51 - 75
51. Basi ukawasibu uovu wa waliyo yachuma. Na wale walio
dhulumu miongoni mwa hawa utawasibu uovu wa waliyo yachuma vile vile. Nao si
wenye kushinda.
52. Kwani wao hawajui kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia
riziki amtakaye na akamkadiria? Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara
kwa watu wanao amini.
53. Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate
tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote.
Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
54. Na rejeeni kwa Mola wenu Mlezi, na silimuni kwake,
kabla ya kukujieni adhabu. Kisha
hapo hamtanusuriwa.
55. Na fuateni
yaliyo bora kabisa katika yale yaliyo teremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu
Mlezi, kabla haijakujieni adhabu kwa ghafla, na hali hamtambui.
56. Isije
ikasema nafsi: Ee majuto yangu kwa yale niliyo poteza upande wa Mwenyezi Mungu,
na hakika nilikuwa miongoni mwa wanao fanya maskhara!
57. Au
ikasema: Ingeli kuwa Mwenyezi Mungu ameniongoa, bila ya shaka ningeli kuwa
miongoni mwa wenye kumchamngu.
58. Au
ikasema inapo ona adhabu: Lau kuwa ningeli pata fursa nyengine, ningeli kuwa
miongoni mwa wafanya mema.
59. Wapi!
Bila ya shaka zilikujia Ishara zangu, nawe ukazikadhibisha, na ukajivuna, na
ukawa miongoni mwa makafiri!
60. Na
Siku ya Kiyama utawaona walio msingizia uwongo Mwenyezi Mungu nyuso zao
zimesawijika. Je! Si katika Jahannamu makaazi ya wanao takabari?
61. Na
Mwenyezi Mungu atawaokoa wenye kujikinga kwa ajili ya kufuzu kwao. Hapana uovu
utao wagusa, wala hawatahuzunika.
62.
Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu, na Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila
kitu.
63. Yeye
anazo funguo za mbingu na ardhi. Na wale walio zikataa Ishara za Mwenyezi
Mungu, hao ndio wenye kukhasiri.
64. Sema:
Je! Mnaniamrisha nimuabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu, enyi majaahili?
65. Na kwa
yakini yamefunuliwa kwako na kwa walio kuwa kabla yako: Bila ya shaka ukimshirikisha
Mwenyezi Mungu a'mali zako zitaanguka, na lazima utakuwa miongoni mwa wenye
kukhasiri.
66. Bali
muabudu Mwenyezi Mungu tu, na uwe miongoni mwa wenye kushukuru.
67. Na
wala hawakumhishimu Mwenyezi Mungu kama anavyo stahiki kadiri yake. Na Siku ya
Kiyama ardhi yote itakuwa mkononi mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono wake
wa kuume. Subhanahu wa Taa'la Ametakasika na Ametukuka na hayo wanayo
mshirikisha nayo.
68. Na
litapulizwa barugumu, wazimie waliomo mbinguni na waliomo katika ardhi, isipo
kuwa aliye mtaka Mwenyezi Mungu. Kisha litapulizwa mara nyengine. Hapo watainuka wawe wanangojea.
69. Na
ardhi itang'ara kwa Nuru ya Mola wake Mlezi, na Kitabu kitawekwa, na wataletwa
Manabii na mashahidi, na patahukumiwa baina yao kwa haki, wala hawatadhulumiwa.
70. Na
kila nafsi italipwa kwa yale iliyo yafanya, na Yeye anayajua sana wanayo
yatenda.
71. Na
walio kufuru wataongozwa kuendea Jahannamu kwa makundi. Mpaka watakapo ifikia
itafunguliwa milango yake, na walinzi wake watawaambia: Kwani hawakukujilieni
Mitume miongoni mwenu wakikusomeeni Aya za Mola wenu Mlezi na kukuonyeni
mkutano wa siku yenu hii? Watasema: Kwani! Lakini limekwisha thibiti neno la
adhabu juu ya makafiri.
72.
Itasemwa: Ingieni milango ya Jahannamu mdumu humo. Basi nayo ni ubaya ulioje wa
makaazi ya wanao takabari!
73. Na
walio mcha Mola wao Mlezi wataongozwa kuendea Peponi kwa makundi, mpaka
watakapo fikilia, nayo milango yake imekwisha funguliwa. Walinzi wake
watawaambia: Salaam Alaikum, Amani iwe juu yenu! Mmet'ahirika. Basi
ingieni humu mkae milele.
74. Nao watasema: Alhamdulillah, Sifa njema zote ni za
Mwenyezi Mungu aliye tutimizia ahadi yake, na akaturithisha ardhi, tunakaa
katika Bustani popote tupendapo. Basi ni malipo mazuri yaliyoje ya watendao!
75. Na utawaona Malaika wakizunguka pembeni mwa Kiti cha
enzi cha Mwenyezi Mungu, wakimtakasa na kumsifu Mola wao Mlezi. Na patahukumiwa
baina yao kwa haki na patasemwa: Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola
Mlezi wa viumbe vyote!
|