34. SURAT SABAA
(Imeteremka
Makka)
Sura hii imeanzia kwa
kumfanya Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kustahiki kusifiwa na kuhimidiwa
kwa alivyo waneemesha waja wake. Kwani vyote vilioko mbinguni na katika ardhi
ni vyake Yeye kwa kuviumba na kuvimiliki. Na Sura inaeleza porojo la makafiri
juu ya Saa ya Kiyama, na kukanya kwao kufufuliwa, na kumsingizia Mtume kuwa ni
mwongo na mwendawazimu. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu anawarejesha kwenye dalili
za uweza wake, na anawahadharisha kuwa atawateremshia kama alivyo wateremshia
walio kama wao, ikawameza ardhi, au vikawaangukia vipande kutoka mbinguni. Na
anawakumbusha anavyo wafanyia vipenzi vyake. Kama alivyo mlainishia chuma
Daudi, na akamtawalisha Sulaiman na akawafanya majini wamtumikie, wakafanya
kama alivyo taka, kama mihrabu na masanamu. Na Daudi na Suleiman waliishukuru
neema, na wachache tu katika waja wa Mwenyezi Mungu wanao shukuru. Hayo
yakafuatia maelezo ya neema aliyo waneemesha Mwenyezi Mungu watu wa Sabaa, nao
wasishukuru. Hao walikuwa na bustani mbili, ya kulia na kushoto. Miji
yao ilikuwa imekaribiana, na wakisafiri baina yao kwa amani. Neema ikawatia
kiburi, wakataka safari ziwe ndefu zaidi. Mwenyezi Mungu akawalipa anavyo
walipa wanao zikataa neema zake. Nao wakatimiza aliyo fikiri Iblisi na
wakamfuata. Na yeye hakuwa na madaraka juu yao, lakini hayo yalikuwa ni mtihani
tu wapate kutengana baina ya wanao iamini Akhera na wenye shaka nayo. Kisha
Sura ikaingia kuwaeleza hao wanao wafanya kuwa ni miungu kwamba kwa hakika
hawana lolote wawezalo. Na inakumbusha Sura kuwa kila mtu ana jukumu la makosa
ayatendayo. Na ikathibitisha Ujumbe wote wa Mtume. Na ikataja kuwa washirikina
wanaiona Siku ya Kiyama inachelewa. Na hiyo ina wakati wake maalumu.
Na Sura inasimulia kauli ya makafiri katika Qur'ani, na majadiliano baina ya
wakuu na wanyonge, na ikaweka mipaka ya kujifakhari kwa mali na wana, na kwamba
hayo mali hayamkaribishi mtu kwa Mwenyezi Mungu ila kwa kadri ya manufaa kwa
watu yanayo patikana kutokana na mali hayo. Kwani hayo mali ni milki yake
Mwenyezi Mungu. Na Yeye humkunjulia riziki amtakaye na humdhikisha. Na inawekwa
wazi sura ya washirikina. Kwani wao walimwabia Mtume wao kwamba yeye anataka
kuwazuilia wasiabudu miungu walio kuwa wakiiabudu baba zao. Na wakaisema
Qur'ani aliyo teremshiwa kuwa ni uzushi ulio tungwa, na uchawi dhaahiri! Na pia
walidai kuwa hawakupewa Vitabu kabla yake, wala hakutumwa Mtume kabla yake. Na
hali hakika tuliwatumia walio kabla yao wanao wajua nguvu zao, na utukufu wao,
na khabari zao. Na walipo kuwa hawakuitikia Wito tuliwashika kwa kuwaadhibu. Na
Mtume s.a.w. anaamrishwa aeleze wazi ujumbe wake muhimu kwao. Na hili ni
kumbusho bila ya kahari. Na wanaamrishwa wamtazame huyu mwenzao. Hana wazimu,
wala hataki mali, na Wito wake kwa watu wafuate Haki ni kwa Ufunuo (Wahyi) unao
tokana na Mwenyezi Mungu Mtukufu ili wapate amani. Na itakapo kuja Saa ya
Kiyama watafazaika, na watakuwa hawana pa kukimbilia, na watakamatwa pahala
karibu. Hapo tena ndio watasema: Tumeamini! Yafaa nini tena hapo Imani nao
walikwisha kataa kabla yake. Watazuiwa baina yao na wanacho kitamani, kama
walivyo fanyiwa walio kuwa mfano wao. Wao wote walikuwa na shaka tupu katika
mambo ya Dini.
