51 - 93
51. Basi angalia ulivyo kuwa mwisho wa mipango yao, ya
kwamba tuliwaangamiza wao pamoja na watu wao wote.
52. Basi hizo nyumba zao ni tupu kwa sababu ya walivyo
dhulumu. Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara kwa watu wanao jua.
53. Na tukawaokoa wale walio amini na walio kuwa
wanamchamngu.
54. Na Lut'i alipo waambia watu wake: Je! Mnafanya uchafu
nanyi mnaona?
55. Hivyo nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio badala
ya wanawake? Hakika nyinyi ni watu mnao fanya ujinga kabisa!
56. Basi haikuwa jawabu ya watu wake ila ni kusema:
Wafukuzeni wafwasi wa Lut'i katika mji wenu. Hao ni watu wanao jitia usafi.
57. Basi tukamwokoa yeye na ahali zake, isipo kuwa mkewe;
tukamkadiria katika walio baki nyuma.
58. Na tukawanyeshea mvua. Ni ovu kweli kweli hiyo mvua ya
walio kwisha onywa.
59. Sema: Alhamdu Lillahi! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi
Mungu! Na amani ishuke juu ya waja wake alio wateuwa. Je! Mwenyezi Mungu ni
bora, au wale wanao washirikisha naye?
60. AU NANI yule aliye ziumba mbingu na ardhi, na
akakuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwa hayo tukaziotesha bustani zenye
kupendeza? Nyinyi hamna uwezo wa kuiotesha miti yake. Je! Yupo mungu pamoja na
Mwenyezi Mungu? Bali hao ni watu walio potoka.
61. Au nani yule aliye ifanya ardhi mahali pa kutua, na
akajaalia ndani yake mito, na akaweka milima? Na akaweka baina ya bahari mbili
kiziwizi? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Bali wengi wao hawajui.
62. Au nani yule anaye mjibu mwenye shida pale anapo
mwomba, na akaiondoa dhiki, na akakufanyeni warithi wa ardhi? Je! Yupo mungu
pamoja na Mwenyezi Mungu? Ni machache mnayo yazingatia.
63. Au nani yule anaye kuongoeni katika giza la bara na
bahari, na akazipeleka pepo kuleta bishara kabla ya rehema zake? Je! Yupo mungu
pamoja na Mwenyezi Mungu? Ametukuka Mwenyezi Mungu juu ya wanao washirikisha
naye.
64. Au nani anaye uanzisha uumbaji, kisha akaurejesha? Na
nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Je! Yupo mungu pamoja na
Mwenyezi Mungu? Sema: Leteni hoja zenu kama nyinyi ni wasema kweli.
65. Sema: Hapana katika mbingu na ardhi ajuaye ya ghaibu
isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Wala wao hawajui lini watafufuliwa.
66. Kwani huo ujuzi wao umefikilia kuijua Akhera? Bali wao
wamo katika shaka nayo tu, bali wao ni vipofu nayo.
67. Na wakasema walio kufuru: Tutapo kuwa mchanga, sisi na
baba zetu, hivyo kweli tutakuja tolewa?
68. Haya haya tuliahidiwa sisi na baba zetu zamani.
Hayakuwa haya ila ni hadithi za uwongo za watu wa kale.
69. Sema: Nendeni katika ardhi, na tazameni ulikuwaje
mwisho wa wakosefu.
70. Wala usiwahuzunukie wala usiwe katika dhiki kwa sababu
ya hila zao wanazo zifanya.
71. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa mnasema
kweli?
72. Sema: Asaa ni karibu kukufikieni sehemu ya yale mnayo
yahimiza.
73. Na hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye fadhila kwa watu,
lakini wengi wao hawashukuru.
74. Na hakika Mola wako Mlezi anayajua yanayo ficha vifua
vyao na wanayo yatangaza.
75. Na hakuna siri katika mbingu na ardhi ila imo katika
Kitabu kinacho bainisha.
76. Hakika Qur'ani hii inawasimulia Wana wa Israili mengi
wanayo khitalifiana nayo.
77. Nayo hakika ni Uwongofu na Rehema kwa Waumini.
78. Hakika Mola wako Mlezi atawahukumu kwa hukumu yake,
naye ni Mwenye nguvu Mjuzi.
79. Basi mtegemee Mweneyezi Mungu; hakika wewe uko juu ya
Haki iliyo wazi.
80. Kwa hakika wewe huwezi kuwafanya maiti wasikie, wala
kuwafanya viziwi wasikie wito, wanapo kwisha geuka kwenda zao.
81. Wala huwezi kuwaongoa vipofu waache upotovu wao. Huwezi
kuwafanya wasikie isipo kuwa wenye kuziamini Ishara zetu; na hao ndio wat'iifu.
82. Na itapo waangukia kauli juu yao, tutawatolea mnyama
katika ardhi atakaye wasemeza, ya kuwa watu walikuwa hawana na yakini na Ishara
zetu.
83. Na Siku tutapo kusanya kutoka kila umma kundi katika
wanao kadhibisha Ishara zetu, nao watagawanywa mafungu mafungu.
84. Hata watakapo fika, atasema (Mwenyezi Mungu): Je!
Nyinyi si mlizikanusha Ishara zangu pasipo kuzijua vyema? Au mlikuwa mkifanya
nini?
85. Na kauli itawaangukia juu yao kwa vile walivyo dhulumu.
Basi hao hawatasema lolote.
86. Je! Hawaoni kwamba sisi tumeufanya usiku ili watulie,
na mchana wa kuangaza. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao amini.
87. Na Siku litapo pulizwa baragumu, watahangaika waliomo
mbinguni na katika ardhi, ila amtakaye Mwenyezi Mungu. Na wote watamfikia nao ni wanyonge.
88. Na unaiona milima unaidhunia imetulia; nayo inakwenda
kama mwendo wa mawingu. Huo ndio ufundi wa Mwenyezi Mungu aliye tengeneza
vilivyo kila kitu. Hakika Yeye anazo khabari za yote myatendayo.
89. Watakao kuja na mema, watapata bora kuliko hayo. Nao
watasalimika na mahangaiko ya Siku hiyo.
90. Na watakao kuja na uovu, basi zitasunukishwa nyuso zao
Motoni. Je! Kwani mnalipwa isipo kuwa mliyo kuwa mkiyatenda?
91. Ama mimi nimeamrishwa nimuabudu Mola Mlezi wa mji huu
aliye ufanya ni mtakatifu; na ni vyake Yeye tu vitu vyote. Na nimeamrishwa niwe
miongoni mwa Waislamu, wenye kunyenyekea.
92. Na niisome Qur'ani. Na mwenye kuongoka, basi ameongoka
kwa faida ya nafsi yake; na aliye potea - basi sema: Hakika mimi ni miongoni
mwa waonyaji.
93. Na sema: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za
Mwenyezi Mungu. Yeye atakuonyesheni Ishara zake, na mtazijua. Na Mola wako
Mlezi si mwenye kughafilika na myatendayo.
|