57. SURAT AL-H'ADIID
(Imeteremka
Madina)
Sura hii imeanzia kwa kueleza
kwamba wote walioko mbinguni na katika ardhi wamemsabihi na kumtakasa Mwenyezi
Mungu Mtukufu na kila kisicho kuwa laiki naye. Kisha ikafuatiliza hayo kwa
kuelekeana na kusabihi huko ufalme wa mbingu na ardhi, na kuvizunguka vyote
hivyo na kuviendesha. Kisha Sura ikaamrisha Imani ya Mwenyezi Mungu, na kutoa
katika njia yake, na ikabainisha khitilafu za daraja za kutoa kwa mujibu wa
kukhtalifiana haja ziliopo na dharura zake. Kisha ikaeleza sura ya Waumini Siku
ya Kiyama, inavyo tangulia nuru yao mbele yao na pembezoni mwao; na sura ya
wanafiki wanavyo waomba Waumini wawangojee ili nao wapate mwangaza kutokana na
nuru yao. Na baina yao umesimamishwa ukuta wenye mlango. Ndani yake ipo rehema,
na nje yake upande wa mbele yake ni adhabu.
Na Sura ikaingia baada ya hayo kuwahimiza Waumini wanyenyekee kwa kumkumbuka
Mwenyezi Mungu, na Haki aliyo iteremsha. Na inawaonyesha vyeo vya wanao sadiki
wanaume na wanawake mbele ya Mola wao Mlezi; na mwisho wa Makafiri wanao
kadhibisha ni katika Jahannamu. Na inapiga mifano ya udhalili wa dunia na hizo
starehe zake, na ukubwa wa Akhera na neema na adhabu zilioko huko. Na Sura
inataka watu wawanie kushindania maghfira kwa Mwenyezi Mungu, na inazituza
nafsi kwamba kila kinacho msibu mtu ikiwa kheri au shari kimeandikwa katika
Kitabu kilichoko kwa Mwenyezi Mungu, ili nyoyo zinyenyekee kwa hukumu ya
Mwenyezi Mungu. Kisha ikasimulia khabari za kuwatuma Mitume na kuwafuatiliza
mmoja baada ya mmoja wakipewa nguvu kwa hoja na Vitabu, na njia za nguvu na
vitendo, ili watu wasimamishe uadilifu. Kisha Aya ikakhitimisha kwa kuwaita
Waumini wamche Mungu, na ikawaahidi kuwa watapewa rehema maradufu na
watafanyiwa hisani ya kufadhiliwa, ambayo hapana mwenye kuiweza hata kidogo ila
Mwenyezi Mungu. Kwani hakika fadhila zote zimo katika mkono wa Mwenyezi Mungu,
humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kuu.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1.Kinamsabihi
kumtakasa Mwenyezi Mungu kila kiliomo ndani ya mbingu na ardhi. Na Yeye
ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
2. Yeye ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Anahuisha
na anafisha. Na Yeye ni Mwenye uweza wa kila kitu.
3. Yeye ndiye wa Mwanzo na ndiye wa Mwisho, naye ndiye wa
Dhaahiri na wa Siri, naye ndiye Mjuzi wa kila kitu.
4. Yeye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi katika siku
sita; kisha akakaa vyema juu ya enzi. Anayajua yanayo ingia katika ardhi na
yanayo toka humo, na yanayo teremka kutoka mbinguni, na yanayo panda humo. Naye
yu pamoja nanyi popote mlipo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona mnayo
yatenda.
5. Ufalme wa mbingu na ardhi ni wake. Na mambo yote
yanarejeshwa kwa Mwenyezi Mungu.
6. Anaingiza usiku katika mchana, na anaingiza mchana
katika usiku. Na Yeye ni Mwenye kuyajua yaliomo vifuani.
7. Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; na toeni katika
alivyo kufanyeni nyinyi kuwa ni waangalizi wake. Basi walio amini miongoni
mwenu, na wakatoa, wana malipo makubwa.
8. Na mna nini hata hamumuamini Mwenyezi Mungu na hali
Mtume anakuiteni mumuamini Mola wenu Mlezi? Naye amekwisha chukua ahadi yenu,
ikiwa nyinyi ni Waumini.
9. Yeye ndiye anaye mteremshia mja wake Aya zinazo bainisha
wazi ili akutoeni gizani muingie kwenye nuru. Na hakika Mwenyezi Mungu kwenu ni
Mpole, Mwenye kurehemu.
10. Na mna nini hata hamtoi katika Njia ya Mwenyezi Mungu,
na hali urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu? Hawawi sawa miongoni
mwenu wenye kutoa kabla ya Ushindi na wakapigana vita. Hao wana daraja kubwa
zaidi kuliko wale ambao walio toa baadae na wakapigana. Na wote hao Mwenyezi
Mungu amewaahidia wema. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
11. Ni nani atakaye mkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema,
ili amrudishie mardufu, na apate malipo ya ukarimu.
