51 - 77
51. Na tungeli taka tungeli peleka katika kila mji
Mwonyaji.
52. Basi usiwat'ii makafiri. Na pambana nao kwayo kwa
Jihadi kubwa.
53. Naye ndiye aliye zipeleka bahari mbili, hii tamu mno,
na hii ya chumvi chungu. Na akaweka baina yao kinga na kizuizi kizuiacho.
54. Naye ndiye aliye muumba mwanaadamu kutokana na maji,
akamjaalia kuwa na nasaba na ushemeji. Na Mola wako Mlezi ni Muweza.
55. Na wanayaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yasiyo wafaa
wala yasiyo wadhuru. Na kafiri daima ni msaidizi wa kumpinga Mola wake Mlezi.
56. Nasi hatukukutuma ila kuwa ni Mbashiri na Mwonyaji.
57. Sema: Sikukuombeni ujira juu yake; ila atakaye na
ashike njia iendayo kwa Mola wake Mlezi.
58. Na mtegemee Aliye Hai, ambaye hafi. Na umtukuze kwa
sifa zake. Na yatosha kwake kuwa yeye ni Mwenye khabari za dhambi za waja wake.
59. Ambaye ameziumba mbingu na ardhi, na viliomo ndani yake
kwa siku sita. Kisha akatawala juu ya A'rshi, Arrahman, Mwingi wa Rehema! Uliza
khabari zake kwa wamjuaye.
60. Na wanapo ambiwa: Msujudieni Arrahman! Wao husema: Ni nani Arrahman? Je! Tumsujudie unaye
tuamrisha wewe tu? Na huwazidishia chuki.
61. Ametukuka aliye zijaalia nyota mbinguni, na akajaalia
humo taa na mwezi unao ng'ara.
62. Naye ndiye aliye fanya usiku na mchana kufuatana kwa
nafuu ya anaye taka kukumbuka, au anaye taka kushukuru.
63. Na waja wa Arrahman Mwingi wa Rehema ni wale wanao
tembea ulimwenguni kwa staha, na wajinga wakiwasemeza hujibu: Salama!
64. Na wale wanao kesha kwa ajili ya Mola wao Mlezi kwa
kusujudu na kusimama.
65. Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu
ya Jahannamu. Hakika adhabu yake ikimpata mtu haimwachi.
66. Hakika hiyo ni kituo na makao mabaya.
67. Na wale ambao wanapo tumia hawatumii kwa fujo wala
hawafanyi ubakhili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo.
68. Na wale wasio mwomba mungu mwengine pamoja na Mwenyezi
Mungu, wala hawaui nafsi aliyo iharimisha Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwa haki,
wala hawazini - na atakaye fanya hayo atapata madhara,
69. Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo kwa
kufedheheka.
70. Isipo kuwa atakaye tubu, na akaamini, na akatenda
vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
71. Na aliye tubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu
kweli kweli kwa Mwenyezi Mungu.
72. Na wale ambao hawatoi ushahidi wa uwongo, na pindi
wapitapo penye upuuzi, hupita kwa hishima yao.
73. Na wale ambao wanapo kumbushwa Ishara za Mola wao Mlezi
hawajifanyi viziwi nazo, na vipofu.
74. Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake
zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamngu.
75. Hao ndio watakao lipwa makao ya juu kwa kuwa
walisubiri, na watakuta humo maamkio na salamu.
76. Wadumu humo - kituo na makao mazuri kabisa.
77. Sema: Mola wangu Mlezi asinge kujalini lau kuwa si
kuomba kwenu. Lakini nyinyi mmemkadhibisha. Basi adhabu lazima iwe.
|