41. SURAT FUSS'ILAT (AU H'A MIM
SAJDAH)
(Imeteremka
Makka)
Sura hii imeanzia kwa
harufi mbili katika harufi za alifbete kama inavyo fanya Qur'ani katika Sura nyingi.
Sura hii imeeleza katika nyingi ya Aya zake shani ya Qur'ani na mambo iliyo
kusanya yaliyo khusu bishara na maonyo. Na imeeleza msimamo wa washirikina
kukhusu Qur'ani, katika kuipuuza na kuupiga vita wito wake, na msimamo wa Mtume
kwa mnasaba wa makafiri, kwa kusimama imara juu ya wito wake kwao na kuwaambia:
"Hakika mimi ni mtu kama nyinyi; inafunuliwa kwangu ya kwamba Mungu wenu
ni Mungu Mmoja tu. Basi tengeneeni kumwendea Yeye, na mumtake msamaha." Na
Sura inaingilia kuwakumbusha washirikina uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika
kuziumba mbingu na ardhi, kisha inawahadharisha na yaliyo watokelea watu wa
mataifa walio karibu mno na makwao, nao ni kina A'adi na Thamudi. Na
inawakumbusha Siku ya Akhera, siku yatakapo washuhudia masikio yao, na macho
yao, na ngozi zao, kwa waliyo kuwa wakiyatenda; na mijadiliano itakayo kuwa
baina yao na viungo vyao siku hiyo; na watayo yaomba wafwasi kwa Mola wao Mlezi
Siku ya Kiyama: "Mola wetu Mlezi! Tuonyeshe wale walio tupoteza miongoni
mwa majini na watu ili tuwaweke chini ya miguu yetu, wapate kuwa miongoni mwa
walio chini kabisa." Na kama ilivyo kuwa mwendo wa Mwenyezi Mungu katika
Kitabu hichi akisimulia khabari ya makafiri, husimulia pia khabari za Waumini.
Basi Sura hii imesimulia khabari za walio sema: "Mola wetu Mlezi ni
Mwenyezi Mungu", kisha wakasimama sawa sawa, neema za daima alizo
waneemesha, na akalinganisha baina ya kheri na shari: "Wema haulingani na
uovu".
Kisha Sura inataka watu waangalie Ishara za uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu
zinazo onyesha kumkinika kufufuliwa maiti, kisha inarejea tena kuzidi kuwakemea
wanao zigeuza Aya za Mwenyezi Mungu, na kwamba hao hawamkhofu Mwenyezi Mungu.
Na kwamba hakika Kitabu hichi hakiingiliwi na upotovu kutoka mbele yake wala
nyuma yake. Huu ni mteremsho ulio tokana na Mwenye hikima, Msifika. Na hakika
Ujumbe wa Muhammad si ujumbe ulio zuliwa tu.
Na Sura inathibitisha khulka moja katika khulka za binaadammu, nayo ni kuwa
Mwenyezi Mungu akimneemesha mtu huipuuza Haki, na ikimgusa tu shari anakuwa na
madua marefu marefu.
Na Sura imekhitimisha kwa kuthibitisha mambo mawili muhimu kabisa, nayo ni la
kwanza: kutaja kwa yenyewe Haki iliyomo ndani yake isiyo na shaka yoyote:
"Tutawaonyesha Aya zetu katika upeo wa macho na katika nafsi zao wenyewe
mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli." Na la pili lake kuwa hilo wanalo
litegemea makafiri si lolote ila ni shaka tu ya kufufuliwa iliyo wapelekea kuwa
nayo ukafiri na upotovu. "Ama hakika wao bado wamo katika shaka ya
kukutana na Mola wao Mlezi. Hakika Yeye amekizunguka kila kitu."
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. H'a Mim
2.
Uteremsho huu umetoka kwa Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
3. Hichi
ni Kitabu kilicho pambanuliwa Aya zake, cha kusomwa kwa Kiarabu kwa watu wanao
jua.
4.
Kitoacho khabari njema, na chenye kuonya. Lakini wengi katika wao wamepuuza;
kwa hivyo hawasikii.
5. Na wakasema:
Nyoyo zetu zimo katika vifuniko kwa hayo unayo tuitia, na masikio yetu yana
uziwi, na baina yetu na wewe lipo pazia. Basi wewe tenda, nasi
tunatenda.
6. Sema: Hakika mimi ni mtu kama nyinyi; inafunuliwa kwangu
ya kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Basi nyookeni sawa kumwendea Yeye, na
mumtake msamaha, na ole wao wanao mshirikisha,
7. Ambao hawatoi Zaka na wanaikataa Akhera.
8. Hakika wanao amini na wakatenda mema watakuwa na ujira
usio na ukomo.
