1 - 50
1. T'aa Siin Miim. (T'.S.M.)
2. Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha.
3. Huenda labda ukajikera nafsi yako kwa kuwa hawawi
Waumini.
4. Tunge penda tungeli wateremshia kutoka mbinguni Ishara
zikanyenyekea shingo zao.
5. Wala hauwafikii ukumbusho mpya kutoka kwa Arrahman ila
wao hujitenga nao.
6. Kwa yakini wamekanusha; kwa hivyo zitakuja wafikia
khabari za yale waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha.
7. Je! Hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo, ya
kila namna nzuri?
8. Hakika katika
haya zipo Ishara. Lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.
9. Na hakika Mola
wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
10. Na Mola wako
Mlezi, alipo mwita Musa, akamwambia: Fika kwa watu madhaalimu,
11. Watu
wa Firauni. Hawaogopi?
12.
Akasema: Hakika mimi nachelea wasinikanushe.
13. Na
kifua changu kina dhiki, na ulimi wangu haukunjuki vyema. Basi mtumie ujumbe
Harun.
14. Na wao
wana kisasi juu yangu, kwa hivyo naogopa wasije kuniuwa.
15.
Akasema: Siyo hivyo kabisa! Nendeni na miujiza yetu. Hakika Sisi tu
pamoja nanyi, tunasikiliza.
16. Basi mfikieni Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni
Mitume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
17. Waachilie Wana wa Israili wende nasi.
18. (Firauni) akasema: Sisi hatukukulea wewe utotoni, na
ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi?
19. Na ukatenda kitendo chako ulicho tenda, nawe ukawa
miongoni mwa wasio na shukrani?
20. (Musa) akasema: Nilitenda hayo hapo nilipo kuwa
miongoni mwa wale walio potea.
21. Basi nikakukimbieni nilipo kuogopeni, tena Mola wangu
Mlezi akanitunukia hukumu, na akanijaalia niwe miongoni mwa Mitume.
22. Na hiyo ndiyo neema ya kunisumbulia, na wewe umewatia
utumwani Wana wa Israili?
23. Firauni akasema: Na nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu
wote?
24. Akasema: Ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na
viliomo baina yao, ikiwa nyinyi ni wenye yakini.
25. (Firauni) akawaambia walio mzunguka: Hamsikilizi?
26. (Musa) akasema: Ndiye Mola wenu Mlezi, na Mola Mlezi wa
baba zenu wa kwanza.
27. (Firauni) akasema: Hakika huyu Mtume wenu aliye tumwa
kwenu ni mwendawazimu.
28. (Musa) akasema: Ndiye Mola Mlezi wa Mashariki na
Magharibi na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi mnatia akilini.
29. (Firauni) akasema: Ukimfuata mungu mwengine asiye kuwa
mimi, basi bila ya shaka nitakufunga gerezani.
30. Akasema: Je!
Ijapo kuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi?
31. Akasema:
Kilete basi, kama wewe ni katika wasemao kweli.
32. Basi
akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka wa kuonekana dhaahiri.
33. Na akautoa
mkono wake, na mara ukawa mweupe kwa watazamao.
34. (Firauni)
akawaambia waheshimiwa walio mzunguka: Hakika huyu ni mchawi mtaalamu.
35. Anataka
kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake. Basi mna shauri gani?
36. Wakasema: Mpe muda yeye na nduguye na uwatume mijini
wapigao mbiu ya mgambo.
37. Wakuletee kila mchawi bingwa mtaalamu.
38. Basi wakakusanywa wachawi wakati na siku maalumu.
39. Na watu wakaambiwa: Je! Mtakusanyika?
40. Huenda tutawafuata wachawi wakiwa wao ndio watakao
shinda.
41. Basi walipo kuja wachawi wakamwambia Firauni: Je!
Tutapata ujira tukiwa sisi ndio tulio shinda?
42. Naam! Na
hakika mtakuwa katika watu wa mbele.
43. Musa akwaambia: Tupeni mnavyo taka kutupa.
44. Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu
za Firauni hakika sisi hapana shaka ni wenye kushinda.
45. Musa tena akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza
walivyo vizua.
46. Hapo wachawi walipinduka wakasujudu.
47. Wakasema: Tunamuamini Mola Mlezi wa walimwengu wote.
48. Mola Mlezi wa Musa na Harun.
49. (Firauni)
akasema: Je! Mmemuamini kabla sijakuruhusuni? Bila ya shaka yeye basi ndiye
mkubwa wenu aliye kufunzeni uchawi. Basi mtakuja jua! Nitakata mikono
yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakubandikeni misalabani nyote.
50. Wakasema: Haidhuru, kwani sisi ni wenye kurejea kwa
Mola wetu Mlezi.
|