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, ambaye ni vyake
vyote viliomo mbnguni na katika ardhi. Na sifa ni zake Yeye katika Akhera. Naye
ni Mwenye hikima, Mwenye khabari.
2. Anajua yanayo ingia katika ardhi na yanayo toka humo, na
yanayo teremka kutoka mbinguni, na yanayo panda huko. Na Yeye ni Mwenye
kurehemu, Mwenye kusamehe.
3. Na walisema walio kufuru: Haitatufikia Saa (ya Kiyama).
Sema: Kwani? Hapana shaka itakufikieni, naapa kwa haki ya Mola wangu Mlezi,
Mwenye kujua ya ghaibu! Hapana kinacho fichikana kwake hata chenye uzito wa
chembe tu, si katika mbingu wala katika ardhi, wala kilicho kidogo kuliko
hivyo, wala kikubwa zaidi; ila vyote hivyo vimo katika Kitabu chake chenye
kubainisha.
4. Ili awalipe walio amini na wakatenda mema. Hao watapata
msamaha na riziki ya ukarimu.
5. Na wale walio jitahidi kuzipinga Ishara zetu wakaona
watashinda, hao watapata adhabu mbaya yenye uchungu.
6. Na walio pewa ilimu wanaona ya kuwa ulio teremshiwa
kutoka kwa Mola wako Mlezi ni haki, nayo huongoa kwendea njia ya Mwenye nguvu,
Mwenye kusifiwa.
7. Na walio kufuru walisema: Je! Tukujuulisheni mtu anaye
kuambieni kwamba mtakapo chambuliwa mapande mapande mtakuwa katika umbo jipya?
8. Ama amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo, au ana wazimu. Bali
wasio amini Akhera wamo adhabuni na upotofu wa mbali kabisa.
9. Kwani hawaoni yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao ya
mbingu na ardhi? Tungeli penda tungeli wadidimiza ndani ya ardhi, au tungeli
wateremshia juu yao vipande vya mbingu. Hakika katika haya zipo Ishara kwa kila
mja aliye tubia.
10. Na tulimpa Daudi fadhila kutoka kwetu, (tukasema): Enyi
milima! Karirini kumtakasa Mwenyezi Mungu pamoja naye! Na ndege pia. Na
tukamlainishia chuma.
11. (Tukamwambia:) Tengeneza nguo za chuma pana, na kadiria
sawa katika kuunganisha. Na tendeni mema. Hakika Mimi nayaona vyema mnayo
yatenda.
12. Na Suleiman tuliufanya upepo umtumikie. Safari yake ya
asubuhi ni mwendo wa mwezi mmoja, na safari yake ya jioni ni mwendo wa mwezi
mmoja. Na tukamyayushia chemchem ya shaba. Na katika majini walikuwako walio
kuwa wakifanya kazi mbele yake kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na kila anaye
jitenga na amri yetu katika wao, tunamwonjesha adhabu ya Moto unao waka.
13. Walikuwa wakimfanyia alipendalo, kama mihrabu, na
masanamu, na madeste makubwa kama mahodhi, na masufuria makubwa yasiyo ondolewa
mahala pake. Enyi watu wa
Daudi! Fanyeni kazi kwa kushukuru. Ni wachache katika waja wangu wanao shukuru.
14. Na tulipo
mhukumia kufa, hapana aliye wajuulisha kufa kwake ila mnyama wa ardhi aliye
kula fimbo yake. Na alipo anguka majini walitambua lau kuwa wangeli jua ya
ghaibu wasingeli kaa katika adhabu hiyo ya kufedhehesha.
15. Hakika
ilikuwapo Ishara kwa (watu wa nchi ya) Sabaa katika maskani yao - bustani
mbili, kulia na kushoto. Kuleni katika riziki ya Mwenyezi Mungu, na mumshukuru.
