51 - 100
51. Enyi Mitume! Kuleni vyakula vizuri na tendeni mema.
Hakika Mimi ni Mjuzi wa mnayo yatenda.
52. Na kwa yakini huu Umma wenu ni Umma mmoja, na Mimi ni
Mola wenu Mlezi, basi nicheni Mimi.
53. Lakini walikatiana jambo lao mapande mbali mbali. Kila
kundi likifurahia kwa waliyo nayo.
54. Basi waache katika ghafla yao kwa muda.
55. Je! Wanadhani ya kuwa kwa vile tunavyo wapa mali na
watoto
56. Ndio tunawahimizia kheri? Lakini wenyewe hawatambui.
57. Kwa
hakika hao ambao kwa kumwogopa Mola wao Mlezi wananyenyekea,
58. Na wale ambao Ishara za Mola wao Mlezi wanaziamini,
59. Na wale ambao Mola wao Mlezi hawamshirikishi,
60. Na wale ambao wanatoa walicho pewa, na hali nyoyo zao
zinagopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao Mlezi,
61. Basi wote hao ndio wanao kimbilia katika mambo ya
kheri, na ndio watakao tangulia kuyafikia.
62. Na hatuilazimishi nafsi ila kwa kadri ya uwezo wake. Na
tunacho kitabu kisemacho kweli. Nao hawatadhulumiwa.
63. Lakini nyoyo zao zimeghafilika na hayo, na wanavyo
vitendo vinginevyo wanavyo vifanya.
64. Hata tutakapo watia katika adhabu wale walio dekezwa
kwa starehe kati yao, hapo ndipo watapo yayatika.
65. Msiyayatike leo! Hakika nyinyi hamtanusurika nasi.
66. Hakika zilikuwa Aya zangu mkisomewa, nanyi mkirudi
nyuma juu ya visigino vyenu,
67. Na huku mkitakabari na usiku mkiizungumza (Qur'ani) kwa
dharau.
68. Je, hawakuifikiri kauli, au yamewajia yasiyo wafikia
baba zao wa zamani?
69. Au hawakumjua Mtume wao, ndio maana wanamkataa?
70. Au wanasema:
Ana wazimu? Bali amewajia kwa Haki, na wengi wao wanaichukia Haki.
71. Na lau kuwa
Haki ingeli fuata matamanio yao, basi zingeli haribika mbingu na ardhi na
waliomo ndani. Bali tumewaletea ukumbusho wao, nao wanajitenga mbali na
ukumbusho wao.
72. Au unawaomba
ujira? Lakini ujira wa Mola wako Mlezi ni bora, na Yeye ndiye Mbora wa wanao
ruzuku.
73. Na kwa
yakini wewe unawaita kwenye Njia Iliyo Nyooka.
74. Na hakika
wale wasio iamini Akhera wanajitenga na Njia hiyo.
75. Na lau
tungeli warehemu na tukawaondolea shida waliyo nayo bila ya shaka wangeli
endelea katika upotofu wao vile vile, wakitangatanga.
76. Na hakika
tuliwatia adhabu kali; lakini hawakuelekea kwa Mola wao Mlezi wala
hawakunyenyekea.
77. Mpaka tulipo
wafungulia mlango wa adhabu kali, hapo ndipo wakawa wenye kukata tamaa.
78. Na Yeye
ndiye aliye kuumbieni kusikia na kuona na nyoyo za kufahamu. Ni kuchache mno
kushukuru kwenu.
79. Na Yeye
ndiye aliye kuenezeni katika ardhi, na kwake Yeye mtakusanywa.
80. Na Yeye
ndiye anaye huisha na kufisha, na yake Yeye mabadiliko ya usiku na mchana. Basi je! Hamfahamu?
81. Bali
wanasema kama walivyo sema watu wa kwanza.
82. Walisema:
Je! Tukisha kufa tukawa udongo na mifupa ndio tutafufuliwa?
83. Tuliahidiwa haya sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa
haya ila ni visa vya uwongo vya watu wa zamani.
84. Sema: Ni ya nani ardhi na viliomo ndani yake, kama
nyinyi mnajua?
85. Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu! Sema: Basi, je, hamkumbuki?
86. Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu saba na Mola Mlezi
wa A'rshi Kuu?
87. Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Sema: Basi je,
hamwogopi?
88. Sema: Ni nani mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu,
naye ndiye anaye linda, wala hakilindwi asicho taka, kama mnajua?
89. Watasema: (Ufalme huo) ni wa Mwenyezi Mungu. Sema: Basi
vipi mnadanganyika?
90. Bali tumewaletea Haki, na kwa yakini hao ni waongo.
91. Mwenyezi Mungu hana mwana yeyote, wala hanaye mungu
mwengine. Inge kuwa hivyo basi kila mungu angeli chukua alivyo umba, na baadhi
yao wangeli washinda wengine. Mwenyezi Mungu ameepukana na sifa wanazo msifu.
92. Mjuzi wa siri na dhaahiri, na ametukuka juu ya hayo
wanayo mshirikisha nayo.
93. Sema: Mola wangu Mlezi! Ukinionyesha adhabu waliyo
ahidiwa,
94. Mola wangu Mlezi! Usinijaalie katika watu madhaalimu
hao.
95. Na hakika Sisi ni waweza wa kukuonyeshsa tuliyo
waahidi.
96. Kinga maovu kwa kutenda yaliyo mema zaidi. Sisi tunajua
wayasemayo.
97. Na sema: Mola wangu Mlezi! Najikinga kwako na wasiwasi
wa mashet'ani.
98. Na najikinga kwako, Mola wangu Mlezi, wasinikaribie.
99. Mpaka yanapo mfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu
Mlezi! Nirudishe.
100. Ili
nitende mema sasa badala ya yale niliyo yaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo
yeye tu. Na nyuma yao kipo kizuizi mpaka siku watapo fufuliwa.
|