54. SURAT AL-QAMAR
(Imeteremka
Makka)
Imekuja Aya ya kwanza
katika Sura hii kuzindua kuwa watu wasikilize kwamba Kiyama kinakaribia, na
watu wanahadharishwa na tukio hilo. Kisha zimekuja Aya nyengine baada yake
kuweka wazi msimamo wa makafiri kwa mintarafu ya miujiza, na kushikilia kwao
kukadhibisha. Na anatakiwa Mtume s.a.w. awapuuze na awangojee mpaka siku
watakapo toka makaburini kama nzige walio tapanyika.
Tena baada ya hapo Aya zikawa zinafuatana, zikieleza hali namna mbali mbali za
mataifa yaliyo tangulia kwa mnasaba na Mitume wao, na adhabu iliyo washukia. Na
baina ya kila kisa na kingine inazindua mawazo ya kwamba imefanywa nyepesi kwa mwenye
kutaka kuwaidhika na kuzingatia.
Mwishoe inabainisha kwamba hao makafiri wa Makka si watu wenye nguvu zaidi au
wakali zaidi kushinda mataifa yaliyo kwisha tangulia, na kwamba wao si wenye
kuiepuka adhabu. Tena Sura ikakhitimisha kwa kuwahadharisha wanao kadhibisha
wenye inda kuwa mwisho wao watakuja tumbukizwa Motoni kifudifudi, na
wataambiwa: Onjeni mguso wa Jahannamu mliyo kuwa mkiikadhibisha. Na inawatuza
wachamngu katika maskani zao za Mabustanini na mito, katika makao mazuri kwa
Mfalme Mwenye uweza.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Saa imekaribia, na mwezi umepasuka!
2. Na wakiona Ishara hugeuka upande na husema: Huu uchawi
tu unazidi kuendelea.
3. Na wamekanusha na wamefuata matamanio yao. Na kila jambo ni lenye kuthibiti.
4. Na bila ya
shaka zimewajia khabari zenye makaripio.
5. Hikima
kaamili; lakini maonyo hayafai kitu!
6. Basi
jiepushe nao. Siku atakapo ita mwitaji kuliendea jambo linalo chusha;
7. Macho
yao yatainama; watatoka makaburini kama nzige walio tawanyika,
8.
Wanamkimbilia mwitaji, na makafiri wanasema: Hii ni siku ngumu.
9. Kabla
yao kaumu ya Nuhu walikanusha; wakamkanusha mja wetu, na wakasema ni
mwendawazimu, na akakaripiwa.
10. Basi
akamwomba Mola wake Mlezi akasema: Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru!
11. Basi
tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayo miminika.
12. Na
tukazipasua ardhi kwa chemchem, yakakutana maji kwa jambo lilio kadiriwa.
13. Na
tukamchukua kwenye safina ya mbao na kamba.
14.Ikawa inakwenda
kwa nadhari yetu, kuwa ni malipo kwa alivyo kuwa amekanushwa.
15. Na
bila ya shaka tuliiacha iwe ni Ishara. Lakini je, yupo anaye kumbuka?
16. Basi
ilikuwaje adhabu yangu, na maonyo yangu.
17. Na bila
ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anaye
kumbuka?
18. Kina
A'di walikanusha. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu?
19. Hakika
Sisi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku korofi mfululizo,
20.
Ukiwang'oa watu kama vigogo vya mitende vilio ng'olewa.
21. Basi
ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu?
22. Na
bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani nyepesi kufahamika; lakini yupo anaye
kumbuka?
23.
Thamudi waliwakanusha Waonyaji.
24.
Wakasema: Ati tumfuate binaadamu mmoja katika sisi? Basi hivyo sisi tutakuwa
katika upotofu na kichaa!
25. Ni
yeye tu aliye teremshiwa huo ukumbusho kati yetu sote? Bali huyu ni mwongo
mwenye kiburi!
26. Kesho
watajua ni nani huyo mwongo mwenye kiburi.
27. Hakika
Sisi tutawapelekea ngamia jike ili kuwajaribu, basi watazame tu na ustahamili.
28. Na
waambie kwamba maji yatagawanywa baina yao; kila sehemu ya maji itahudhuriwa na
aliye khusika.
29. Basi
wakamwita mtu wao akaja akamchinja.
30. Basi
ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu!
31. Hakika
Sisi tuliwapelekea ukelele mmoja tu, wakawa kama mabuwa ya kujengea uwa.
32. Na
bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani iwe nyepesi kwa kukumbuka, lakini yupo
akumbukaye?
33. Kaumu
Lut'i nao waliwakadhibisha Waonyaji.
34. Hakika
Sisi tukawapelekea kimbunga cha vijiwe, isipo kuwa wafuasi wa Lut'i. Hao
tuliwaokoa karibu na alfajiri.
35. Kwa
neema inayo toka kwetu. Hivyo ndivyo tumlipavyo anaye shukuru.
36. Na
hakika yeye aliwaonya adhabu yetu; lakini wao waliyatilia shaka hayo maonyo.
37. Na
walimtaka awape wageni wake. Tukayapofua macho yao, na tukawaambia: Onjeni basi
adhabu na maonyo yangu!
38. Na
iliwafikia wakati wa asubuhi adhabu yangu ya kuendelea.
39. Basi onjeni adhabu na maonyo yangu!
40. Na hakika tumeisahilisha Qur'ani kuikumbuka. Lakini
yupo anaye kumbuka?
41. Na Waonyaji waliwafikia watu wa Firauni.
42. Walizikadhibisha Ishara zetu zote, nasi tukawashika
kama anavyo shika Mwenye nguvu Mwenye uweza.
43. Je! Makafiri wenu ni bora kuliko hao, au yameandikwa
vitabuni kuwa nyinyi hamtiwi makosani?
44. Au ndio wanasema: Sisi ni wengi tutashinda tu.
45. Wingi wao huu utashindwa, na wao watasukumwa nyuma.
46. Bali Saa ya Kiyama ndio miadi yao, na Saa hiyo ni nzito
zaidi na chungu zaidi.
47. Hakika wakosefu wamo katika upotofu na wazimu.
48. Siku watakapo kokotwa Motoni kifudifudi waambiwe:
Onjeni mguso wa Jahannamu!
49. Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo.
50. Na amri yetu haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa
jicho.
51. Na bila ya shaka tumekwisha waangamiza wenzenu. Lakini
yupo anaye kumbuka?
52. Na kila jambo walilo lifanya limo vitabuni.
53. Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa.
54. Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na mito.
55. Katika makalio ya haki kwa Mfalme Mwenye uweza.
|