Mji mzuri na Mola Mlezi aliye Msamehevu.
16. Lakini wakaacha. Tukawapelekea mafuriko makubwa, na
tukawabadilishia badala ya bustani zao hizo kwa bustani nyengine zenye matunda makali
machungu, na mivinje, na kidogo katika miti ya kunazi.
17. Hayo tuliwalipa kwa sababu ya walivyo kufuru. Nasi
kwani tunamuadhibu isipo kuwa anaye kufuru?
18. Na baina yao na miji mingine tuliyo ibariki tuliweka
miji iliyo dhaahiri, na tukaweka humo vituo vya safari. Tukawaambia: Nendeni
humo usiku na mchana kwa amani.
19. Lakini wakasema: Mola wetu Mlezi! Weka mwendo mrefu
baina ya safari zetu. Na wakazidhulumu nafsi zao. Basi tukawafanya ni
masimulizi tu, na tukawatawanya tawanya. Hakika katika hayo bila ya shaka zimo
Ishara kwa kila mwenye kusubiri sana na akashukuru.
20. Na bila ya shaka Iblisi alihakikisha ile dhana yake juu
yao. Nao walimfuata, isipo kuwa kundi la Waumini.
21. Na yeye hakuwa na mamlaka yoyote juu yao, ila kwa
sababu ya kuwajaribu tujue nani mwenye kuamini Akhera, na nani anaye tilia
shaka. Na Mola wako Mlezi ni Mwenye kuhifadhi kila kitu.
22. Sema: Waite mnao wadaia kuwa ni badala ya Mwenyezi
Mungu. Hawamiliki hata uzito wa chembe hichi katika mbingu wala ardhi. Wala hawana ushirika wowote humo. Wala
Yeye hana msaidizi miongoni mwao.
23. Wala uombezi mbele yake hautafaa kitu, isipo kuwa kwa
aliye mpa idhini. Hata itapo ondolewa khofu kwenye nyoyo zao watasema: Mola
wenu Mlezi kasema nini? Watasema: Yaliyo kweli! Na Yeye ndiye Aliye juu,
Mkubwa.
24. Sema: Ni nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni na
kwenye ardhi? Sema: Mwenyezi Mungu! Na hakika sisi au nyinyi bila ya shaka tuko
kwenye uwongofu au upotofu ulio wazi.
25. Sema: Nyinyi hamtaulizwa kwa makosa tuliyo yafanya,
wala sisi hatutaulizwa kwa mnayo yatenda nyinyi.
26. Sema: Mola wetu Mlezi atatukusanya, kisha atatuhukumu
kwa haki; na Yeye ndiye Hakimu Mwenye kujua.
27. Sema: Nionyesheni mlio waunganisha naye kuwa washirika.
Hasha! Bali Yeye ndiye Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
28. Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mbashiri, na
mwonyaji. Lakini watu wengi hawajui.
29. Na wanasema: Ahadi hii itakuwa lini, ikiwa nyinyi
mnasema kweli?
30. Sema: Nyinyi mnayo miadi ya Siku ambayo hamtaakhirika
nayo kwa saa moja, wala hamtaitangulia.
31. Na walisema walio kufuru: Hatutaiamini Qur'ani hii,
wala yaliyo kuwa kabla yake. Na ungeli waona madhaalimu watapo simamishwa mbele
ya Mola wao Mlezi, wakirudishiana maneno wao kwa wao! Wanyonge wakiwaambia
walio takabari: Lau kuwa si nyinyi, bila ya shaka tungeli kuwa Waumini sisi.
32. Walio takabari watawaambia wanyonge: Kwani sisi ndio
tulio kuzuieni na uwongofu baada ya kukujieni? Bali nyinyi wenyewe ni wakosefu.
33. Na wanyonge wakawaambia walio takabari: Bali ni vitimbi
vyenu vya usiku na mchana, mlipo kuwa mkituamrisha tumkufuru Mwenyezi Mungu, na
tumfanyie washirika. Nao wataficha majuto watakapo iona adhabu. Na tutaweka
makongwa shingoni mwao walio kufuru. Kwani wanalipwa ila kwa waliyo kuwa
wakiyatenda?