9. Sema: Hivyo nyinyi mnamkataa aliye umba ardhi katika
siku mbili, na mnamfanyia washirika? Huyu ndiye Mola Mlezi wa walimwengu wote.
10. Na akaweka humo milima juu yake, na akabarikia humo na
akakadiria humo chakula chake katika siku nne. Haya ni sawa kabisa kwa wanao
uliza.
11. Kisha akazielekea mbingu, na zilikuwa moshi, akaziambia
hizo na ardhi: Njooni, kwa khiari au kwa nguvu! Vyote viwili vikasema: Tumekuja
nasi ni wat'iifu.
12. Basi akazifanya mbingu saba kwa siku mbili, na
akazipangia kila mbingu mambo yake. Na tukaipamba mbingu ya chini kwa mataa na
kwa ulinzi. Hichi ndicho kipimo cha Mwenyezi Mungu Mwenye Kujua.
13. Basi wakipuuza wewe sema: Nakuhadharisheni adhabu mfano
wa adhabu ya A'di na Thamudi,
14. Walipo wajia Mitume mbele yao na nyuma yao wakawaambia:
Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu! Wakasema: Angeli taka Mola wetu Mlezi bila ya
shaka angeli wateremsha Malaika. Basi sisi hakika tunayakataa hayo mliyo tumwa.
15. Ama kina A'di walijivuna katika nchi bila ya haki, na
wakasema: Nani aliye kuwa na nguvu kushinda sisi? Kwani wao hawakuona kwamba Mwenyezi
Mungu aliye waumba ni Mwenye nguvu kushinda wao? Na wao wakawa wanazikataa
Ishara zetu!
16. Basi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku za
ukorofi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwahizi katika uhai wa duniani, na bila ya
shaka adhabu ya Akhera ina hizaya zaidi, na wala wao hawatanusuriwa.
17. Na ama Thamudi tuliwaongoza, lakini walipenda upofu
kuliko uwongofu. Basi uliwachukua moto wa adhabu ya kuwafedhehi kwa sababu ya
yale waliyo kuwa wakiyachuma.
18. Na tukawaokoa walio amini na wakawa wanamcha-mngu.
19. Na siku watakapo kusanywa maadui wa Mwenyezi Mungu
kwenye Moto, nao wakikgawanywa kwa makundi.
20. Hata watakapo ufikia Moto yatawashuhudia masikio yao,
na macho yao na ngozi zao kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
21. Na wao wataziambia ngozi zao: Kwa nini mmetushuhudilia?
Nazo zitasema: Ametutamkisha Mwenyezi Mungu ambaye ametamkisha kila kitu! Na
Yeye ndiye aliye kuumbeni mara ya kwanza, na kwake Yeye tu mtarejeshwa.
22. Na hamkuwa wenye kujificha hata masikio yenu, na macho
yenu, na ngozi zenu, zisikushuhudilieni. Lakini mlidhani kwamba Mwenyezi Mungu
hayajui mengi katika mliyo kuwa mkiyatenda.
23. Basi hiyo dhana yenu mliyo kuwa mkimdhania Mola wenu
Mlezi. Imekuangamizeni; na mmekuwa miongoni mwa walio khasiri.
24. Basi wakisubiri Moto ndio maskani yao. Na wakiomba
radhi hawakubaliwi.
25. Na tukawawekea marafiki, na wakawapambia yaliyo mbele
yao na nyuma yao. Basi ikawathibitikia kauli wawe pamoja na mataifa yaliyo pita
kabla yao, miongoni mwa majini na watu. Hakika hao wamekuwa ni wenye
kukhasirika.
26. Na walio kufuru walisema: Msiisikilize Qur'ani hii, na
timueni zogo, huenda mkashinda.
27. Basi hapana shaka tutawaonjesha hao walio kufuru adhabu
kali, na hapana shaka tutawalipa malipo mabaya ya yale waliyo kuwa wakiyafanya.
28. Hayo ndiyo malipo ya Maadui wa Mwenyezi Mungu - Moto!
Humo watakuwa na maskani ya kudumu, ndiyo malipo yao kwa sababu walikuwa
wakizikataa Ishara zetu.
29. Na walio kufuru watasema: Mola wetu Mlezi! Tuonyeshe
walio tupoteza miongoni mwa majini na watu ili tuwaweke chini ya miguu yetu,
wapate kuwa miongoni wa walio chini kabisa.
30. Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu!
Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala
msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyo kuwa mkiahidiwa.
31. Sisi ni vipenzi vyenu katika maisha ya dunia na katika
Akhera, na humo mtapata kinacho tamaniwa na nafsi zenu, na humo mtapata
mtakavyo vitaka.
