1 - 50
1. T'aa Siin. (T'.S.), Hizi ni Aya za Qur'ani na Kitabu
kinacho bainisha;
2. Uwongofu na bishara kwa Waumini,
3. Ambao wanashika Sala, na wanatoa Zaka, na Akhera wana
yakini nayo.
4. Kwa hakika wale wasio iamini Akhera tumewapambia vitendo
vyao, kwa hivyo wanatangatanga ovyo.
5. Hao ndio watapata adhabu mbaya kabisa, na hao katika
Akhera ndio watapata khasara zaidi.
6. Na hakika wewe unafundishwa Qur'ani inayo tokana kwake
Mwenye hikima Mwenye kujua.
7. (Kumbuka) Musa alipo waambia ahali zake: Hakika nimeona
moto, nitakwenda nikuleteeni khabari, au nitakuleteeni kijinga kinacho waka ili
mpate kuota moto.
8. Basi alipo fika ilinadiwa: Amebarikiwa aliomo katika
moto huu na walioko pembezoni mwake. Na ametakasika Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi
wa walimwengu wote.
9. Ewe Musa! Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu, Mwenye
nguvu, Mwenye hikima.
10. Na itupe fimbo yako! Alipo iona ikitikisika kama nyoka,
aligeuka nyuma wala hakungoja. Ewe Musa! Usikhofu! Hakika hawakhofu mbele yangu
Mitume.
11. Lakini aliye dhulumu, kisha akabadilisha wema baada ya
ubaya, basi Mimi ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
12. Na ingiza mkono wako katika mfuko wako, utatoka mweupe
bila ya maradhi. Ni katika Ishara tisa za kumpelekea Firauni na kaumu yake.
Hakika hao walikuwa watu waovu.
13. Basi zilipo wafikia Ishara zetu hizo zenye kuonyesha,
wakasema: Huu ni uchawi dhaahiri.
14. Na wakazikataa kwa dhulma na kujivuna, na hali ya kuwa
nafsi zao zina yakini nazo. Basi angalia ulikuwaje mwisho wa mafisadi!
15. Na hakika tuliwapa Daudi na Sulaiman ilimu, na wakasema:
Alhamdu Lillahi, Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu aliye tufadhilisha
kuliko wengi katika waja wake Waumini.
16. Na Sulaiman alimrithi Daudi, na akasema: Enyi watu!
Tumefunzwa usemi wa ndege, na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo
dhaahiri.
17. Na alikusanyiwa Sulaiman majeshi yake ya majini, na
watu, na ndege; nayo yakapangwa kwa nidhamu.
18. Mpaka walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu,
alisema mdudu chungu mmoja: Enyi wadudu chungu! Ingieni majumbani mwenu,
asikupondeni Sulaiman na majeshi yake bila ya wao kutambua.
19. Basi (Sulaiman) akatabasamu akacheka kwa neno hili, na
akasema: Ee Mola wangu Mlezi! Nizindue niishukuru neema yako uliyo nineemesha
mimi na wazazi wangu, na nipate kutenda mema uyapendayo, na uniingize kwa
rehema yako katika waja wako wema.
20. Na akawakagua ndege, na akasema: Imekuwaje, mbona
simwoni Hud-hud, au amekuwa miongoni mwa walio ghibu?
21. Kwa yakini nitamuadhibu kwa adhabu kali, au
nitamchinja, au aniletee hoja ya kutosha.
22. Basi (Hud-hud) akakaa si mbali na akasema: Nimegundua
usilo gundua wewe, na ninakujia hivi kutoka nchi ya Sabai, na nakuletea khabari
za yakini.
23. Hakika mimi nimemkuta mwanamke anawatawala, naye
amepewa kila kitu, na anacho kiti cha enzi kikubwa.
24. Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya
Mwenyezi Mungu; na Shet'ani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia Njia. Kwa
hivyo hawakuongoka,
25. Na hawamsujudii Mwenyezi Mungu ambaye huyatoa yaliyo
fichikana katika mbingu na ardhi, na anayajua mnayo yaficha na mnayo yatangaza.
26. Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa
A'rshi tukufu..
27. Akasema (Sulaiman): Tutatazama umesema kweli au wewe ni
miongoni mwa waongo.
28. Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha waache
na utazame watarejesha nini.
