58. SURAT AL-MUJAADALAH
(Imeteremka
Madina)
Sura
imeanza kwa kueleza khabari za mwanamke anaye tengwa na mumewe, na ikafuatia
kubainisha hukumu za kutengana. Na Mwenyezi Mungu katika sura hii katika zaidi
ya Aya moja amewatia makosani wanao ifanyia uadui Dini yake, na amewahadharisha
na kunong'ona nong'ona kwa ajili ya madhambi na uadui. Na amewaongoza Waumini
juu ya adabu za kunong'ona baina yao kwa wao, na baina yao na Mtume s.a.w. Kama
vile vile alivyo watia makosani wanaafiki kwa kushirikiana na makafiri, na
akawaeleza kuwa hao ni kundi la Shetani lenye kuingia khasarani.
Na Sura ikakhitimisha kwa kueleza kwa jumla yaliyo ya waajibu juu ya Waumini ya
kupendelea kumridhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake kuliko wengine wasio kuwa wao,
hata wangeli kuwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Na
akawasifu Waumini hao kuwa ni Hizbu-Llahi, Kundi la Mwenyezi Mungu, lenye
kufanikiwa.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. MWENYEZI MUNGU amekwisha sikia usemi wa mwanamke anaye
jadiliana nawe juu ya mumewe, na anamshitakia Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu
anayasikia majibizano yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye
kuona.
2. Wale miongoni mwenu wanao watenga wake zao, hao si mama
zao. Hawakuwa mama zao ila wale walio wazaa. Na hakika hao wanasema neno linalo
chusha, na la uwongo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kughufiria, Mwenye kusamehe.
3. Na wale wanao jitenga na wake zao, kisha wakarudia
katika yale waliyo yasema, basi wamkomboe mtumwa kabla hawajagusana. Mnapewa
maonyo kwa hayo. Na Mwenyezi Mungu anayajua yote mnayo yatenda.
4. Na asiye pata mtumwa kumkomboa, basi na afunge miezi
miwili mfululizo kabla hawajagusana. Na asiye weza hayo basi awalishe masikini
sitini. Hayo ni hivyo ili mumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na hiyo ndiyo
mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na kwa makafiri iko adhabu chungu.
5. Hakika wanao pinzana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake,
watadhalilishwa kama walivyo dhalilishwa wale walio kuwa kabla yao. Na
tulikwisha teremsha Ishara zilizo wazi. Na makafiri watapata adhabu ya kufedhehesha.
6. Siku atapo wafufua Mwenyezi Mungu, na awaambie yale
waliyo yatenda. Mwenyezi Mungu ameyadhibiti, na wao wameyasahau! Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kushuhudia kila kitu.
7. Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu anajua vilivyomo
katika mbingu na vilivyomo katika ardhi? Hauwi mnong'ono wa watu watatu ila
Yeye huwa ni wane wao, wala wa watano ila Yeye huwa ni wa sita wao. Wala wa
wachache kuliko hao, wala walio wengi zaidi, ila Yeye yu pamoja nao popote pale
walipo. Kisha Siku ya Kiyama atawaambia waliyo yatenda. Hakika Mwenyezi Mungu
ni Mjuzi wa kila kitu.
8. Kwani huwaoni wale walio katazwa kunong'onezana kisha
wakayarudia yale yale waliyo katazwa, na wakanong'ona juu ya mambo ya dhambi,
na ya uadui, na ya kumuasi Mtume? Na wakikujia hukuamkia sivyo anavyo kuamkia
Mwenyezi Mungu. Na husema katika nafsi zao: Mbona Mwenyezi hatuadhibu kwa haya
tuyasemayo? Basi Jahannamu itawatosha; wataingia humo! Na hayo ndiyo marejeo
maovu yaliyoje!
9. Enyi mlio amini! Mnapo nong'ona msinong'one kwa sababu
ya mambo ya madhambi, na uadui, na kumuasi Mtume. Bali nong'onezane kwa kutenda
mema na kuacha maovu. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwake mtakusanywa nyote.
10. Kwa hakika minong'ono hiyo inatokana na Shetani ili
awahuzunishe walio amini, na wala haitawadhuru chochote ila kwa idhini ya Mwenyezi
Mungu. Na juu ya Mwenyezi Mungu tu ndio wategemee Waumini.
11. Enyi mlio amini! Mkiambiwa: Fanyeni nafasi katika
mabaraza, basi fanyeni nafasi. Na Mwenyezi Mungu atakufanyieni nyinyi nafasi.
Na mkiambiwa: Ondokeni, basi ondokeni. Mwenyezi Mungu atawainua walio amini
miongoni mwenu, na walio pewa ilimu daraja za juu. Na Mwenyezi Mungu anazo
khabari za mnayo yatenda.
12. Enyi mlio amini! Mnapo sema siri na Mtume, basi
tangulizeni sadaka kabla ya kusemezana kwenu. Hiyo ni kheri kwenu na usafi
zaidi. Na ikiwa hamkupata cha kutoa, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe,
Mwenye kurehemu.
13. Mnachelea kutanguliza hiyo sadaka kabla ya kusemezana
kwenu? Ikiwa hamkufanya hayo, na Mwenyezi Mungu akapokea toba yenu, basi
shikeni Sala, na toeni Zaka, na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na
Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
14. Huwaoni wale walio fanya urafiki na watu ambao Mwenyezi
Mungu amewakasirikia? Hao si katika
nyinyi, wala si katika wao. Na huapa kwa uwongo, na hali kuwa wanajua.
15. Mwenyezi
Mungu amewaandalia adhabu kali. Kwa hakika waliyo kuwa wakiyatenda ni maovu
kabisa.
16. Wamefanya
viapo vyao ni ngao, na wakaipinga Njia ya Mwenyezi Mungu. Basi hao watapata
adhabu ya kufedhehesha.
17. Hayatawafaa
kitu mali yao wala watoto wao mbele ya Mwenyezi Mungu. Hao ndio watu wa Motoni.
Humo watadumu milele.
18. Siku atakayo
wafufua Mwenyezi Mungu wote, wamuwapie kama wanavyo kuwapieni nyinyi. Na
watadhani kuwa wamepata kitu! Kwa hakika hao ndio waongo.
19. Shetani
amewatawala na akawasahaulisha kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hao ndio kundi
la Shetani. Kweli hakika kundi la Shetani ndilo lenye kukhasirika.
20. Hakika wanao mpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hao
ndio miongoni mwa madhalili wa mwisho.
21. Mwenyezi Mungu ameandika: Hapana shaka Mimi na Mtume
wangu tutashinda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.
22. Huwakuti watu wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya
Mwisho kuwa wanawapenda wanao mpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa
ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao ameandika katika
nyoyo zao Imani, na amewapa nguvu kwa Roho itokayo kwake. Na atawaingiza katika
Mabustani yapitayo mito kati yake. Humo watakaa daima. Mwenyezi Mungu awe radhi
nao, na wao wawe radhi naye. Hao ndio Hizbullahi, Kundi la Mwenyezi Mungu.
Hakika Kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufanikiwa.
|