wewe Subhanaka Uliye takasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa
wenye kudhulumu.
88. Basi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na dhiki. Na
hivyo ndivyo tunavyo waokoa Waumini.
89. Na Zakariya alipo mwita Mola wake Mlezi: Mola wangu
Mlezi! Usiniache peke yangu, na Wewe ndiye Mbora wa wanao rithi.
90. Basi tukamwitikia, na tukampa Yahya na tukamponyeshea
mkewe. Hakika wao walikuwa wepesi wa kutenda mema, na wakituomba kwa shauku na
khofu. Nao walikuwa wakitunyenyekea.
91. Na mwanamke aliye linda uke wake, na tukampulizia
katika roho yetu, na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa ni Ishara kwa walimwengu.
92. Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola
wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi.
93. Nao wakalikata jambo lao hili mapande mapande baina
yao. Wote watarudi kwetu.
94. Na atendaye mema naye ni Muumini basi haitakataliwa
juhudi yake. Na hakika Sisi tunamwandikia.
95.Na haiwi kwa wana-mji tulio uangamiza, ya kwamba
hawatarejea,
96. Mpaka watapo funguliwa Juju na Maajuju wakawa
wanateremka kutoka kila mlima;
97. Na miadi ya haki ikakaribia. Hapo ndipo yatapo kodoka
macho ya walio kufuru (na watasema:) Ole wetu! Bila ya shaka tulikuwa
tumeghafilika na haya, bali tulikuwa wenye kudhulumu.
98. Hakika nyinyi na hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi
Mungu ni kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu.
99. Lau kuwa hawa ni miungu, wasingeli ingia. Na wote
watadumu humo.
100. Lao wao humo ni kupiga mayowe, na wala hawatasikia
(jenginelo).
|