52. SURAT ATT'UR
(Imeteremka
Makka)
Sura hii imeanza kwa kiapo
cha watano katika bora wa viumbe kuwa adhabu itawateremkia hao wanao kanusha. Kisha
ikafikia kusimulia kuwateremkia hiyo adhabu, na namna zake mbali mbali siku ya
kufufuliwa na kulipwa. Na ikaingia kutaja mazungumzo juu ya neema za wachamngu
na watakayo stareheshwa nayo katika Mabustani ya milele, na namna ya ukarimu
watakao upata, na kisha yatakavyo tua macho yao kwa kuwa dhuriya zao watavyo
wafuata, na kunyanyuliwa vyeo vyao wawafikie wao. Na baada ya hayo Sura
inamuamrisha Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. adumishe kukumbusha bila ya kujali
wanayo mzulia makafiri kumpinga yeye, au kushughulika na wayasemayo juu ya ,
kwa vile inavyo onyesha kuwa wameshindwa kuleta maneno mfano wa Qur'ani.
Sura hii pia imekashifu maoni yao makafiri ya ufisadi ya kutangaza upotovu wao,
na uovu wa kupima kwao. Kisha ikakhitimishia kwa kumuelekea Nabii s.a.w. na
kumwambia awaachilie mbali mpaka watakapo ikuta siku yao watapo situshwa, naye
akaamrishwa aistahamilie hukumu ya Mola wake Mlezi ya kuwapa muhula hao, kwani
hayo hayatamdhuru kitu yeye kwa sababu yumo katika uhifadhi wa Mola wake Mlezi
na ulinzi wake. Kadhaalika imemtaka amtakase Mwenyezi Mungu na katika nyakati
zote, na katika kila msimamo atakao kuwamo kwa jambo lolote, na usiku zinapo
tua nyota.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Naapa kwa mlima wa T'ur,
2. Na Kitabu kilicho andikwa
3. Katika ngozi iliyo kunjuliwa,
4. Na kwa Nyumba iliyo jengwa,
5. Na kwa dari iliyo nyanyuliwa,
6. Na kwa bahari iliyo jazwa,
7. Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi hapana shaka itatokea.
8. Hapana
wa kuizuia.
9. Siku
zitakapo tikisika mbingu kwa mtikiso,
10. Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa.
11. Basi ole wao siku hiyo hao wanao kadhibisha,
12. Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi.
13. Siku watapo sukumwa kwenye Moto kwa msukumo wa nguvu,
14. (Waambiwe): Huu ndio ule Moto mlio kuwa mkiukanusha!
15. Je! Huu ni
uchawi, au hamwoni tu?
16. Uingieni,
mkistahamili au msistahamili - ni mamoja kwenu. Hakika mnalipwa kwa mliyo kuwa
mkiyatenda.
17. Hakika
wachamngu watakuwa katika Mabustani na neema,
18. Wakifurahi
kwa yale aliyo wapa Mola wao Mlezi. Na Mola wao Mlezi atawalinda na
adhabu ya Motoni.
19. Kuleni na kunyweni kwa raha kabisa kwa sababu ya mliyo
kuwa mkiyatenda.
20. Watakuwa wameegemea juu ya viti vya enzi vilivyo pangwa
kwa safu. Na tutawaoza mahuru-l-aini.
21. Na walio amini na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani
tutawakutanisha nao dhuriya zao, na wala hatutawapunja hata kidogo katika
vitendo vyao. Kila mtu lazima atapata alicho kichuma.
22. Na tutawapa matunda, na nyama kama watavyo penda.
23. Watapeana humo bilauri zisio na vinywaji vya kuleta
maneno ya upuuzi wala dhambi.
24. Iwe wanawapitia watumishi wao kama kwamba ni lulu
zilizomo katika chaza.
25.
Wataelekeana wakiulizana.
26.
Waseme: Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa;
27. Basi Mwenyezi
Mungu akatufanyia hisani na akatulinda na adhabu ya upepo wa Moto.
28. Hakika
sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye tu. Hakika Yeye ndiye Mwema Mwenye
kurehemu.
29. Basi
kumbusha! Kwani wewe, kwa neema ya Mola wako Mlezi, si kuhani wala
mwendawazimu.
30. Au
wanasema: Huyu ni mtunga mashairi, tunamtarajia kupatilizwa na dahari.
31. Sema:
Tarajieni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika kutarajia.
32. Au
hizo akili zao ndio zinawaamrisha haya, au wao basi ni watu majeuri tu?
33. Au ndio wanasema: Ameitunga hii! Bali basi tu
hawaamini!
34. Basi nawalete masimulizi kama haya ikiwa wao wanasema
kweli.
35. Au wao wameumbwa pasipo kutokana na kitu chochote, au
ni wao ndio waumbaji?
36. Au wao wameziumba mbingu na ardhi? Bali hawana na
yakini.
37. Au wanazo khazina za Mola wako Mlezi au wao ndio wenye
madaraka?
38. Au wanazo ngazi za kusikilizia? Basi huyo msikilizaji
wao na alete hoja ilio wazi!
39. Au Yeye Mwenyezi Mungu ana wasichana, na nyinyi ndio
mna wavulana?
40. Au wewe unawaomba ujira, na kwa hivyo ndio wanaelemewa
na uzito wa gharama?
41. Au wanayo ilimu ya ghaibu, nao wameandika?
42. Au wanataka
kufanya vitimbi tu? Lakini hao walio kufuru ndio watakao tegeka.
43. Au wanae
mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu? Subhanallah! Ametaksika Mwenyezi Mungu na hao
wanao washirikisha naye.
44. Na hata
wange ona pande linatoka mbinguni linaanguka wange sema: Ni mawingu yaliyo
bebana.
45. Basi waache
mpaka wakutane na siku yao watakapo hilikishwa.
46. Siku ambayo
hila zao hazitawafaa hata kidogo, wala wao hawatanusuriwa.
47. Na hakika
walio dhulumu watapata adhabu nyengine isiyo kuwa hii, lakini wengi wao
hawajui.
48. Na ingojee
hukumu ya Mola wako Mlezi. Kwani wewe hakika uko mbele ya macho yetu, na
mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi unapo simama,
49. Na usiku pia
mtakase, na zinapo kuchwa nyota.
|