51. SURAT ADH-DHAARIYAAT
(Imeteremka
Makka)
Sura hii imeanza kwa kiapo
cha ukweli wa kufufuliwa na kutokea malipo. Kisha ikafuatisha kwa kiapo kingine
juu ya ubabaishi wa wanao kanya katika maneno yao juu ya Mtume wa Mwenyezi
Mungu, na juu ya . Kisha ikaingia kuwaonya wanao kanya kuwa watapata mwisho
muovu katika Akhera. Tena ikaeleza waliyo ahidiwa wachamngu katika malipo ya
vitendo vyao vyema walivyo vitanguliza duniani. Kisha ikawazindua watu
wazingatie Ishara za Mwenyezi Mungu katika kuumba kwake, na katika nafsi zao,
na katika mambo ya ufundi wa ajabu na uzuri wa umbo alio uweka humo.
Na ikasimulia kisa cha Ibrahim na wageni wake Malaika, kisha ikaeleza hali za
baadhi ya mataifa na maangamizo yaliyo wasibu kwa kuwakadhibisha Manabii wao.
Kisha ikaashiria kwa jumla baadhi ya Ishara za uumbaji, na ikahimiza watu
warejee kwa Mwenyezi Mungu, na wamuabudu Yeye peke yake, ambayo hayo ndio
makusudi ya kuumbwa majini na watu. Na Sura imekhitimisha kwa kuwaonya wanao
mkadhibisha Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. kuwa watapata adhabu iliyo kwisha
wapata kaumu za kabla yao.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1.
Naapa kwa pepo zinazo tawanya,
2. Na zinazo beba mizigo,
3. Na zinazo kwenda kwa wepesi.
4. Na zinazo gawanya kwa amri,
5. Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka ni kweli,
6. Na kwa hakika malipo bila ya shaka yatatokea.
7. Naapa kwa mbingu zenye njia,
8. Hakika nyinyi bila ya shaka mmo katika kauli inayo
khitalifiana.
9. Anageuzwa kutokana na haki mwenye kugeuzwa.
10.
Wazushi wameangamizwa.
11. Ambao
wameghafilika katika ujinga.
12.
Wanauliza: Ni lini hiyo siku ya malipo?
13. Hiyo
ni siku watakayo adhibiwa Motoni.
14. Onjeni
adhabu yenu! Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyahimiza.
15. Hakika
wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem.
16.
Wanapokea aliyo wapa Mola wao Mlezi. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya
wakifanya mema.
17.
Walikuwa wakilala kidogo tu usiku.
18. Na
kabla ya alfajiri wakiomba maghfira.
19. Na
katika mali yao ipo haki ya mwenye kuomba na asiye omba.
20. Na
katika ardhi zipo Ishara kwa wenye yakini.
21. Na pia
katika nafsi zenu - Je! Hamwoni?
22. Na katika mbingu ziko riziki zenu na mliyo ahidiwa.
23. Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, hakika
haya ni kweli kama ilivyo kweli kuwa nyinyi mnasema.
24. Je! Imekufikia hadithi ya wageni wa Ibrahim wanao
hishimiwa?
25. Walipo ingia kwake wakasema: Salama! Na yeye akasema:
Salama! Nyinyi ni watu nisio
kujueni.
26. Akenda kwa
ahali yake na akaja na ndama aliye nona.
27.
Akawakaribisha, akasema: Mbona hamli?
28. Akahisi
kuwaogopa katika nafsi yake. Wakasema: Usiwe na khofu, nao wakambashiria kupata
kijana mwenye ilimu.
29. Ndipo mkewe
akawaelekea, na huku anasema na akijipiga usoni kwa mastaajabu, na kusema: Mimi
ni kikongwe na tasa!
30. Wakasema:
Ndivyo vivyo hivyo alivyo sema Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na
Mwenye kujua.
31. AKASEMA:
Basi ujumbe wenu ni nini, enyi mlio tumwa?
32. Wakasema:
Hakika sisi tumetumwa kwa watu wakosefu,
33. Tuwatupie
mawe ya udongo,
34. Yaliyo tiwa
alama kutoka kwa Mola wako Mlezi kwa ajili ya wanao pindukia mipaka.
35. Kwa hivyo
tutawatoa katika hao wale walio amini.
36. Lakini hatukupata
humo ila nyumba moja tu yenye Waislamu!
37. Na tukaacha
humo Ishara kwa ajili ya wanao iogopa adhabu chungu.
38. Na katika
khabari za Musa, tulipo mtuma kwa Firauni na hoja wazi.
39. Lakini
alipuuza kwa sababu ya nguvu zake na akasema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu!
40. Basi
tukamkamata yeye na majeshi yake na tukawatupa baharini, na yeye ndiye wa
kulaumiwa.
41. Na katika
khabari za A'di tulipo wapelekea upepo wa kukata uzazi.
42. Haukuacha
chochote ulicho kifikia ila ulikifanya kama kilio nyambuka.
43. Na katika
khabari za Thamudi walipo ambiwa: Jifurahisheni kwa muda mdogo tu.
44. Wakaasi amri
ya Mola wao Mlezi. Basi uliwanyakua moto wa radi nao wanaona.
45. Basi hawakuweza kusimama wala hawakuwa wenye kujitetea.
46. Na kaumu ya Nuhu hapo mbele. Hakika hao walikuwa watu
wapotovu.
47. Na mbingu tumezifanya kwa nguvu na uwezo na hakika Sisi
bila ya shaka ndio twenye uwezo wa kuzitanua.
48. Na ardhi tumeitandaza; basi watandazaji wazuri namna
gani Sisi!
49. Na katika kila kitu tumeumba kwa jozi ili mzingatie.
50. Basi kimbilieni kwa Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni
mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake.
51. Wala msifanye kuwa kuna mungu mwengine pamoja na
Mwenyezi Mungu. Hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake.
52. Basi ndio hivyo hivyo, hakuwajia kabla yao Mtume ila
walisema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu.
53. Je!
Wameambizana kwa haya? Bali hawa ni watu waasi.
54. Basi waachilie mbali, nawe hulaumiwi.
55. Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa Waumini.
56. Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.
57. Na sitaki kwao riziki, wala sitaki wanilishe.
58. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye
nguvu, Madhubuti.
59. Hakika walio dhulumu wana fungu lao la adhabu kama
fungu la wenzao. Basi wasinihimize.
60. Ole wao walio ikanusha siku yao waliyo ahidiwa.
|