45. SURAT AL-JAATHIYA
(Imeteremka
Makka)
Imeanzia Sura hii kwa
harufi mbili katika harufi za Alifbete, na ikafuatiliza kwa kubainisha kuwa
kuteremshwa Qur'ani kumetokana na Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu Mwenye hikima.
Kisha ikazitaja dalili za uumbaji na za kiakili kuthibitisha itikadi ya Imani
na kuitia watu waifuate. Hali kadhaalika imekusanya wito kwa wenye kukadhibisha
Ishara. Kisha ikaingia kuzihisabu neema za Mwenyezi Mungu na fadhila zake kwa
waja wake; na ikawataka Waumini wawasamehe makafiri wanao kanya. Kwani Mwenyezi
Mungu peke yake ndiye wa kumlipa kila mtu kwa alilo litenda. Kisha Sura baada
ya hayo ikazungumzia vipi Mwenyezi Mungu alivyo wafadhili Wana wa Israili kwa
kuwapa neema nyingi, na khitilafu zilizo zuka baina yao ambazo Mwenyezi Mungu
atazitolea hukumu Siku ya Kiyama. Kisha ikaingia kufarikisha baina ya walio
fuata Haki na walio fuata matamanio, wakakanya kufufuliwa, na wakapinga Ishara
za uweza kwa kutaka wafufuliwe baba zao! Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye
kuhuisha, na ndiye Mwenye kufisha. Yeye ana ufalme wa kila kitu. Na siku
watakapo kusanywa wapotovu kila nafsi itaitwa ikapokee kitabu chake. Hapo
watafuzu Waumini na watakemewa walio takabari. Sura tena inarejea hadithi ya
kule kuikataa kwao Saa ya Kiyama, na kuzikadhibisha Ishara zinazo ionyesha; na
vile Mwenyezi Mungu atavyo wasahau wao kama wao walivyo isahau hii Siku. Na ikabainisha
kuwa makaazi yao ni Motoni kwa kule kuzikejeli kwao Ishara za Mwenyezi Mungu na
kudanganyika kwao na dunia. Na Sura imekhitimisha kwa kumsifu Muumba mbingu na
ardhi, Mwenye utukufu kote humo, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. H'a Mim
2.
Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
3. Hakika
katika mbingu na ardhi ziko Ishara kwa Waumini.
4. Na katika
umbo lenu na katika wanyama alio watawanya zimo Ishara kwa watu wenye yakini.
5. Na
kupishana usiku na mchana, na riziki anayo iteremsha Mwenyezi Mungu kutoka
mbinguni, na kwayo akaifufua ardhi baada ya kufa kwake, na mabadiliko ya upepo,
ni Ishara kwa watu wenye akili.
6. Hizi
Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki; basi hadithi gani watakayo iamini
baada ya Mwenyezi Mungu na Aya zake?
7. Ole
wake kila mzushi mwenye dhambi!
8. Anaye
sikia Aya za Mwenyezi Mungu akisomewa, kisha anashikilia yale yale aliyo
katazwa, na anajivuna, kama kwamba hakuzisikia. Basi mbashirie adhabu chungu!
9. Na
anapo kijua kitu kidogo katika Aya zetu hukifanyia mzaha. Watu hao ndio watakao
kuwa na adhabu ya kufedhehesha.
10. Na nyuma yao ipo Jahannamu. Na walio yachuma
hayatawafaa hata kidogo, wala walinzi walio washika badala ya Mwenyezi Mungu.
Na watapata adhabu kubwa.
11. Huu ni uwongofu. Na wale wale walio zikataa Ishara za
Mola wao Mlezi watapata adhabu inayo tokana na ghadhabu iliyo chungu.
12. Mwenyezi Mungu ndiye aliye ifanya bahari ikutumikieni,
ili humo zipite marikebu kwa amri yake, na ili mtafute fadhila yake, na mpate
kushukuru.
13. Na amefanya vikutumikieni vilivyomo mbinguni na
vilivyomo katika ardhi, vyote vimetoka kwake. Hakika katika hayo zimo Ishara
kwa watu wanao fikiri.
14. Waambie walio amini wawasamehe wale wasio zitaraji siku
za Mwenyezi Mungu, ili awalipe kwa waliyo kuwa wakiyachuma.