29. (Malkia) akasema: Enyi wahishimiwa! Hakika nimeletewa
barua tukufu.
30. Imetoka kwa Sulaiman nayo ni: Kwa jina la Mwenyezi
Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
31. Msinifanyie jeuri, na fikeni kwangu nanyi mmekwisha kuwa
wenye kusalimu amri.
32. Akasema: Enyi wahishimiwa! Nipeni shauri katika jambo
langu hili, kwani mimi sikati shauri yoyote mpaka mhudhurie.
33. Wakasema: Sisi ni wenye nguvu na wakali kwa vita; na
amri iko kwako, basi tazama ni nini unaamrisha.
34. Akasema: Hakika wafalme wanapo uingia mji wanauharibu,
na wanawafanya wale watukufu wake kuwa wanyonge. Na hivyo ndivyo watendavyo.
35. Lakini
mimi nitawapelekea zawadi, nami nitangoja watakayo rudi nayo wajumbe.
36. Basi
alipo fika (mjumbe) kwa Sulaiman, alisema (Sulaiman): Hivyo ndio nyinyi
mnanisaidia kwa mali? Aliyo nipa Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kuliko aliyo
kupeni nyinyi. Lakini nyinyi mnafurahia hii zawadi yenu.
37. Rejea
kwao! Kwa yakini sisi tutawajia kwa majeshi wasio yaweza kuyakabili. Na hakika
tutawatoa humo na hali wao wamekuwa madhalili na wanyonge.
38.
Akasema: Enyi wahishimiwa! Ni nani kati yenu atakaye niletea kiti chake cha
enzi kabla hawajanijia nao wamekwisha salimu amri.
39.
Akasema: Afriti, katika majini: Mimi nitakuletea kabla hujainuka pahala pako
hapo. Na mimi kwa hakika nina nguvu na muaminifu.
40. Akasema
mwenye ilimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea kabla ya kupepesa jicho lako. Basi
alipo kiona kimewekwa mbele yake, akasema: Haya ni katika fadhila zake Mola
wangu Mlezi, ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru. Na mwenye kushukuru, kwa
hakika, anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake; na anaye kufuru, kwa hakika Mola
wangu Mlezi ni Mkwasi na Karimu.
41.
Akasema: Mgeuzieni kiti chake cha enzi hiki, tuone ataongoka, au atakuwa
miongoni mwa wasio ongoka.
42. Basi (Malkia) alipo fika akaambiwa: Je! Kiti chako cha
enzi ni kama hiki? Akasema: Kama kwamba ndicho hichi. (Sulaiman na watu wake
wakasema): Na sisi tumepewa ilimu kabla yake (Malkia), na tukawa Waislamu.
43. Na yale aliyo kuwa akiyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu
yalimzuilia. Hakika yeye (Malkia) alikuwa katika kaumu ya makafiri.
44. Akaambiwa: Liingie behewa la hili jumba. Alipo liona
alidhani ni maji, na akapandisha nguo mpaka kwenye miundi yake. (Sulaiman)
akasema: Hakika hilo ni behewa lilio sakafiwa kwa viyoo! Akasema (Malkia): Mola
wangu Mlezi! Mimi nimejidhulumu nafsi yangu, na sasa nanyenyekea pamoja na
Sulaiman kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.
45. Na kwa kina Thamud tulimtuma ndugu yao Saleh kuwaambia:
Muabuduni Mwenyezi Mungu. Basi wakawa makundi mawili yanayo gombana.
46. Akasema: Enyi watu wangu! Kwa nini mnauhimiza uwovu
kabla ya wema? Kwa nini hamuombi msamaha kwa Mwenyezi Mungu ili mrehemewe?
47. Wakasema: Tuna kisirani nawe na wale walio pamoja nawe.
Yeye akasema: Uaguzi wa ukorofi wenu uko kwa Mwenyezi Mungu; lakini nyinyi ni
watu mnao jaribiwa.
48. Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika
nchi wala hawafanyi la maslaha.
49. Wakasema: Apishaneni kwa Mwenyezi Mungu tutamshambulia
usiku yeye na ahali zake; kisha tutamwambia mrithi wake: Sisi hatukuona
maangamizo ya watu wake, na sisi bila ya shaka tunasema kweli.
50. Basi wakapanga mipango yao, na Sisi tukapanga mipango
yetu, na wao hawatambui.
|