Table of Contents | Words: Alphabetical - Frequency - Inverse - Length - Statistics | Help | IntraText Library

Qu'rani

IntraText CT - Text

  • 39. SURAT AZZUMAR
Previous - Next

Click here to show the links to concordance

39. SURAT AZZUMAR

(Imeteremka Makka)

Sura hii ni ya Makka, yasemekana, isipo kuwa Aya 52, 53 na 54. Na Aya zake ni 75. Imefunguliwa Sura hii kwa kuisifu Qur'ani, kisha kwa kuwataka watu wamsafie ibada Mwenyezi Mungu peke yake, na inawarudi wale wanao sema kwamba Mwenyezi ana mwana. Kisha Aya zikaeleza uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kuumba mbingu na ardhi, na kumuumba mtu; na kwamba watu wakimkanya Yeye basi Yeye si mwenye kuwahitajia wao, na kwamba wakimshukuru, Yeye huwa radhi nao, na wala hawaridhii wakimkanusha. Na kadhaalika Sura hii imeeleza khulka ya binaadamu katika hali mbili, yaani anapo patwa na shida humwomba Mola wake na akarejea kwake, na akimneemesha mara husahau yale aliyo kuwa akiyaomba kabla yake.
Kisha Sura ikaunganisha makhusiano baina ya anaye tahadhari na Akhera na akataraji rehema ya Mola wake Mlezi, na wale wanao muasi; na malipo aliyo waandalia hawa na wale kwa Siku ya Kiyama. Kisha inawakumbusha neema za Mwenyezi Mungu kwa kuwateremshia maji, na kwamba Yeye huihuisha ardhi baada ya kufa kwake, na huotesha mimea ambayo inapitia viwango mbali mbali. Na katika hayo yapo makumbusho kwa wenye akili.
Kisha Sura inarejea kusimulia khabari ya Qur'ani na athari zake kwa wanao mwogopa Mola wao Mlezi. Na kwamba Mwenyezi Mungu kawapigia mifano ndani yake ili wazingatie, hiyo ni Qur'ani isio na pogo ili wamchemungu. Kisha Sura ikalinganisha baina ya mja mshirikina na mja mwenye kumtakasisha Mwenyezi Mungu kwa ibada, na kuwa hakika hawa wawili hawawi sawa. Na kuwa hakika mauti ndio mwisho wa wote, na baadae mbele ya Mola wao Mlezi ndio watazozana.
Kisha Sura ikabainisha mwisho wa mwenye kumzulia uwongo Mwenyezi Mungu na akaikadhibisha kweli, na mwisho wa wasemao kauli ya kweli, wenye kusadiki waliyo teremshiwa. Na hakika hao washirikina ukiwauliza: Nani aliye umba mbingu na ardhi? Hapana shaka watasema: Mwenyezi Mungu. Lakini nao juu ya hayo wanawaabudu wasio walinda na madhara pindi Mwenyezi Mungu akitaka kuwadhuru, wala hawaizuii rehema ya Mwenyezi Mungu pindi akiwatakia rehema. Tena Sura hii inathibitisha kwamba Kitabu hichi kimeteremshwa kwa haki. Basi mwenye kuongoka ni kwa maslaha ya nafsi yake, na mwenye kupotea dhambi zake ni juu ya nafsi yake. Na hakika Mtume s.a.w. si mwakilishi juu yao.
Kisha Sura inarejea kuwakumbusha kufa na kufufuliwa, na kwamba wale miungu ya kishirikina (ya kipagani) walio wafuata badala ya Mwenyezi Mungu hawawafai kitu, hata kuwaombea. Kwani hakika uombezi wote uko kwa Mwenyezi Mungu.
Na yalipo kithiri maneno juu ya adhabu chungu walio andaliwa waasi na waharibifu - na labda haya ndiyo yaliyo zipelekea nyoyo zao kukata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu - amewafungulia mlango wa kutumai rehema yake kwa kusema: "Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Msamehevu Mwenye kurehemu." Na akawataka warejee kwake kabla haijawajia adhabu kwa ghafla na wao hawatambui: "Na Siku ya Kiyama utawaona wale walio msingizia uwongo Mwenyezi Mungu nyuso zao zimesawijika. Je! Si katika Jahannamu makaazi ya wale wanao takabari?" Na wenye kuchamngu halitawagusa ovu, na wala hawatahuzunika. Na Sura ikakhitimisha kwa kusimulia khabari za Siku ya Mwisho, tangu mwanzo wake litapo pulizwa barugumu wakapigwa bumbuazi walioko mbinguni na kwenye ardhi isipo kuwa wale ambao Mwenyezi Mungu amewatakia. Mpaka pale kila mwenye haki akaitwaa haki yake. Tena wakasukumwa watu wa Motoni wende Motoni, na watu wa Peponi wakapelekwa huko. Nao hao waseme: Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye timiza ahadi yake, na akawahukumia wote kwa haki, na ikasemwa: Alhamdulilahi Rabbi'la'alamiin. Sifa njema zote ni za Mola Mlezi wa viumbe vyote.

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU




Previous - Next

Table of Contents | Words: Alphabetical - Frequency - Inverse - Length - Statistics | Help | IntraText Library

Best viewed with any browser at 800x600 or 768x1024 on Tablet PC
IntraText® (V89) - Some rights reserved by EuloTech SRL - 1996-2007. Content in this page is licensed under a Creative Commons License