32. Ni takrima itokayo kwa Mwenye kusamehe, Mwenye
kurehemu.
33. Na ni nani mbora wa kusema kuliko aitaye kwa Mwenyezi
Mungu na akatenda mema, na akasema: Hakika mimi ni katika Waislamu?
34. Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa lilio jema zaidi.
Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa
kukuonea uchungu.
35. Lakini hawapewi wema huu ila wanao subiri, wala
hawapewi ila wenye bahati kubwa.
36. Na Shet'ani akikuchochea kwa uchochezi wewe jikinge kwa
Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
37. Na katika Ishara zake ni usiku na mchana, na jua na
mwezi. Basi msilisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Mwenyezi Mungu aliye
viumba, ikiwa nyinyi mnamuabudu Yeye tu.
38. Na ikiwa watajivuna, basi hao walioko kwa Mola wako
Mlezi wanamtakasa Yeye usiku na mchana, na wao hawachoki.
39. Na katika Ishara zake ni kwamba unaiona ardhi nyonge,
lakini tunapo iteremshia maji mara unaiona inataharaki na kuumuka. Bila ya
shaka aliye ihuisha ardhi ndiye atakaye huisha wafu. Hakika Yeye ni Muweza wa
kila kitu.
40. Hakika wale wanao upotoa ukweli uliomo katika Ishara zetu
hawatufichikii Sisi. Je! Atakaye tupwa Motoni ni bora au atakaye kuja kwa amani
Siku ya Kiyama? Tendeni mpendavyo, kwa hakika Yeye anayaona mnayo yatenda.
41. Kwa hakika wanayo yakataa mawaidha haya yanapo wajia
(wataangamia), na haya bila ya shaka ni Kitabu chenye nguvu na utukufu.
42. Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake.
Kimeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa.
43. Huambiwi ila yale yale waliyo ambiwa Mitume wa kabla
yako. Hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ni Mwenye maghfira, na ni Mwenye
adhabu chungu.
44. Na lau tungeli ifanya Qur'ani kwa lugha ya kigeni
wangeli sema: Kwanini Aya zake haziku pambanuliwa? Yawaje lugha ya kigeni na
Mtume Mwaarabu? Sema: Hii Qur'ani ni uwongofu na poza kwa wenye kuamini. Na
wasio amini umo uziwi katika masikio yao, nayo kwao imezibwa hawaioni. Hao
wanaitwa nao wako pahala mbali.
45. Na hakika tulimpa Musa Kitabu, lakini pakatokea
khitilafu kati yake. Na lau kuwa halikwisha tangulia neno la Mola wako Mlezi
wangeli hukumiwa. Na hakika wao wamo katika shaka yenye kuwatia wasiwasi.
46. Anaye tenda mema basi anajitendea mwenyewe nafsi yake,
na mwenye kutenda uovu basi ni juu ya nafsi yake vile vile; wala Mola wako
Mlezi si mwenye kuwadhulumu waja.
47. UJUZI wa kuijua Saa ya Kiyama unarudishwa kwake tu
Mwenyezi Mungu. Na matunda hayatoki katika mafumba yake, wala mwanamke hachukui
mimba, wala hazai, ila kwa kujua kwake. Na siku atakayo waita, akawaambia: Wako
wapi washirika wangu? Hapo watasema: Tunakiri kwako ya kwamba hapana miongoni
mwetu anaye shuhudia hayo.
48. Na wakawapotea wale walio kuwa wakiwaomba hapo kwanza,
na wakawa na yakini kuwa hawana pa kukimbilia.
49. Mwanaadamu hachoki kuomba dua za kheri, na inapo mpata
shari, mara huvunjika moyo akakata tamaa.
50. Na pindi tukimwonjesha rehema itokayo kwetu baada ya
kumgusa dhara, bila ya shaka husema: Haya nayastahiki mimi, wala sidhani kuwa
Kiyama kitakuja. Na hata nikirudishwa kwa Mola wangu Mlezi bila ya shaka nina
mema yangu kwake! Basi kwa yakini tutawaelezea walio kufuru hayo waliyo
yatenda, na kwa yakini tutawaonjesha adhabu ngumu.
51. Na tukimneemesha mwanaadamu hugeuka na kujitenga
upande, na inapo mgusa shari, huwa na madua marefu marefu.
52. Sema: Mnaonaje! Ikiwa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu,
nanyi ikawa ndio mmeyakataa, ni nani aliye potea zaidi kuliko aliye katika
upinzani wa mbali?
53. Tutawaonyesha Ishara zetu katika upeo wa mbali na
katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi
kwamba Mola wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu?
54. Ama wao wamo katika shaka ya kukutana na Mola wao
Mlezi! Ama hakika Yeye amekizunguka kila kitu.
|