65. SURAT ATT'ALAAQ
(Imeteremka
Madina)
Sura
hii inaeleza baadhi ya hukumu za talaka, na eda, na namna zake, na hukumu zake
- tangu kubaki mwenye eda katika nyumba aliyo pewa talaka ndani yake, na
waajibu wa kumtazama kwa matumizi, na maskani. Na kati ya hukumu hizi, kama
ilivyo mwendo wa Qur'ani, ipo ahadi kwa mwenye kufuata amri za Mwenyezi Mungu,
na onyo kwa mwenye kukiuka mipaka yake. Kisha Sura imeashiria malipo ya wenye
kutakabari wakakataa kutimiza amri za Mwenyezi Mungu na Watume wake. Na
ikakhitimisha Sura kwa kuwahimiza Waumini wamche Mwenyezi Mungu, na
kuwakumbusha neema za kuwapelekea Mtume anaye wasomea Aya za Mwenyezi Mungu,
ili awatoe kwenye giza wende kwenye mwangaza, na kwa uweza wake Mwenyezi Mungu
kuziumba mbingu saba, na katika ardhi mfano wa hizo.
KWA JINA LA MWENYEZI
MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. Ewe
Nabii! Mtakapo wapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wa eda
zao. Na fanyeni hisabu ya eda. Na mcheni Mwenyezi Mungu, Mola wenu
Mlezi. Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya jambo
la uchafu ulio wazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu, msiikiuke. Na mwenye
kuikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi amejidhulumu nafsi yake. Hujui; labda
Mwenyezi Mungu ataleta jambo jengine baada ya haya.
2. Basi wanapo fikia muda wao, ima warejeeni muwaweke kwa
wema, au farikianeni nao kwa wema. Na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu
miongoni mwenu. Na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Hivyo
ndivyo anavyo agizwa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na anaye
mcha Mwenyezi Mungu humtengezea njia ya kutokea.
3.Na humruzuku kwa jiha asiyo tazamia. Na anaye mtegemea Mwenyezi
Mungu Yeye humtosha. Hakika Mwenyezi Mungu anatimiza amri yake. Mwenyezi Mungu
kajaalia kila kitu na kipimo chake.
4. Na wale walio sita hedhi miongoni mwa wanawake wenu,
ikiwa mnayo shaka, basi muda wa eda yao ni miezi mitatu, pamoja na ambao
hawapati hedhi. Na wenye mimba eda yao mpaka watakapo zaa. Na anaye mcha
Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu humfanyia mambo yake kuwa mepesi.
5. Hiyo ni amri ya Mwenyezi Mungu amekuteremshieni. Na
anaye mcha Mwenyezi Mungu atamfutia maovu yake, na atampa ujira mkubwa.
6. Wawekeni humo humo mnamo kaa nyinyi kwa kadiri ya pato
lenu, wala msiwaletee madhara kwa kuwadhiki. Na wakiwa wana mimba, wagharimieni
mpaka wajifungue. Na wakikunyonyesheeni, basi wapeni ujira wao, na shaurianeni
kwa wema. Na mkiona uzito kati yenu, basi amnyonyeshee mwanamke mwengine.
7. Mwenye wasaa atoe kadiri ya wasaa wake, na mwenye dhiki
atoe katika alicho mpa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu ila kwa
kadiri ya alicho mpa. Mwenyezi Mungu atajaalia baada ya dhiki faraji.
8. Na miji mingapi iliyo vunja amri ya Mola wake Mlezi na
Mitume wake, basi tuliihisabia hisabu ngumu na tukaiadhibu kwa adhabu kali.
9. Basi ikauonja ubaya wa mambo yake; na mwisho wa mambo
yao ilikuwa khasara.
10. Mwenyezi Mungu aliwaandalia adhabu kali. Basi mcheni Mwenyezi
Mungu, enyi wenye akili, mlio amini! Hakika Mwenyezi Mungu amekuteremshieni
Ukumbusho,
11. Mtume anaye kusomeeni Aya za Mwenyezi Mungu zinazo
bainisha, ili kuwatoa walio amini na wakatenda mema kutoka gizani kuwapeleka
kwenye nuru. Na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, na akatenda mema, atamwingiza
katika Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Mwenyezi Mungu
amekwisha mpa riziki nzuri.
12. Mwenyezi Mungu ni yule ambaye ameziumba mbingu saba, na
ardhi kwa mfano wa hizo. Amri zake zinashuka baina yao, ili mjue kwamba
Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu, na kwamba Mwenyezi Mungu
amekizunguka kila kitu kukijua vilivyo kwa ilimu yake.
|