51 - 89
51. Na Firauni alitangaza kwa watu wake, akisema: Enyi watu
wangu! Kwani mimi sinao huu ufalme wa Misri, na hii mito inapita chini yangu?
Je! Hamwoni?
52. Au mimi si bora kuliko huyu aliye mnyonge, wala hawezi
kusema waziwazi?
53. Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu, au hawakuja
Malaika pamoja naye wakamwandama?
54. Basi aliwachezea watu wake, na wakamt'ii. Kwa hakika
hao walikuwa watu wapotovu.
55. Walipo tukasirisha tuliwapatiliza tukawazamisha wote!
56. Kisha tukawafanya kuwa watangulizi na mfano kwa wa
baadaye.
57. Na alipo pigiwa mfano Mwana wa Mariamu, watu wako
waliupiga ukelele.
58. Wakasema: Miungu yetu kwani si bora kuliko huyu?
Hawakukupigia mfano huo ila kwa ubishi tu. Bali hao ni watu wagomvi!
59. Hakuwa yeye (Isa) ila ni Mtumwa tuliye mneemesha na
tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili.
60. Na tungeli penda tungeli wafanyia miongoni mwenu
Malaika katika ardhi wakifuatana.
61. Na kwa hakika yeye ni alama ya Saa ya Kiyama. Basi
usiitilie shaka, na nifuateni. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
62. Wala asikuzuilieni Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu
wa dhaahiri.
63. Na alipo kuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema:
Nimekujieni na hikima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyo khitalifiana.
Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnit'ii mimi.
64. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na ni
Mola wenu Mlezi. Basi Muabuduni Yeye tu. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
65. Lakini makundi kwa makundi yao yalikhitalifiana wao kwa
wao. Ole wao walio dhulumu kwa adhabu ya siku chungu.
66. Je! Nini wanangojea ila Saa iwajie kwa ghafla na wala
wao hawatambui?
67. Siku hiyo marafiki watakuwa ni maadui, wao kwa wao,
isipo kuwa wachamngu.
68. Enyi
waja wangu! Hamtakuwa na khofu siku hiyo, wala hamtahuzunika.
69. Ambao
waliziamini Ishara zangu na walikuwa Waislamu.
70.
Ingieni Peponi, nyinyi na wake zenu; mtafurahishwa humo.
71.
Watakuwa wanapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe; na vitakuwamo ambavyo
nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia, na nyinyi mtakaa humo milele.
72. Na
hiyo ni Pepo mliyo rithishwa kwa hayo mliyo kuwa mkiyafanya.
73. Mnayo
humo matunda mengi mtakayo yala.
74. Kwa
hakika wakosefu watakaa katika adhabu ya Jahannamu.
75.
Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa.
76. Wala
Sisi hatukuwadhulumu, bali wao ndio walio kuwa madhaalimu.
77. Nao
watapiga kelele waseme: Ewe Malik! Na atufishe Mola wako Mlezi! Naye
aseme: Hakika nyinyi mtakaa humo humo!
78. Kwa yakini tulikuleteeni Haki, lakini wengi katika
nyinyi mlikuwa mnaichukia Haki.
79. Au waliweza kupitisha amri yao? Bali ni Sisi ndio tunao
pitisha.
80. Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na minong'ono
yao? Wapi! Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika.
81. Sema: Ingeli kuwa Rahmani ana mwana, basi mimi ningeli
kuwa wa kwanza kumuabudu.
82. Ametakasika Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, Mola Mlezi
wa A'rshi, na hayo wanayo msifia.
83. Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe na
hiyo siku yao waliyo ahidiwa.
84. Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika
ardhi. Naye ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi.
85. Na ametukuka Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na
viliomo ndani yake. Na uko kwake ujuzi wa Saa ya Kiyama, na kwake Yeye
mtarudishwa.
86. Wala hao mnao waomba badala yake Yeye hawana uweza wa
kumwombea mtu, isipo kuwa anaye shuhudia kwa haki, na wao wanajua.
87. Na ukiwauliza ni nani aliye waumba? Bila ya shaka
watasema: Mwenyezi Mungu! Basi ni wapi wanako geuziwa?
88. Na usemi wake (Mtume) ni: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika
hawa ni watu wasio amini.
89. Basi wasamehe, na uwambie maneno ya salama. Watakuja jua.
|