64. SURAT ATTAGHAABUN
(Imeteremka
Madina)
Imeanzia Sura hii kwa
kueleza kuwa kila kiliomo katika mbingu na katika ardhi kinamtakasa Mwenyezi
Mungu na kisio laiki na utukufu wake, na kwamba Yeye ndiye Mwenye Ufalme na
Mwenye sifa njema zote, na kwamba Yeye ni Muweza wa kila kitu. Kisha hayo
yakafuatilizwa na kutajwa baadhi ya dalili za utimilivu wa uweza wake na ujuzi
wake. Kisha Sura ikatupa macho kuwaangalia makafiri walio kuwa kabla ya hawa,
na wakawaasi Mitume wa Mola wao Mlezi, na kwamba wao walionja matokeo maovu ya
vitendo vyao. Na hayo yalikuwa hivyo kwa sababu Mitume wao walipo kuwa
wakiwajia kwa hoja, waliwakataa na wakawapuuza! Sura tena ikaingia baada ya
hayo kuvunja madai ya makafiri kwamba wao ati hawatafufuliwa. Na ikawataka watu
wamuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na Nuru iliyo teremshwa juu yake. Na
ikawahadharisha na Siku ya Mkusanyo, siku kutapo dhihiri kupunjana kwa watu.
Kwani wale walio amini na wakatenda mema watapata kufuzu kukubwa, na walio
kufuru ndio watakuwa watu wa Motoni, na hayo ndiyo marudio maovu. Na hakika
masaibu yatakuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na hakika mwenye kumuamini
Mwenyezi Mungu ndio anauongoa moyo wake.
Sura inawataka watu wamt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Wakipuuza, basi
hakika Mtume hana juu yake ila kufikisha Ujumbe. Na inawaambia Waumini kuwa
mali yao na watoto wao ni fitna, majaribio. Basi isiwe kuyashughulikia hayo
kukawapelekea kuacha waliyo amrishwa. Kisha ikawaamrisha wamche Mwenyezi Mungu
kwa kadri wawezavyo. Na Sura ikakhitimisha kwa kuwakhusisha Waumini watoe
katika njia za kheri, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushukuru, Mpole,
Mjuzi wa yaliyo fichikana na yanayo onekana. Basi atawalipa kwa mali yao wanayo
yatumia. Na kwamba Yeye ni Mwenye nguvu asiye shindika, Mwenye hikima, hafanyi
upuuzi.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Kinamtakasa Mwenyezi Mungu kila kilichomo katika mbingu
na katika ardhi. Ufalme ni wake, na sifa njema ni zake. Na Yeye ni Mwenye uweza
juu ya kila kitu.
2. Yeye
ndiye aliye kuumbeni. Miongoni mwenu yupo aliye kafiri, na yupo aliye Muumini.
Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
3.
Ameziumba mbingu na ardhi kwa haki, na akakupeni sura, na akazifanya nzuri sura
zenu. Na marudio ni kwake.
4. Anajua
viliomo katika mbingu na ardhi, na anajua mnayo yaficha na mnayo yatangaza. Na
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliomo vifuani.
5. Kwani
haikukujieni khabari ya walio kufuru kabla, wakaonja matokeo mabaya ya mambo
yao? Na wao wana adhabu iliyo chungu.
6. Hayo ni
kwa kuwa walikuwa wakiwajia Mitume wao kwa hoja zilizo wazi, nao wakasema:
Hivyo binaadamu ndio atuongoe? Basi wakakufuru, na wakageuka upande. Mwenyezi Mungu
akawa hana haja nao. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, si mhitaji, naye ni Msifiwa.
7. Walio
kufuru wanadai kuwa hawatafufuliwa. Sema: Kwani? Naapa kwa Mola wangu Mlezi!
Hapana shaka mtafufuliwa, na kisha hapana shaka mtaambiwa mliyo yatenda. Na
hayo ni mepesi kwa Mwenyezi Mungu.
8. Basi
muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na Nuru tuliyo iteremsha. Na Mwenyezi
Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
9. Siku
atakayo kukusanyeni kwa ajili ya Siku ya Mkusanyiko; hiyo ni siku ya kupunjana.
Na anaye muamini Mwenyezi Mungu na akatenda mema, atamfutia maovu yake, na
atamuingiza katika Mabustani yenye kupitiwa kati yake na mito, watadumu humo
milele. Huko ndiko kufuzu
kukubwa.
10. Na walio
kufuru na wakakadhibisha Ishara zetu, hao ni watu wa Motoni, watadumu humo
milele. Na hayo ndiyo marudio mabaya.
11. Haufiki msiba wowote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu huuongoa moyo wake. Na Mwenyezi Mungu ni
Mjuzi wa kila kitu.
12. Na mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume. Mkigeuka,
basi hakika juu ya Mtume wetu ni kufikisha (Ujumbe wake) kwa uwazi tu.
13.
Mwenyezi Mungu, hapana mungu isipo kuwa Yeye. Na juu ya Mwenyezi Mungu
nawategemee Waumini.
14. Enyi mlio amini! Hakika miongoni mwa wake zenu na
watoto wenu wamo maadui zenu. Basi tahadharini nao. Na mkisamehe, na mkapuuza,
na mkaghufiria basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, Mwenye
kurehemu.
15. Hakika mali yenu na watoto wenu ni jaribio. Na kwa
Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa.
16. Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo, na sikieni,
na t'iini, na toeni, itakuwa kheri kwa nafsi zenu. Na mwenye kuepushwa na
uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio walio fanikiwa.
17. Mkimkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri, atakuzidishieni
mardufu, na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa shukra, Mpole.
18. Mwenye kujua siri na dhaahiri, Mwenye nguvu, Mwenye
hikima.
|