51 - 88
51. Na sasa kwa yakini tumewafikishia Neno ili wapate
kukumbuka.
52. Wale tulio wapa Kitabu kabla yake wanakiamini hiki.
53. Na wanapo somewa wanasema: Tunaiamini. Hakika hii ni Haki
inayo toka kwa Mola wetu Mlezi. Hakika sisi kabla yake tulikuwa ni Waislamu,
tulio nyenyekea.
54. Basi hao watapewa ujira wao mara mbili kwa walivyo vumilia,
na wakaondoa ubaya kwa wema, na wakatoa katika tuliyo waruzuku.
55. Na wanapo sikia upuuzi hujitenga nao na husema: Sisi
tuna vitendo vyetu, na nyinyi mna vitendo vyenu. Salamun Alaikum, Amani juu
yenu! Sisi hatutaki kujibizana na wajinga.
56. Kwa hakika wewe humwongoi umpendaye, lakini Mwenyezi
Mungu humwongoa amtakaye. Na Yeye ndiye anawajua zaidi waongokao.
57. Na wakasema: Tukiufuata uwongofu huu pamoja nawe
tutanyakuliwa kutoka nchi yetu. Je! Kwani Sisi hatukuwaweka imara katika pahala
patakatifu, penye amani, ambapo huletewa matunda ya kila aina kuwa ni riziki
itokayo kwetu? Lakini wengi
wao hawajui.
58. Na
miji mingapi iliyo jifakharisha tumeiangamiza! Na hayo maskani yao hayakukaliwa
tena baada yao, ila kwa uchache tu. Na Sisi ndio tumekuwa warithi wao.
59. Na Mola wako Mlezi haangamizi miji mpaka ampeleke Mtume
katika miji yake mikuu awasomee Ishara zetu. Wala hatuiangamizi miji mpaka watu
wake wawe madhaalimu.
60. Na chochote mlicho pewa ni matumizi ya maisha ya dunia
na pambo lake. Na yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ndio bora na yatakayo baki zaidi.
Basi je, hamfahamu?
61. Je! Yule
tuliye muahidi ahadi nzuri, tena naye akayapata, ni kama tuliye mstarehesha kwa
starehe za maisha ya duniani, na kisha Siku ya Kiyama akawa miongoni mwa wanao
hudhurishwa?
62. Na siku
atakapo waita na akasema: Wako wapi mlio kuwa mkidai kuwa ni washirika wangu?
63. Watasema
wale iliyo thibiti juu yao kauli: Mola wetu Mlezi! Hawa ndio tulio
wapoteza. Tuliwapoteza kama tulivyo potea sisi. Tunajitenga nao mbele yako.
Hawakuwa wakituabudu sisi.
64. Na itasemwa: Waiteni hao miungu wa kishirikina wenu!
Basi watawaita, lakini hawatawaitikia, na wataiona adhabu; laiti wangeli kuwa
wameongoka!
65. Na siku atapo waita na akasema: Mliwajibu nini Mitume?
66. Basi zitawapotea khabari siku hiyo, nao hawataulizana.
67. Ama mwenye kutubu na akaamini na akatenda mema, huyo
atakuwa miongoni mwa wenye kufanikiwa.
68. Na Mola wako Mlezi huumba na huteuwa atakavyo. Viumbe
hawana khiari. Mwenyezi Mungu ametukuka na ametakasika na hao wanao
washirikisha naye.
69. Na Mola wako Mlezi anayajua yaliyo ficha vifua vyao, na
wanayo yatangaza.
70. Naye ni Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa
Yeye. Sifa zote njema ni zake Yeye, mwanzo na mwisho. Na hukumu ni yake Yeye. Na kwake Yeye mtarejeshwa.
71 Sema:
Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya usiku umekukalieni moja kwa moja mpaka
Siku ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu atakaye kuleteeni
mwangaza? Basi je, hamsikii?