34. Na hatukumtuma mwonyaji yeyote kwenye mji, ila walisema
walio jidekeza kwa starehe zao wa mji huo: Hakika sisi tunayakataa hayo mliyo
tumwa nayo.
35. Na wakasema: Sisi tuna mali mengi zaidi na watoto, wala
sisi hatutaadhibiwa.
36. Sema: Hakika Mola wangu Mlezi humkunjulia riziki na
humdhikisha amtakaye. Lakini watu wengi hawajui.
37. Na si mali yenu wala watoto wenu watakao kukaribisheni
kwetu muwe karibu, isipo kuwa aliye amini na akatenda mema. Hao basi watapata
malipo mardufu kwa walio yafanya. Nao watakuwa salama katika maghorofa.
38. Na wanao jitahidi kuzipinga Ishara zetu, wakaona
watashinda, hao watahudhurishwa kwenye adhabu.
39. Sema: Kwa hakika Mola wangu Mlezi humkunjulia riziki na
humdhikisha amtakaye katika waja wake. Na chochote mtakacho kitoa Yeye atakilipa. Naye ni Mbora wa wanao
ruzuku.
40. Na
siku atakayo wakusanya wote, kisha atawaambia Malaika: Je! Hawa walikuwa
wakikuabuduni?
41.
Waseme: Subhanak, Umetakasika. Wewe ndiye kipenzi chetu si hao. Bali wao
walikuwa wakiwaabudu majini; wengi wao wakiwaamini hao.
42. Hii
leo hataweza yeyote kumletea nafuu wala madhara mwenzie. Na tutawaambia walio
dhulumu: Onjeni adhabu ya Moto mlio kuwa mkiukanusha.
43. Na
wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi wanasema: Huyu si chochote ila ni mtu anaye
taka kukuzuieni na waliyo kuwa wakiabudu baba zenu. Na wakasema: Haya si
chochote ila ni uwongo ulio zuliwa. Na walio kufuru waliiambia Haki ilipo
wajia: Haya si chochote ila ni uchawi ulio dhaahiri.
44. Wala hatukuwapa Vitabu wavisome, wala hatukuwatumia
Mwonyaji kabla yako wewe.
45. Na walikadhibisha walio kuwa kabla yao. Na
hawakufikilia hata sehemu moja katika kumi ya tulivyo wapa hao. Nao
waliwakadhibisha Mitume wangu. Basi kuangamiza kwangu kulikuwa namna gani!
46. Sema: Mimi nakunasihini kwa jambo moja tu - ya kwamba
msimame kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wawili-wawili na mmoja-mmoja; kisha
mfikiri. Mwenzenu huyu hana wazimu. Yeye si chochote ila ni Mwonyaji kwenu
kabla ya kufika adhabu kali.
47. Sema: Ujira nilio kuombeni ni wenu nyinyi. Sina ujira
ila kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye ni Shahidi juu ya kila kitu.
48. Sema: Hakika Mola wangu Mlezi anaondoa upotovu kwa
Haki. Yeye ndiye Mwenye kujua vyema yaliyo ghaibu.
49. Sema: Kweli imefika, na uwongo haujitokezi, wala
haurudi.
50. Sema: Ikiwa mimi nimepotea, basi nimepotea kwa kudhuru
nafsi yangu mwenyewe. Na ikiwa nimeongoka, basi ni kwa sababu ya kunifunulia
Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Aliye karibu.
51. Na lau ungeli ona watapo babaika, basi hapana pa
kukimbilia! Na watakamatwa mahala pa karibu.
52. Na watasema: Tunaiamini! Lakini wataipata wapi kutoka
huko mahala mbali?
53. Na hapo kabla yake waliikataa, na wakiyatupilia mbali
maneno ya ghaibu kutoka mahali mbali.
54. Na watatiliwa kizuizi baina yao na hayo wanayo
yatamani, kama walivyo fanyiwa wenzao zamani. Hakika hao walikuwa na shaka ya
kutia wasiwasi.
|