1 - 50
1. Enyi
watu! Mcheni Mola wenu Mlezi. Hakika tetemeko la Saa (ya Kiyama) ni
jambo kuu.
2. Siku mtapo iona, kila mwenye kunyonyesha atamsahau
amnyonyeshaye, na kila mwenye mimba ataharibu mimba yake. Na utaona watu
wamelewa, na kumbe hawakulewa. Lakini adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali.
3. Na miongoni mwa watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi
Mungu bila ya ilimu, na wanamfuata kila shet'ani aliye asi.
4. Ameandikiwa kwamba anaye mfanya kuwa rafiki, basi huyo
hakika atampoteza na atamwongoza kwenye adhabu ya Moto mkali.
5. Enyi
watu! Ikiwa nyinyi mna shaka ya kufufuliwa basi kwa hakika Sisi tulikuumbeni
kutokana na udongo, kisha kutokana na manii, kisha kutokana na kipande cha damu
ilio gandana, kisha kutokana na kipande cha nyama chenye umbo na kisicho kuwa
na umbo, ili tukubainishieni. Nasi tunakiweka katika matumbo ya uzazi tunacho
kitaka mpaka muda ulio wekwa. Kisha tunakutoeni kwa hali ya mtoto mchanga,
kisha mfikie kutimia akili. Na wapo katika nyinyi wanao kufa, na wapo katika
nyinyi wanao rudishwa kwenye umri wa unyonge kabisa, hata mtu awe hajui kitu
baada ya kuwa anakijua. Na unaiona ardhi imetulia kimya, lakini tunapo
yateremsha maji juu yake husisimka na kututumka, na kumea kila namna ya mimea
mizuri.
6. Hayo ni
kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ndiye Haki, na kwamba hakika Yeye ndiye mwenye
kuhuisha wafu, na kwamba hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.
7. Na
kwamba hakika Saa itakuja hapana shaka kwa hilo, na kwamba hakika Mwenyezi
Mungu atawafufua walio makaburini.
8. Na
katika watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilimu, wala
uwongofu, wala Kitabu chenye nuru.
9. Anaye
geuza shingo yake ili kupoteza watu waache Njia ya Mwenyezi Mungu. Duniani
atapata hizaya, na Siku ya Kiyama tutamwonjesha adhabu ya kuungua.
10.
(Ataambiwa): Hayo ni kwa sababu ya iliyo tanguliza mikono yako. Na hakika
Mwenyezi Mungu si dhaalimu kwa waja.
11. Na
katika watu wapo wanao muabudu Mwenyezi Mungu kwa ukingoni. Ikimfikia kheri
hutulia kwayo, na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake. Amekhasiri dunia na
Akhera; hiyo ndiyo khasara iliyo wazi.
12. Badala
ya Mwenyezi Mungu, yeye huomba kisicho mdhuru wala kumnufaisha. Huko ndiko
kupotolea mbali!
13.
Humuomba yule ambaye bila ya shaka dhara yake ipo karibu zaidi kuliko nafuu
yake. Kwa hakika huyo ni mlinzi muovu, na rafiki muovu.
14. Hakika
Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na wakatenda mema katika Bustani
zipitazo mito kati yake. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda atakayo.
15. Anaye
dhani kwamba Mwenyezi Mungu hatamnusuru (Mtume) katika dunia na Akhera na
afunge kamba kwenye dari kisha aikate. Atazame je hila yake itaondoa hayo
yaliyo mkasirisha?
16. Na
namna hivi tumeiteremsha (Qur'ani) kuwa ni Aya zilizo wazi, na hakika Mwenyezi
Mungu humwongoa amtakaye.
17. Hakika
walio amini, na ambao ni Mayahudi na Wasabai na Wakristo na Majusi na wale
walio shiriki - hakika Mwenyezi Mungu atawapambanua baina yao Siku ya Kiyama.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa kila kitu.
18. Je!
Huoni kwamba vinamsujudia Mwenyezi Mungu viliomo mbinguni na viliomo katika
ardhi, na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti, na wanyama, na wengi
miongoni mwa watu. Na wengi imewastahiki adhabu. Na anaye fedheheshwa na
Mwenyezi Mungu hana wa kumhishimu. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda apendayo.
19. Hawa
wagomvi wawili walio gombana kwa ajili ya Mola wao Mlezi. Basi walio kufuru
watakatiwa nguo za moto, na yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yanayo chemka.
20. Kwa
maji hayo vitayayushwa viliomo matumboni mwao, na ngozi zao pia.
21. Na kwa
ajili yao yatakuwapo marungu ya chuma.
22. Kila
wakitaka kutoka humo kwa sababu ya uchungu watarudishwa humo humo, na
wataambiwa: Onjeni adhabu ya kuungua!
23. Hakika
Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na wakatenda mema katika Bustani
zipitiwazo na mito kati yake. Watapambwa humo kwa mapambo ya mikononi ya
dhahabu na lulu. Na mavazi yao humo ni hariri.
24. Na wataongozwa kwenye maneno mazuri, na wataongozwa
kwenye Njia ya Msifiwa.