72. Sema:
Mwaonaje, Mwenyezi Mungu angeli ufanya mchana umekukalieni moja kwa moja mpaka Siku
ya Kiyama, mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu ataye kuleteeni usiku
mkapumzika humo? Basi je, hamwoni?
73. Na ni katika
rehema zake amekufanyieni usiku na mchana mpate kupumzika humo na mtafute
fadhila zake, na ili mpate kushukuru.
74. Na siku
atakapo waita na akasema: Wako wapi hao mlio kuwa mkidai kuwa ni washirika
wangu?
75. Na tutatoa shahidi katika kila umma, na tutasema:
Leteni hoja zenu! Hapo watajua kwamba hakika kweli ni ya Mwenyezi Mungu, na
yatawapotea yale waliyo kuwa wakiyazua.
76. Hakika Qaruni alikuwa katika watu wa Musa, lakini
aliwafanyia dhulma. Na tulimpa khazina ambazo funguo zake zinawatopeza watu
wenye nguvu kuzichukua. Walipo mwambia watu wake: Usijigambe! Hakika Mwenyezi
Mungu hawapendi wanao jigamba.
77. Na utafute, kwa aliyo kupa Mwenyezi Mungu, makaazi ya
Akhera. Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyezi Mungu
alivyo kufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika
Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.
78. Akasema: Kwa hakika nimepewa haya kwa sababu ya ilimu
niliyo nayo. Je! Hakujua kwamba Mwenyezi Mungu kesha waangamiza, katika vizazi
vya walio kabla yake, watu walio kuwa wenye ngubvu zaidi kuliko yeye, na wenye
makundi makubwa zaidi kuliko yake. Na wakosefu hawataulizwa khabari ya dhambi
zao.
79. Basi akawatokea watu wake katika pambo lake. Wakasema
wale walio kuwa wanataka maisha ya duniani: Laiti tungeli kuwa tunayo kama
aliyo pewa Qaruni! Hakika yeye ni mwenye bahati kubwa.
80. Na wakasema wale walio pewa ilimu: Ole wenu! Malipo ya
Mwenyezi Mungu ni bora kwa mwenye kuamini na akatenda mema. Wala hawatapewa
hayo isipo kuwa wenye subira.
81. Basi tukamdidimiza yeye na nyumba yake katika ardhi;
wala halikuwepo kundi lolote la kumnusuru kwa Mwenyezi Mungu, wala hakuwa
miongoni mwa wanao jitetea.
82. Na wale walio tamani kuwa pahala pake jana, wakawa
wanasema: Kumbe Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye katika waja wake, na
humdhikisha amtakaye. Ingeli kuwa Mwenyezi Mungu hakutufanyia hisani angeli
tudidimiza. Kumbe makafiri hawafanikiwi!
83. Hayo ndiyo makaazi ya Akhera, tumewafanyia wale wasio
taka kujitukuza duniani wala ufisadi. Na mwisho mwema ni wa wachamngu.
84. Atakaye tenda wema atapata malipo bora kuliko huo wema
alio utenda. Na atakaye tenda uovu, hawalipwi watendao uovu ila waliyo kuwa
wakiyatenda.
85. Hakika aliye kulazimisha kuifuata Qur'ani hapana shaka
atakurudisha pahala pa marejeo. Sema: Mola wangu Mlezi ndiye anaye mjua zaidi
mwenye kuja na uwongofu, na nani aliyomo katika upotofu ulio dhaahiri.
86. Nawe hukuwa unataraji kuletewa Kitabu; lakini ni rehema
tu ya Mola wako Mlezi. Basi usiwe msaidizi wa makafiri.
87. Wala wasikuzuie kuzifuata Aya za Mwenyezi Mungu baada
ya kuteremshiwa wewe. Na lingania kwa Mola wako Mlezi, wala usiwe miongoni mwa
washirikina.
88. Wala usimwombe pamoja na Mwenyezi Mungu mungu
mwenginewe. Hapana mungu ila Yeye. Kila kitu kitaangamia isipo kuwa Yeye.
Hukumu iko kwake, na kwake mtarejezwa.
|