12. Siku utakapo waona Waumini wanaume na Waumini wanawake,
nuru yao iko mbele yao, na kuliani kwao: Furaha yenu leo - Bustani zipitazo
mito kati yake mtakaa humo milele. Huko
ndiko kufuzu kukubwa.
13. Siku
wanaafiki wanaume na wanaafiki wanawake watapo waambia walio amini: Tungojeni
ili tupate mwangaza katika nuru yenu. Waambiwe: Rejeeni nyuma yenu mkaitafute
nuru! Utiwe baina yao ukuta wenye mlango - ndani yake mna rehema, na nje upande
wake wa mbele kuna adhabu.
14. Watawaita
wawaambie: Kwani vile hatukuwa pamoja nanyi? Watawaambia: Ndiyo, lakini
mlijifitini wenyewe, na mkasitasita, na mkatia shaka, na matamanio ya nafsi
zenu yakakudanganyeni. mpaka ilipo kuja amri ya Mwenyezi Mungu, na mdanganyifu
akakudanganyeni msimfuate Mwenyezi Mungu.
15. Basi leo
haitapokelewa kwenu fidia, wala kwa wale walio kufuru. Makaazi yenu ni Motoni,
ndio bora kwenu; na ni marejeo maovu yalioje!
16. Je! Wakati
haujafika bado kwa walio amini zikanyenyekea nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi
Mungu na haki iliyo teremka? Wala wasiwe kama walio pewa Kitabu kabla yao, muda
wao ukawa mrefu, kwa hivyo nyoyo zao zikawa ngumu, na wengi wao wakawa
wapotovu.
17. Jueni kwamba
Mwenyezi Mungu huifufua ardhi baada ya kufa kwake. Tumekubainishieni
Ishara ili mpate kuzingatia.
18. Kwa hakika wanaume wanao toa sadaka, na wanawake wanao
toa sadaka, na wakamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, watazidishiwa mardufu
na watapata malipo ya ukarimu.
19. Na walio muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, hao
ndio Masidiqi na Mashahidi mbele ya Mola wao Mlezi. Wao watapata malipo yao na
nuru yao. Na walio kufuru na wakakadhibisha Ishara zetu, hao ndio watu wa
Motoni.
20. Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo, na pumbao,
na pambo, na kujifakhirisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na
watoto. Mfano wake ni kama mvua ambayo huwafurahisha wakulima mimea yake, kisha
hunyauka ukayaona yamepiga manjano kisha yakawa mabua. Na akhera kuna adhabu
kali na maghfira kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi. Na maisha ya dunia si
chochote ila ni starehe ya udanganyifu.
21. Kimbilieni msamaha wa Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo
upana wake ni kama upana wa mbingu na ardhi, iliyo wekewa walio muamini
Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa
amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu.
22. Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwisha
andikwa katika Kitabu kabla hatujauumba. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni
mepesi.
23. Ili msihuzunike kwa kilicho kupoteeni, wala msijitape
kwa alicho kupeni. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye jivuna
akajifakhirisha.
24. Ambao wanafanya ubakhili, na wanaamrisha watu wafanye
ubakhili. Na anaye geuka, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.
25. Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi,
na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu, na
tumeteremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu, na ili Mwenyezi
Mungu amjue anaye mnusuru Yeye na Mitume wake kwa ghaibu. Hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwenye nguvu Mwenye kushinda.
26. Na bila ya shaka tulimtuma Nuhu na Ibrahim, na tukaweka
katika dhuriya zao Unabii na Kitabu. Basi wapo miongoni mwao walio ongoka, na
wengi katika wao ni wapotovu.
27. Tena tukafuatisha nyuma yao Mitume wengine, na
tukamfuatisha Isa bin Mariamu, na tukampa Injili. Na tukajaalia katika nyoyo za
walio mfuata upole na rehema. Na umonaki (utawa wa mapadri) wameuzua wao. Sisi
hatukuwaandikia hayo, ila kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Lakini hawakuufuata
inavyo takiwa kuufuata. Basi wale walio amini katika wao tuliwapa ujira wao. Na
wengi wao ni wapotovu.
28. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na muaminini
Mtume wake, atakupeni sehemu mbili katika rehema yake, na atakujaalieni muwe na
nuru ya kwenda nayo. Na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe,
Mwenye kurehemu.
29. Ili watu wa Kitabu wajue kwamba wao hawana uweza wowote
juu ya fadhila za Mwenyezi Mungu. Na fadhila zote zimo mikononi mwa Mwenyezi
Mungu. Humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kuu.
|