25. Hakika wale walio kufuru na wakazuilia Njia ya Mwenyezi
Mungu na Msikiti Mtakatifu, ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawasawa,
kwa wakaao humo na wageni. Na kila atakaye taka kufanya upotofu humo kwa
dhulma, basi tutamwonjesha adhabu chungu.
26. Na pale tulipomweka Ibrahim pahala penye ile Nyumba
tukamwambia: Usinishirikishe na chochote; na isafishe Nyumba yangu kwa ajili ya
wanao izunguka kwa kut'ufu, na wanao kaa hapo kwa ibada, na wanao rukuu, na
wanao sujudu.
27. Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya
kila ngamia aliye konda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali.
28. Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Mwenyezi
Mungu katika siku maalumu juu ya nyama hoa alio waruzuku. Basi kuleni katika
hao na mlisheni mwenye shida aliye fakiri.
29. Kisha wajisafishe taka zao, na waondoe nadhiri zao, na
waizunguke Nyumba ya Kale.
30. Ndio hivyo iwe! Na anaye vitukuza vitakatifu vya
Mwenyezi Mungu basi hayo ndiyo kheri yake mbele ya Mola wake Mlezi. Na
mmehalalishiwa nyama hoa ila wale mlio somewa. Basi jiepusheni na uchafu wa
masanamu, na jiepusheni na usemi wa uwongo.
31. Kwa kumtakasikia Imani Mwenyezi Mungu, bila ya
kumshirikisha. Na anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka
kutoka mbinguni, kisha ndege wakamnyakua au upepo ukamtupa pahala mbali.
32. Ndio hivyo! Na anayetukuza ibada za Mwenyezi Mungu,
basi hayo ni katika unyenyekevu wa nyoyo.
33. Katika hao nyinyi mna manufaa mpaka muda maalumu. Kisha
pahala pa kuchinjiwa kwake ni kwenye Nyumba ya Kale.
34. Na kila umma tumewafanyia mahala pa kuchinjia mihanga
ya ibada ili walitaje jina la Mwenyezi Mungu juu ya vile walivyo ruzukiwa
katika wanyama wa mifugo. Basi Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Jisalimishieni
kwake tu, na wabashirie wanyenyekevu,
35. Ambao, anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hutetemeka,
na wanao vumilia kwa yanao wasibu, na wanao shika Sala, na wanatoa katika
tulivyo waruzuku.
36. Na ngamia wa sadaka tumekufanyieni kuwa ni kudhihirisha
matukuzo kwa Mwenyezi Mungu; kwa hao mna kheri nyingi. Basi litajeni jina la
Mwenyezi Mungu juu yao wanapo simama kwa safu. Na waangukapo ubavu kuleni
katika hao na walisheni walio kinai na wanao lazimika kuomba. Ndio kama hivi
tumewafanya hawa wanyama dhalili kwenu ili mpate kushukuru.
37. Nyama zao hazimfikii Mwenyezi Mungu wala damu zao,
lakini unamfikia uchamngu wenu. Namna hivi tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze
Mwenyezi Mungu kwa alivyo kuongoeni. Na wabashirie wafanyao mema.
38. Hakika
Mwenyezi Mungu huwakinga walio amini. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila
khaini mwingi wa kukanya mema.
39.
Wameruhusiwa kupigana wale wanao pigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa - na kwa
yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia -
40. Wale
ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa wanasema: Mola wetu
Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawakingi watu kwa watu,
basi hapana shaka zingeli vunjwa nymba za wat'awa, na makanisa, na masinagogi,
na misikiti, ambamo ndani yake jina la Mwenyezi Mungu linatajwa kwa wingi. Na
bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anaye msaidia Yeye. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu.
41. Wale
ambao tukiwapa madaraka katika nchi husimamisha Sala, na wakatoa Zaka, na
wakaamrisha mema, na wakakataza mabaya. Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya
mambo yote.
42. Na
wakikukanusha basi walikwisha kanusha kabla yao watu wa Nuhu, na kina A'ad na
kina Thamud,
43. Na
watu wa Ibrahim na watu wa Lut'i
44. Na watu wa Madiana. Na Musa pia alikanushwa. Nikawapa muda
makafiri, kisha nikawatia mkononi. Basi ilikuwaje adhabu yangu!
45. Miji mingapi tuliiangamiza iliyo kuwa ikidhulumu, ikawa
imebaki magofu, na visima vilivyo achwa, na majumba yaliyo kuwa madhubuti?
46. Je! Hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na nyoyo
zao za kuzingatia, au masikio ya kusikilia? Kwani hakika si macho yanayo
pofuka, lakini zinazo pofuka ni nyoyo ziliomo vifuani.
47. Na wanakuhimiza ulete adhabu, lakini Mwenyezi Mungu
hatakwenda kinyume na ahadi yake kabisa. Na hakika siku moja kwa Mola wako
Mlezi ni kama miaka elfu mnavyo hisabu nyinyi.
48. Na miji mingapi niliipa muda na hali ilikuwa
imedhulumu, na kisha nikaitia mkononi? Na kwangu Mimi ndio marudio yote.
49. Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni mwonyaji kwenu niliye
dhaahiri.
50. Basi walio amini na wakatenda mema watapata maghfira na
riziki za ukarimu.
|