1 - 50
1. HAKIKA wamefanikiwa Waumini,
2. Ambao ni wanyenyekevu katika Sala zao,
3. Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi,
4. Na ambao wanatoa Zaka,
5.Na ambao wanazilinda tupu zao,
6. Isipo kuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono yao
ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa.
7. Lakini anaye taka kinyume cha haya, basi hao ndio
warukao mipaka.
8. Na ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao,
9. Na ambao Sala zao wanazihifadhi -
10. Hao ndio warithi,
11. Ambao watairithi Pepo ya Firdausi, wadumu humo.
12. Na kwa yakini tumemuumba mtu kutokana na asli ya
udongo.
13. Kisha tukamjaalia awe tone ya mbegu ya uzazi katika
kalio madhubuti.
14. Kisha tukaiumba tone kuwa damu iliyo ganda, na
tukaiumba damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa
mifupa, na mifupa tukaivika nyama. Kisha tukamfanya kiumbe mwengine. Basi
ametukuka Mwenyezi Mungu Mbora wa waumbaji.
15. Kisha hakika nyinyi baada ya hayo mtakufa.
16. Kisha hakika nyinyi Siku ya Kiyama mtafufuliwa.
17. Na kwa yakini tumeziumba juu yenu njia saba. Nasi
hatukuwa wenye kughafilika na viumbe.
18. Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi na
tukayatuliza katika ardhi. Na hakika Sisi tunaweza kuyaondoa.
19. Kwa maji hayo tukakufanyieni bustani za mitende na
mizabibu, mnapata humo matunda mengi, na katika hayo mnakula;
20. Na mti utokao katika mlima wa Sinai, unatoa mafuta na
kuwa kitoweo kwa walao.
21. Na hakika mnayo mazingatio makubwa katika nyama hoa -
tunakunywesheni katika vile viliomo matumboni mwao, na nyinyi mnapata katika
hao manufaa mengi, na pia mnawala.
22. Na juu yao na juu ya marikebu mnabebwa.
23. Na hakika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, akasema: Enyi
watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna mungu asiye kuwa Yeye. Basi je! Hamwogopi?
24. Walisema wale
wakuu walio kufuru katika watu wake: Huyu si chochote ila ni mtu tu kama
nyinyi. Anataka kujipa ubora juu yenu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu amependa basi
yakini angeli teremsha Malaika. Hatukusikia haya kwa baba zetu wa zamani.
25. Huyu si
lolote ila ni mtu mwenye wazimu. Basi mngojeeni tu kwa muda.
26. Akasema
(Nuhu): Mola wangu Mlezi! Ninusuru kwa kuwa wamenikanusha.
27. Tukampa
wahyi: Unda jahazi mbele ya macho yetu na uwongozi wetu! Basi itapo fika amri
yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize ndani yake wa kila namna dume na jike,
na ahali zako, isipo kuwa yule ambaye katika wao juu yake imekwisha tangulia
kauli. Wala usinitajie hao walio dhulumu. Kwani hao bila ya shaka
watazamishwa.
28. Basi utakapo tulia wewe na walio pamoja nawe humo
marikebuni, sema: Alhamdulillahi Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, aliye
tuokoa na watu madhaalimu!
29. Na sema: Mola wangu Mlezi! Niteremshe mteremsho wenye
baraka, na Wewe ni Mbora wa wateremshaji.
30. Hakika katika hayo yapo mazingatio. Na kwa yakini Sisi
ni wenye kuwafanyia mtihani.
31. Kisha baada yao tukaanzisha kizazi kingine.
32. Tukawapelekea Mtume miongoni mwao, kuwaambia: Muabuduni
Mwenyezi Mungu! Hamna mungu
asiye kuwa Yeye. Jee, hamwogopi?
33. Na
wakubwa katika watu wake walio kufuru na wakakanusha mkutano wa Akhera, na
tukawadekeza kwa starehe katika maisha ya dunia, walisema: Huyu si chochote ila
ni binaadamu kama nyinyi; anakula mlacho, na anakunywa mnywacho.
34. Na
nyinyi mkimt'ii mtu kama nyinyi basi hakika mtakuwa khasarani.
35. Hivyo
anakuahidini ati ya kwamba mtakapo kufa na mkawa udongo na mifupa kuwa
mtatolewa?
36. Hayawi!
Hayawi hayo mnayo ahidiwa.
37. Hapana ila uhai wetu wa duniani tu, tunakufa na kuishi
basi. Wala sisi hatutafufuliwa.
38. Huyu si lolote ila ni mtu anaye mzulia Mwenyezi Mungu
uwongo, wala sisi sio wa kumuamini.
39. Akasema: Mola wangu Mlezi! Ninusuru kwa sababu
wananikanusha.
40. (Mwenyezi Mungu) akasema: Baada ya muda mchache
watakuwa wenye kujuta.
41. Basi ukawanyakua ukelele kwa haki, na tukawafanya kama
takataka zinazo elea juu ya maji. Ikapotelea mbali kaumu ya madhaalimu!
42. Kisha tukaleta baada yao vizazi vingine.
43. Hapana umma uwezao kutanguliza ajali yake wala
kuikawiza.
44. Kisha tukawatuma Mitume wetu, mmoja baada ya mmoja.
Kila umma alipo wafikia Mtume wao walimkanusha. Tukawafuatanisha hawa baada ya hawa,
na tukawafanya ni hadithi za kusimuliwa. Wakapotelea mbali watu wasio amini.
45. Kisha tukamtuma Musa na nduguye, Haaruni, pamoja na
ishara zetu na hoja zilizo wazi.
46. Kumwendea Firauni na wakuu wake. Lakini walijivuna, nao
walikuwa watu majeuri.
47. Wakasema: Je, tuwaamini wanaadamu wawili hawa kama
sisi, na ambao watu wao ni watumwa wetu?
48. Basi wakawakanusha, na wakawa miongoni mwa walio
angamizwa.
49. Na hakika tulimpa Musa Kitabu ili wapate kuongoka.
50. Na tukamfanya mwana wa Mariamu na mama yake kuwa ni
Ishara, na tukawapa makimbilio kwenda mahali palipo inuka penye utulivu na
chemchem za maji.
|