63. SURAT AL-MUNAAFIQUN
(Imeteremka
Madina)
Sura hii imekusanya kikundi
cha sifa za wanaafiki; ikataja kwamba hao hutangaza imani yao kwa ndimi zao
bila ya kuwa wanasema kweli. Na ikabainisha kwamba wanafanya yamini zao za uwongo
kuwa ni kinga wasiambiwe kuwa ni makafiri, ambao kwa hakika ndivyo walivyo na
ndivyo watakavyo lipwa hivyo. Pia imebainisha kuwa hao wanaafiki wana umbo zuri
la kumpendeza anao waona, na wana ufasihi mzuri wa kusikilizwa. Na juu ya
hivyo, nyoyo zao zi tupu, hazina Imani ndani yake. Wao ni kama magogo yaliyo
egemezwa, yasiyo na uhai.
Na Sura inaelezea kuwa wakiitwa ili Mtume wa Mwenyezi Mungu awaombee maghfira,
hali yao hubainika kwa kuwa hutakabari, na hudhihirisha kukataa kwao kuitikia,
nao wanajivuna.
Kisha Sura ikaingia kutaja madai ya wanaafiki kwamba wao ati ndio watukufu
wenye nguvu, na Waumini ni madhalili; na ahadi walio waahidi Waumini kuwa
watawatoa mji wakisha rejea Madina. Sura imebainisha wepi katika makundi mawili
hayo walio watukufu na wenye nguvu.
Na khatimaye Sura inaelekeza kuwasemeza Waumini watoe kwa ajili ya Njia ya
Mwenyezi Mungu, wafanye haraka kwa hayo kabla mauti hayajamfikia mmoja wao,
akajuta, na akatamani laiti inge akhirishwa ajali yake. Na wala Mwenyezi Mungu
hamuakhirishi yeyote ikisha fika ajali yake.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Wanapo kujia wanaafiki husema: Tunashuhudia ya kuwa wewe
ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa wewe ni Mtume wa
Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu anashuhudia ya kuwa hakika wanaafiki ni
waongo.
2. Wamevifanya viapo vyao ni kinga, na wao wakajizuia
kuifuata Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika ni mabaya kabisa waliyo kuwa
wakiyafanya.
3. Hayo ni kwa sababu ya kuwa waliamini, kisha wakakufuru;
kwa hivyo umepigwa muhuri juu ya nyoyo zao. Kwa hivyo hawafahamu lolote.
4. Na unapo waona, miili yao inakupendeza, na wakisema,
unasikiliza usemi wao. Lakini wao ni kama magogo yaliyo egemezwa. Wao hudhania
kila ukelele unao pigwa ni kwa ajili yao. Hao ni maadui; tahadhari nao.
Mwenyezi Mungu awaangamizilie mbali! Vipi wanapotoka na haki?
5. Na wanapo ambiwa: Njooni ili Mtume wa Mwenyezi Mungu
akuombeeni maghfira, huvigeuza vichwa vyao, na unawaona wanageuka nao wamejaa
kiburi.
6. Sawa sawa kwao, ukiwatakia maghfira au hukuwatakia
maghfira, Mwenyezi Mungu hatawaghufiria. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu
wapotovu.
7. Hao ndio wanao sema: Msitoe mali kwa ajili ya walioko
kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ili waondokelee mbali! Na Mwenyezi Mungu ndiye
Mwenye khazina za mbingu na ardhi, lakini wanaafiki hawafahamu.
8. Wanasema: Tukirejea Madina mwenye utukufu zaidi bila ya
shaka atamfukuza aliye mnyonge. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu - Yeye,
na Mtume wake, na Waumini. Lakini wanaafiki hawajui.
9. Enyi mlio amini! Yasikusahaulisheni mali yenu, wala
watoto wenu, kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Na wenye kufanya hayo ndio walio
khasiri.
10. Na toeni katika tulicho kupeni kabla hayajamfikia mmoja
wenu mauti, tena hapo akasema: Mola wangu Mlezi! Huniakhirishi muda kidogo
nipate kutoa sadaka, na niwe katika watu wema?
11. Wala Mwenyezi Mungu hataiakhirisha nafsi yoyote inapo
fika ajali yake; na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
|