62. SURAT AL-JUMUA'
(Imeteremka
Madina)
Imefunguka Sura hii kwa
kutoa khabari yake Mtukufu kwamba viliomo katika mbingu na ardhi vyote
vinamsabihi Yeye. Na Mwenyezi Mungu aliye tukuka shani yake amesema kwamba
ameineemesha kaumu isio jua kuandika wala kusoma kwa kuwaletea Mtume miongoni
mwao, ambaye anawafundisha Kitabu, na hikima, na anawatakasa. Na hakika hii ni
fadhila ya Mwenyezi Mungu humpa amtakaye.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amewakemea Mayahudi kwa kuacha kwao kutenda yaliyo
amrishwa katika Taurati, na hali wao wanajua yaliomo humo. Na amepinga madai
yao kwamba wao peke yao ndio vipenzi vya Mwenyezi Mungu, si watu wenginewe. Na
amebariziana nao kwa kuwataka watamani kufa ikiwa wao wanasema kweli! Na Sura
imekhitimisha kwa kuwaamrisha Waumini wakimbilie kwenda sali Sala ya Ijumaa
pindi wakisikia adhana, na waache biashara. Na Sala ikisha malizika watawanyike
katika nchi wende kutafuta fadhila za Mwenyezi Mungu. Na kawakataza wasiache
biashara au jambo la pumbao lolote kuwashughulisha wasiisikilize khutba ya
Ijumaa. Na Mwenyezi Mungu amewadhamini kuwaruzuku, na Yeye ndiye mbora wa
kuruzuku.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi vinamtakasa
Mwenyezi Mungu, Mfalme, Mtakatifu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
2. Yeye ndiye aliye mpeleka Mtume kwenye watu wasio jua
kusoma, awasomee Aya zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, ijapo
kuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri.
3. Na kwa wengine ambao bado hawajaungana nao. Na Yeye
ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
4. Hiyo ni fadhila ya Mwenyezi Mungu anayo mpa amtakaye. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa.
5. Mfano wa walio bebeshwa Taurati kisha wasiibebe, ni
mfano wa punda anaye beba vitabu vikubwa vikubwa. Mfano muovu mno wa watu walio
kadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu
madhaalimu.
6. Sema: Enyi mlio Mayahudi! Ikiwa nyinyi mnadai kuwa ni
vipenzi vya Mwenyezi Mungu pasipo kuwa watu wengine, basi yatamanini mauti,
ikiwa mnasema kweli.
7. Wala hawatayatamani kabisa, kwa sababu ya iliyo kwisha
yatanguliza mikono yao. Na Mwenyezi Mungu anawajua walio dhulumu.
8. Sema: Hayo mauti mnayo yakimbia, bila ya shaka
yatakukuteni. Kisha mtarudishwa kwa Mwenye kuyajua yaliyo fichikana na yanayo
onekana. Hapo atakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
9. Enyi mlio amini! Ikiadhiniwa Sala siku ya Ijumaa,
nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara. Hayo ni
bora kwenu, lau kama mnajua.
10. Na itakapo kwisha Sala, tawanyikeni katika nchi mtafute
fadhila za Mwenyezi Mungu, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate kufanikiwa.
11. Na wanapo iona biashara au pumbao wanayakimbilia hayo
na wakakuacha umesimama. Sema: Yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko pumbao
na biashara. Na Mwenyezi Mungu ni Mbora wa watoa riziki.
|