15. Mwenye kutenda mema basi ni kwa ajili ya nafsi yake, na
mwenye kutenda uovu ni juu yake mwenyewe. Kisha mtarudishwa kwa Mola wenu
Mlezi.
16. Na hakika tuliwapa Wana wa Israili Kitabu na hukumu na
Unabii, na tukawaruzuku vitu vizuri vizuri, na tukawafadhilisha kuliko
walimwengu wote.
17. Na tukawapa maelezo wazi ya amri. Basi hawakukhitalifiana
ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa ajili ya uhasidi uliyo kuwa baina yao. Hakika
Mola wako Mlezi atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika mambo waliyo kuwa
wakikhitalifiana.
18. Kisha tukakuweka wewe juu ya Njia ya haya mambo, basi
ifuate, wala usifuate matamanio ya wasio jua kitu.
19. Kwa hakika hao hawatakufaa kitu mbele ya Mwenyezi
Mungu. Na hakika wenye kudhulumu ni marafiki wao kwa wao. Na Mwenyezi Mungu ni
rafiki wa wamchao.
20. Hizi ni dalili zilizo wazi kwa watu wote, na ni
uwongofu, na rehema kwa watu wanao yakinisha.
21. Je! Wanadhani wanao tenda maovu kuwa tutawafanya kama
walio amini, na wakatenda mema, sawa sawa uhai wao na kufa kwao? Ni hukumu
mbaya wanayo ihukumu!
22. Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki,
na ili kila nafsi ilipwe yale iliyo yachuma. Nao hawatadhulumiwa.
23. Je! Umemwona aliye fanya matamanio yake kuwa ndiye
mungu wake, na Mwenyezi Mungu akamwacha apotee pamoja na kuwa ana ujuzi, na
akapiga muhuri juu ya masikio yake, na moyo wake, na akambandika vitanga
machoni mwake? Basi nani atamwongoa huyo baada ya Mwenyezi Mungu? Hamkumbuki?
24. Na
walisema: Hapana ila huu uhai wetu wa duniani - twafa na twaishi, na hapana
kinacho tuhiliki isipo kuwa dahari. Lakini wao hawana ilimu ya hayo, ila wao
wanadhani tu.
25. Na
wakisomewa Aya zetu zilizo wazi hawana hoja ila kusema: Waleteni baba zetu,
ikiwa nyinyi ni wasemao kweli.
26. Sema:
Mwenyezi Mungu anakuhuisheni, kisha anakufisheni, kisha anakukusanyeni Siku ya
Kiyama isiyo na shaka. Lakini watu wengi hawajui.
27. Na
Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Na siku itapo simama Saa
ya Kiyama, siku hiyo wataangamia wenye kushikamana na upotovu.
28. Na
utauona kila umma umepiga magoti, na kila umma utaitwa kwenda soma kitabu
chake: Leo mtalipwa mliyo kuwa mkiyatenda.
29. Hichi
kitabu chetu kinasema juu yenu kwa haki. Hakika Sisi tulikuwa tukiyaandika
mliyo kuwa mkiyatenda.
30. Ama
walio amini na wakatenda mema, Mola wao Mlezi atawatia katika rehema yake. Huko
ndiko kufuzu kulio wazi.
31. Na ama
walio kufuru, wataambiwa: Kwani hamkuwa mkisomewa Aya zangu nanyi mkapanda
kichwa, na mkawa watu wakosefu?
32. Na
ikisemwa: Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli, na Saa haina shaka, nyinyi
mkisema: Hatuijui hiyo Saa, tunadhania dhana tu, wala hatuna yakini.
33. Basi
ubaya wa waliyo yatenda utawadhihirikia, na yatawazunguka waliyo yafanyia
maskhara.
34. Na itasemwa:
Leo tunakusahauni kama nyinyi mlivyo sahau mkutano wa siku yenu hii; na mahali
penu ni Motoni, wala hamna wa kukunusuruni.
35. Hayo
ni kwa sababu nyinyi mlizifanyia mzaha Aya za Mwenyezi Mungu; na maisha ya
dunia yakakudanganyeni. Basi leo hawatatolewa humo wala hao hawatakubaliwa
udhuru wao.
36. Basi
sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa mbingu, na Mola Mlezi wa
ardhi, na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
37. Na
ukubwa ni wake Yeye tu, mbinguni na katika ardhi, naye ni Mwenye nguvu, Mwenye
hikima.
|